Yanga yapita njia ya AC Milan

Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji

Muktasari:

  • Tangu Manji alipojipeleka polisi kuhojiwa kuhusu suala hilo, amekuwa chini ya ulinzi pamoja na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

Dar es Salaam. Bingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga inapita katika kipindi kigumu kiuchumi kutokana na mwenyekiti wake, Yusuf Manji kuingia kwenye matatizo tangu alipotajwa katika orodha ya watu wanajihusisha na dawa za kulevya.

Tangu Manji alipojipeleka polisi kuhojiwa kuhusu suala hilo, amekuwa chini ya ulinzi pamoja na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

Wakati Manji akikumbwa na maswahibu hayo, klabu yake ya Yanga nayo imepatwa na mtikisiko wa kiuchumi unaotishia kuweka rehani ubingwa wake wa Ligi Kuu pamoja na ndoto ya kucheza hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika wakijiandaa na mechi dhidi ya Zanaco ya Zambia, Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa.

Iwapo juhudi za haraka hazitachukuliwa kunusuru hali ya mambo, huenda Yanga ikakumbana na changamoto ya kutofanya vizuri kutokana na mazingira ambayo Manji aliwatengenezea vijana wake.

Taarifa za klabu hiyo kuyumba kifedha huku ilidaiwa kuwa kuna ucheleweshaji wa mishahara kwa wachezaji, ni mwendelezo wa changamoto ambazo klabu mbalimbali zinazotegemea nguvu ya mtu mmoja zimewahi kukutana nazo.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alikiri kuwa wana hali ngumu kifedha ndani ya klabu hiyo baada ya mwenyekiti wao Manji kukumbwa na matatizo na Serikali ikiwamo kufungwa kwa akaunti zake.

“Ukweli ulivyo ni kwamba, wachezaji wote wamelipwa mishahara yao isipokuwa mshahara mmoja tu wa mwezi wa nane mwaka jana na wameahidiwa watalipwa,” alisema Mkwasa.

Hivi karibuni, Yanga ilitangaza kuachana na aliyekuwa Mkurugenzi wake, Hans Pluijm ili kupunguza gharama zisizo na ulazima kutokana na mchango na nafasi ya Mzungu huyo kwenye kikosi chao kwa sasa.

Mshahara wa Pluijm ambaye alikuwa ni mkurugenzi wa ufundi ulikuwa ni Dola 10,000 kwa mwezi sanjari na marupurupu mengine ulikuwa unafikia kiasi cha Dola 15,000 ambazo ni zaidi ya Sh33.5 milioni.

Mbali na Pluijm, klabu hiyo pia iko mbioni kuwapa mkono wa kwaheri mastaa watatu ambao wanatajwa kuwa ndio vinara wa kulipwa ‘fedha ndefu’ kwenye kikosi chao kwa sasa.

Haruna Niyonzima anayetajwa kupokea Dola 4,000, pamoja na Vincent Bossou na Donald Ngoma wanatajwa kupokea Dola 3,500 kila mmoja, inadaiwa kuwa Yanga inataka kuwaondoa kikosini kutokana na matatizo ya kinidhamu, ingawa kwa kiasi kikubwa suala la fedha linaonekana kuwa chanzo. Ukiondoa Ngoma ambaye Yanga awali ilikuwa iko tayari kumwongezea mkataba, ugumu wa kuwaongezea mikataba Bossou na Niyonzima umekuja kutokana na mahitaji makubwa ya dau ambalo nyota hao wanataka.

Wakati mikataba yao inayomalizika wakisaini kwa dau linalotajwa kuwa Dola 60,000 (zaidi ya Sh122 milioni), nyota hao inasemekana wanataka dau kubwa zaidi ambalo Yanga haiko tayari kuwapa kwa sasa.

Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Ngaya Club De Mbe, Yanga ililazimika kwenda Comoro siku moja kabla ya mechi huku ikiwa na kikosi cha wachezaji 20 tu tofauti na hapo nyuma, jambo lililohusishwa moja kwa moja na hali ya ukata inayoikabili klabu.

Hata katika mchezo dhidi ya Simba, Yanga ambayo mara kwa mara ilijenga mazoea ya kuweka kambi kisiwani Pemba na kurudi kwa ndege jijini kila inapojiandaa na mechi hiyo, iliamua kuweka kambi yake Kigamboni eneo la Kimbiji tofauti na ilivyozoeleka.

Mwananchi imeangalia jinsi kashfa na matatizo ya matajiri zinavyoyumbisha klabu za soka duniani.

Silvio Berlusconi, AC Milan

Baada ya kutamba chini ya umiliki wa Silvio Berlusconi mwishoni mwa miaka ya 90 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, AC Milan ilikutana na anguko baada ya bilionea huyo kukutana na changamoto za kisiasa nchini Italia akiwa Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Italia, Berlusconi alipoteza nafasi yake ya kisiasa na kashfa ya kukwepa kodi pamoja kujihusisha kimapenzi na wasichana wenye umri mdogo jambo lililompoteza kabisa.

Matatizo hayo ya Berlusconi yaliingia katika timu ya AC Milan kiasi cha kushindwa kufanya vizuri katika Ligi Kuu Italia ya Serie A na mashindano ya Ulaya huku wakilazimika kuuza nyota wake.

Moise Katumbi (TP Mazembe)

Mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi aliteka vichwa vya habari alipoamua kujitosa katika siasa na kuwania urais wa DR Congo mwaka jana kabla ya uchaguzi huo kufutwa hadi Desemba mwaka huu.

Hata hivyo, uamuzi wake huo ulimwingiza matatizo na Serikali ya DR Congo iliyomshutumu kwa kuajili walinzi wageni kinyume sheria na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela. Lakini alikimbilia uhamishoni London.

Tangu Katumbi akimbie DR Congo klabu yake ya TP Mazembe imeshindwa kufanya usajili mkubwa na hivi karibuni walimrudisha mkongwe Tresor Mputu pia walipoteza mchezo katika fainali ya Super Cup Afrika baada ya Mamelodi Sundowns kuwalaza bao 1-0.

Tommaso Ghirardi, Parma

Mabingwa mara mbili wa Kombe la UEFA sasa Europa Ligi, Parma ilitangazwa mufilisi 2015 na kushushwa daraja kutoka Ligi Kuu hadi daraja la nne hiyo baada ya kukosa mmiliki mpya wa kuichukua timu hiyo.

Parma iliingia katika janga hilo baada ya rais wake Tommaso Ghirardi kushindwa kulipa mishahara pamoja na kushindwa kuiuza kwa tajiri mwingine wa Russia kutokana na mzingo wa madeni.

Wakati akiwa hajaweka sawa masuala hayo Ghirardi alikamatwa na polisi na kufungwa kwa makosa ya kugushi na kutakatisha fedha.

Klabu nyingine ambayo ilijikuta ikipotea kwenye ramani ya soka ni Fulham ambayo ilikuwa kiboko ya vigogo kwenye Ligi Kuu ya Uingereza ikitambia fedha za Bilionea Omary Al Fayed lakini baada ya mmiliki huyo kuyumba kiuchumi, klabu hiyo imeporomoka hadi Ligi Daraja la Pili.

Akizungumzia changamoto hiyo, mbunge wa Jimbo la Chemba, Juma Nkamia alisema kuwa suluhisho lake ni klabu kubadili mfumo wake wa uendeshaji na kuongozwa na bodi.

“Mpira wa kisasa unahitaji kuwa na mfumo ambao hautoi nafasi kwa watu wachache kuwa na sauti ya mwisho kwa sababu inapotokea wanapata tatizo wanayumbisha timu na inakuwa kwenye wakati mgumu.