Ndesamburo aacha rekodi mjini Moshi

Umati wa wananchi ukiwa kwenye foleni ya kwenda kutoa heshima ya mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo katika Uwanja wa Majengo, mjini Moshi, jana. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

  • Haijapata kutokea tangu Uhuru wa nchi hii kwa kiongozi kuagwa uwanjani na watu wengi kwani kumbukumbu zinaonyesha wote waliomtangulia ama waliagwa nyumbani kwao au katika makanisa waliyokuwa wakisali.
  • Awali, Ndesamburo alikuwa aagwe katika Uwanja vya Mashujaa ili kuakisi ushujaa wake wa kuwaletea maendeleo wananchi wa Moshi, lakini Serikali ilizuia.

Moshi. Mwili wa mbunge wa zamani wa Moshi Mjini kupitia Chadema (2000-2015), Philemon Ndesamburo jana uliweka rekodi ya aina yake mkoani Kilimanjaro kwa kuagwa na kuhudhuriwa na maelfu ya waombolezaji.

Haijapata kutokea tangu Uhuru wa nchi hii kwa kiongozi kuagwa uwanjani na watu wengi kwani kumbukumbu zinaonyesha wote waliomtangulia ama waliagwa nyumbani kwao au katika makanisa waliyokuwa wakisali.

Awali, Ndesamburo alikuwa aagwe katika Uwanja vya Mashujaa ili kuakisi ushujaa wake wa kuwaletea maendeleo wananchi wa Moshi, lakini Serikali ilizuia.

Hata hivyo, pamoja na kuzuia shughuli ya kufanya kumbukizi na kutoa heshima za mwisho katika uwanja huo na kuhamishia shughuli hiyo katika Uwanja wa Majengo, bado tukio hilo liliutikisa mji wa Moshi.

Mapema jeneza lililobeba mwili wake lilipangiwa kutembezwa katika mitaa na barabara mbalimbali za mji huo, lakini polisi ikazuia ikisema hayo yangekuwa ni sawa na maandamano. Hata jeshi hilo lilipoelekeza msafara huo utoke hospitali ya rufaa ya KCMC hadi Uwanja wa Majengo, bado barabarani watu walikusanyika kuuaga mwili huo hali iliyowapa wakati mgumu polisi.

Kuanzia saa 4:20 asubuhi, polisi wa kutuliza ghasia wakishirikiana na askari wa usalama barabarani, walianza kujipanga katika mzunguko wa magari wa YMCA ili msafara usiingie katikati ya mji.

Polisi hao wakiwa na magari matatu na silaha walijipanga na kuelekezana namna watakavyohakikisha msafara huo hauingii mjini kama jeshi hilo lilivyokuwa limetoa maelekezo.

Msafara ulipokaribia shule ya msingi J.K Nyerere (zamani Kibo) polisi walitumia mbinu ya kukamata magari ya kiraia na kuyatumia kuziba barabara inayoelekea mjini ili kuhakikisha hakuna gari linapita.

Kutokana na ukubwa wa msafara wa magari likiwamo lililobeba mwili wa Ndesamburo, barabara zote zinazoingia na kutoka katika mzunguko huo wa YMCA zilifungwa isipokuwa ya kuelekea Majengo.

Baadhi ya madereva waliokuwa wakienda barabara kuu ya Moshi-Dar es Salaam walilazimika kutumia barabara mbadala, ingawa hata huko mbele walikutana na vizuizi vya polisi wakiwamo wa usalama barabarani.

Msafara huo ulitanguliwa na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na kisha watembea kwa miguu ambao walitembea kuanzia maeneo ya madukani hadi Uwanja wa Majengo.

Mbali na pikipiki na watembea kwa miguu, msafara huo ulikuwa na magari zaidi ya 50 yaliyowabeba baadhi ya viongozi wa kitaifa ambao walilazimika kwenda mwendo sawa na wa watembea kwa miguu.

Mamia ya wananchi walijipanga katika barabara nzima kuanzia KCMC hadi Uwanja wa Majengo huku baadhi ya wananchi wakitumia simu zao za mikononi kupiga picha za kumbukumbu.

Msafara ulipofika uwanjani, ulipokewa na wabunge, madiwani na watu waliopata shahada ya udaktari wa heshima (PhD) pamoja na marehemu ambao walipata fursa ya kubeba jeneza lake.

Pia, washirika hao waliopata heshima hiyo pamoja na Ndesamburo walifanya tendo la kuweka joho na kofia ya Ndesamburo aliyotunukiwa juu ya jeneza lake.