VIDEO: Polisi wamtafuta mfanyabiashara Mo Dewji Bahari ya Hindi

Gari la Polisi likifanya doria katika maeneo ya fukwe za Yacht Club jijini Dar es Salaam jana.

Muktasari:

Alhamisi asubuhi Oktoba 11, 2018 mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ alitekwa katika Hoteli ya Colosseum na Jeshi la Polisi limesema linaendelea kuimarisha ulinzi huku likifanya uchunguzi katika Pwani ya Bahari ya Hindi hususani katika hoteli zilizo ukanda huo ikiwamo Yacht Club

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limeendelea kuimarisha ulinzi huku likifanya uchunguzi katika Pwani ya Bahari ya Hindi hususani katika hoteli zilizo ukanda huo ikiwamo Yacht Club.

Polisi hao wamekuwa wakikagua kamera za video (CCTV) katika hoteli ya Yacht Club, lengo likiwa ni kumsaka mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ aliyetekwa juzi alfajiri na watu wasiojulikana.

Mo (43), alitekwa katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam saa 11 alfajiri alikokwenda kwa ajili ya kufanya mazoezi kwenye gym ya hoteli hiyo.

Meneja Mkuu wa Yacht Club, Brian Fernandez aliliambia Mwananchi jana kuwa tangu tukio la kupotea kwa Mo lilipotokea, polisi wameimarisha ulinzi na uchunguzi katika eneo hilo ambalo liko pwani ya Bahari ya Hindi.

Fernandez alisema Mo alikuwa mwanachama wa klabu hiyo na hakuonekana katika eneo hilo tangu juzi na hakuna boti ya mwanachama yeyote iliyoondoka tangu jana.

“Kama mwanachama anataka kwenda kwenye boti yake tunampeleka na boti yetu. Kwanza anaandika muda wa kuondoka na kurudi ili kama akichelewa afuatiliwe,” alisema.

Alisema Mo ni mtu maarufu na kama angefika eneo hilo angejulikana.

Awali, waandishi walifika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo maeneo ya Laibon, Oysterbay lakini walinzi waliwaambia msemaji wa familia amezuiwa kuzungumza na wanahabari.

Jaji, mawakili wataja za

sababu watu kutekwa

Baadhi ya mawakili, majaji, wasomi na wanasheria waliojibu maswali waliyoulizwa na Mwananchi ikiwamo ni kwa nini watu hutekwa, wamesema zipo sababu kadhaa zinazowasukuma watekaji kufanya hivyo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) mkoani Iringa, Dady Igogo alisema miongoni mwa sababu hizo hasa kwa wafanyabiashara wakubwa ni kushindwa kurejesha mikopo kutoka kwa wafanyabiashara wenzao.

Hata hivyo, alisema utekaji wa aina hiyo mara nyingi hutokea Hong Kong nchini China.

Lakini sababu nyingine, alisema ni watu kutaka kujipatia fedha kwa kuzihamisha kutoka kwenye akaunti ya mtekwaji kwa njia ya kimtandao.

Mhadhiri huyo alisema kwa Tanzania, utekaji haujaanza miaka ya karibuni kwani hata zamani ulikuwapo.

“Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Kassim Hanga alitekwa na kupotea tangu miaka ya 1960 hadi leo hii hajawahi kupatikana,” alisema Igogo.

“(Kuanzia) utawala wa Mwalimu Nyerere hadi (John) Magufuli, wapo Watanzania wengi wametekwa. Ila sema kwa sasa zinasikika kwa sababu ya ongezeko la vyombo vya habari sambamba na teknolojia ya habari na mawasiliano.”

Aliitaja sababu nyingine ya wafanyabiashara kutekwa kuwa ni kama utajiri wa mhusika unahatarisha hali ya usalama kwa Taifa na Serikali.

Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Lawrence Mchome alisema sababu nyingine za utekaji ni kutaka kulipiza kisasi.

“Kuna sababu nyingi za utekaji, lakini moja inaweza kuwa watekaji wanataka fedha, kwa hiyo wanamteka ili atoe fedha lakini nyingine ni ulipizaji tu visasi na vinaweza kuwa vya kisiasa,” alisema.

Wakili wa Mahakama Kuu, Frank Robert alisema mtu anaweza kutekwa kama njia ya kumtisha ili akubaliane na matakwa fulani ama ya kisiasa, kibiashara au kijamii.

“Hii inategemea na nini mtekaji au boss (mkuu) wake anakerwa na mtekwaji. Mtu akishatekwa kama si jasiri humfanya kukubaliana na matakwa ya mtekaji,” alisema Robert.

Wakili huyo alisema wapo watu wanaoteka kwa ajili ya kujipatia kipato na mara nyingi watekaji wa aina hiyo hutoa madai yao mapema na kuelekeza wapi fedha zipelekwe au zitumwe.

“Kuna ufahari sijui tunauitaje, ila mwingine anajisikia ufahari kuteka. Lakini kuna wengine wanateka ili kutuma ujumbe. Mtu anaweza akateka ili kutuma ujumbe huko nje.”

Utekaji watoto

Mwaka 2011 liliibuka kundi la ‘kimafya’ lililokuwa likiteka watoto mjini Moshi na kuwasafirisha hadi mji wa Busia nchini Uganda kisha kudai fedha kutoka kwa wazazi ili wawarejeshe.

Aprili 2011, kundi hilo lilimteka mtoto Faraji Haruna na kwenda naye hadi Busia na kutoa masharti ya kulipwa Dola 1,000 za Marekani ili wamrejeshe (Sh1.5 milioni).

Baba wa mtoto huyo, Haruna Ayoub alikaririwa akisema baada ya majadiliano ya muda mrefu watekaji hao walimtaka alipe Dola 400 za Marekani (sawa na Sh600,000) ambazo ziliingizwa kwenye akaunti ya benki.

Akaunti hiyo ilikuwa tawi la Busia nchini Uganda na baada ya kulipwa fedha hizo watekaji walimpandisha mtoto huyo kwenye basi na kumrejesha Moshi.

Mtoto Ibrahim Lawrence wakati huo akiwa na umri wa miaka saba alitekwa Julai 2011 na watekaji kusafiri naye hadi Busia na kumwachia baada ya wazazi wake kuwalipa Sh3.5 milioni.

Mkoani Mwanza

Tukio la kutekwa kwa Mo limeibua hofu ya kiusalama miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa mkoani Mwanza ambao wameiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti za kuimalisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Akizungumza na Mwananchi jana, mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani humo, Elibariki Mmari alisema wameshtushwa na tukio hilo na kuviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kila lililo ndani ya uwezo wao kumtafuta na kumpata mfanyabiashara mwenzao akiwa salama.

“Kwa kipindi sasa matukio ya watu kudaiwa kutekwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha yamekuwa yakitokea na kuripotiwa, lakini hili la Mo ni la kipekee na la kwanza kwa mfanyabiashara mkubwa wa kiwango chake. Ni mshtuko siyo tu kiusalama, bali pia katika masuala ya biashara na hata uchumi,” alisema Mmari.

“Simaanishi kuwa yaliyotokea hayakushtua na kutisha. La hasha. Yalitisha ni matukio mabaya yanayotakiwa kupigwa vita, kulaaniwa, kukemewa na kukomeshwa. Ila hatujawahi kuona mfanyabiashara na mtu mwenye uwezo kama (Mohammed) Dewji akitekwa.”

Akizungumzia ulinzi binafsi nyumbani, ofisini na maeneo ya biashara, Mmari alisema, “Kwa mshtuko tulioupata kutokana na tukio hili, sisi tunachotaka kwa sasa ni mwenzetu apatikane akiwa hai na salama huku wahusika wakitiwa mbaroni.”

Alisema Dewji kutopatikana na wahusika kutiwa mbaroni kwa haraka kunazidisha hofu miongoni mwa wafanyabiashara.

“Kiuhalisia, hofu hii inaweza kuleta athari katika sekta ya biashara na uchumi wa Taifa,” alisema Mmari.

Alisema hofu ya wafanyabiashara na Watanzania kwa sasa inatokana na kutojulikana kwa nini mfanyabiashara huyo ametekwa na wahusika wana nia gani.

“Pengine wamemteka kwa sababu zao binafsi. Yawezekana ni watu wanataka fedha na wataanza kudai kwa sharti labda la kumwachia. Haya yote ni mambo yanayoibua hofu yanayohitaji kuchunguzwa na kufuatiliwa.”

Mkazi wa Igogo jijini humo, Lameck Kayamba alisema tukio hilo ni pigo kiuchumi kwa sababu litarejesha nyuma juhudi za Serikali za kuwa na uchumi wa kati kupitia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025, iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kukomesha tabia ya utekaji.

Kayamba alisema anahofia huenda wawekezaji kutoka nje wataanza kuogopa kuja nchini wakihofia usalama wao. “Hata fursa za kiuchumi na ajira rasmi, na zisizo rasmi katika viwanda na biashara za Dewji ndani na nje ya nchi ziko shakani,” alisema.

Singida walaani Mo kutekwa

Katibu wa Baraza la Kiislamu Tanzania (Bakwata) mkoani Singida, Burhani Mlau alisema wanalaani kitendo cha kutekwa kwa mfanyabiashara huyo na kuviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya juhudi ili apatikane. “Bakwata leo katika wilaya zote saba mkoani hapa tunaomba dua maalumu ya kumuombea muumini mwenzetu apatikane akiwa hai,” alisema Mlau.

Askofu mstaafu wa Kanisa la Pentekoste (FPCT) Mjini Kati, Paulo Samweli alisema wanaungana na wapenda amani kukemea vitendo vya utekaji vinavyoendelea kuibuka nchini.

Alisema kanisa litaendelea kumkumbuka katika maombi mbunge wao huyo wa zamani kwa kuwa alikuwa akitoa misaada mingi bila kubagua dini wala kabila na yote ililenga kustawisha jamii.

“Kanisa litaendelea kumwombea kwa Mungu apatikane mapema, arudi kuungana na familia yake na Watanzania ili kuiendeleza nchi,” alisema Askofu.

Katibu wa CCM mkoani humo, Amina Imbo alisema wakazi wa Singida wanaukumbuka mchango wa Mo aliokuwa akiutoa alipokuwa akiwatumikia katika nafasi yake ya ubunge.

Alisema hata baada ya kustaafu ubunge, Dewji aliendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za maendeleo mkoani humo.

Lugola kuongoza kikao leo

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni aliiambia Mwananchi jana kuwa viongozi wa juu wa wizara hiyo wakiongozwa na waziri wake, Kangi Lugola, leo watafanya kikao kitakachokuwa na ajenda ya utekaji.

Masauni alisema kikao hicho kitahudhuriwa na katibu mkuu wa wizara, Meja Jenerali Jacob Kingu; naibu wake, Ramadhan Kailima na mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro atakayeambatana na makamishna, manaibu kamishna na baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa. “Mada itakuwa moja tu, kujadili suala la utekaji. Kikao kikiisha tutawaeleza Watanzania tulichokubaliana kuhusu ajenda tuliyokuwa tukiijadili,” alisema Masauni.

Imeandikwa na Elias Msuya, Kelvin Matandiko, Khatimu Naheka, Daniel Mjema, Bakari Kiango, Jesse Mikofu, Ngollo John na Sada Amir na Gasper Andrew.