Ukomo wa umri wa Rais wakipasua chama tawala Uganda

Muktasari:

 

  • *Wajumbe 121 wajitokeza kupinga kusudio la kuondoa ukomo wa umri
  • *Wasema kusudio hilo ni sawa na jaribio la kupindua sheria mama ya nchi
  • *Wataka zifanyike taratibu za kukabidhi uongozi kwa mrithi kwa amani

Kikundi cha wafuasi kindakindaki wa chama tawala cha NRM wakiwemo baadhi ya wenyeviti wa majimbo wameelezea pendekezo la kufuta Ibara ya 102 (b) ya Katiba ili kuondoa ukomo wa umri wa rais ni jaribio la kupindua sheria mama.

Katika taarifa yao iliyosomwa jana na Dennis Sekabira, ambaye ni mwenyekiti wa Jimbo la Nakaseke Kusini, kikundi hicho kiliwaambia waandishi wa habari kwamba wanapinga msimamo wa wabunge wa chama hicho kwa sababu mradi wao huo hauna maslahi kwa amani ya nchi.

“Huu ni mwelekeo hatari na unahatarisha amani tuliyoifaidi nchini,” alisema Sekabira ambaye ameeleza kwamba kikundi hicho kina wajumbe 121 wa Halmashauri Kuu ya Taifa, chombo cha pili kwa ukubwa katika uongozi wa chama.

Mwenyekiti huyo alisema wajumbe hao hawaungi mkono juhudi za kuzuia maoni ya wengi dhidi ya kusudio la kuondoa ibara hiyo na kwamba inahitajika amani wakati wa kukabidhi madaraka.

“Tumeamua tusiinyime haki nchi yetu nafasi pekee ya kubadilisha mamlaka kwa amani,” alisema. “Badala ya kuhutubia suala la ukomo wa umri, wabunge wa NRM wanapaswa kujikita katika utekelezaji wa Ilani ya chama.”

Mwaka 2015 Waganda walibadili katiba kuondoa ukomo wa mihula kumwezesha Rais Yoweri Museveni kugombea muhula wa tatu na kuendelea na sasa ukiondolewa ukomo wa umri wa miaka 75, rais huyo mwenye umri wa miaka 73 sasa atakuwa huru kugombea tena mwaka 2021 akiwa na umri wa miaka 77.