Upinzani waja na bajeti ya Sh29.9 trilioni

Muktasari:

  • Hotuba hiyo itawasilishwa na naibu msemaji wa upinzani kwa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde kutokana na mwenye dhamana hiyo, Halima Mdee kuwa nje kwa ajili ya kutumikia adhabu.

Kambi Rasmi ya Upinzani leo inawasilisha bajeti mbadala ya Sh29.9 trilioni kwa mwaka 2017/18, ikiwa ni pungufu ya Sh1.8 trilioni kulinganisha na bajeti ya Waziri Philip Mpango, huku ikiibua vyanzo sita vipya vya mapato.

Hotuba hiyo itawasilishwa na naibu msemaji wa upinzani kwa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde kutokana na mwenye dhamana hiyo, Halima Mdee kuwa nje kwa ajili ya kutumikia adhabu.

Na katika kile kinachoonekana kuepuka hotuba yao kumezwa na hafla ya kukabidhi ripoti ya kamati ya pili iliyoundwa kuchunguza athari za kiuchumi za kusafirisha mchanga wa madini nje na matatizo ya kisheria katika mikataba, wapinzani waliamua kuzungumzia kilichomo katika bajeti hiyo jana mjini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mdee alisema bajeti iliyowasilishwa na Serikali mwishoni mwa wiki ilikuwa na mapungufu ambayo hayawezi kuwa na tija kwa Watanzania.

Hata hivyo, mbunge huyo wa Kawe alisema upinzani unakubaliana na baadhi ya mambo ambayo Serikali ilipendekeza, kama kuondolewa kwa ada ya mwaka ya leseni za magari, ongezeko la bei ya mafuta isipokuwa mafuta ya taa.

Mdee alitaja vyanzo vipya ambavyo wapinzani wameviibua kuwa ni mapato yatokanyo na uvuvi katika bahari kuu, madini ya vito kutokana leseni na kodi na malipo kulingana na kipato (P.A.Y.E).

Nyingine ni kupunguza misamaha ya kodi kwa asilimia moja ya Pato la Taifa, amana za fedha za kigeni (eurobond), mapato kutoka sekta ya utalii na mapato katika sekta ya michezo ya kubahatisha ambavyo kwa ujumla wake alisema vingeliingizia Taifa Sh30 trilioni

“Hapo kusingekuwa na ubabaishaji hata kidogo kuliko ilivyo kwa wenzetu (Serikali) ambao wamekuja na mambo ya mbwembwe nyingi ilihali wameshindwa hata kuainisha vyanzo kamili na wakati huo huo vitabu vyao vinatofautiana,” alisema Mdee.

Akizungumzia tofauti ya vitabu vya bajeti ya Serikali, Mdee alisema kitabu cha mapato kinaonyesha kuwa Serikali kwa mwaka 2017/18 itakusanya Sh23.9 trilioni wakati kitabu cha matumizi kinasema watatumia Sh26.9 trilioni ikiwa ni ongezeko la Sh3 trilioni ambavyo vyanzo vyake havijaonyeshwa kwenye kitabu cha mapato.

“Bajeti ya Serikali iliyosomwa bungeni inaonyesha kuwa mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18 ni Sh31.7 trilioni, kiasi ambacho hakionekani popote katika vitabu vyote vya mapato na matumizi ya Serikali na kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano tarakimu hiyo inaonyesha ni makisio ya mwaka 2018/19 jambo linaloonyesha hatutekelezi bajeti ya 2017/18 badala yake ni ya 2018/19,” alisema Mdee.

Msemaji huyo alieleza masikitiko ya upinzani kuwa bajeti hiyo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania inawalipisha kodi ya mafuta wananchi masikini wasio na uwezo wa kumiliki magari baada ya kuweka tozo ya nishati hiyo katika mafuta ya taa.

Kwa mujibu wa Mdee, bajeti ya Serikali imelenga kuwabebesha mzigo wananchi masikini ambao mwisho wake watakosa hata mwanga wa taa kwa kubeba mzigo wa watu wa tabaka la kati na juu.

Akizungumzia vipaumbele vya upinzani, Mdee alisema wanavyo vitano ambavyo kama wangepewa jukumu la kusimamia bajeti hiyo, wangeanza navyo.

“Cha kwanza kwetu ni elimu asilimia 20, viwanda asilimia 15, nishati asilimia 15, kilimo 10 na sekta nyingine zingechukua asilimia 40 ya bajeti ya maendeleo,” alisema Mdee.

Alisema kama vipaumbele hivyo vingetekelezwa kwa ukamilifu, Tanzania ingepunguza umasikini kwa asilimia 50 kwa kuwa vipaumbele hivyo vinachochea ajira kwa watu wengi.

Kwa upande mwingine upinzani umelia na kile alichosema ni danganya toto ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo iliahidi kupeleka Sh50 milioni kwa kila kijiji, lakini imeshindwa kufanya hivyo na hata kwenye bajeti imeshindwa kuingiza.

Mdee alisema mpango huo ulikuwa ni ahadi za siasa ambazo hata wangefanya miujiza, Serikali haitaweza kwa kuwa inapaswa kutengwa Sh960 bilioni kwa vijiji vyote.

Akizungumzia suala la mapato kwa halmashauri, Mdee alisema kitendo cha Serikali kuondoa kodi ya majengo katika halmashauri na kuipeleka TRA ni sawa na kuziua wakati huu ambao zinaonekana kulegalega.

“Hii ni bajeti ambayo imedhamiria kuua kabisa dhana ya ugatuaji madaraka kwa serikali za mitaa (D by D) kwa kuziondolea madaraka ambayo ni ya kisheria,” alisema.