Prime
Jicho la DCEA lageukia watumishi wa umma matumizi dawa za kulevya
Muktasari:
- Baada ya kubainika baadhi ya watumishi wa Serikali wanatumia dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Kanda ya Kaskazini imeanza kuimarisha operesheni, kutoa elimu kwa watumishi wa umma na kufanya ukaguzi katika kumbi za starehe, hasa maeneo maalumu (VIP), ambayo wamebaini baadhi yanatumika kwa ajili ya kuvuta bangi na kula mirungi.
Arusha. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini, imepanua mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya kwa kuhamishia kampeni za elimu katika taasisi za umma, kuimarisha operesheni kwenye kumbi za starehe na kuongeza ushirikiano na wadau mbalimbali.
Hii ni kutokana na kubainika kuwa baadhi ya watumishi wa Serikali wanajihusisha na matumizi ya dawa hizo.
Hatua hiyo inafuatia kauli ya hivi karibuni ya Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, aliyesema uchunguzi umebaini baadhi ya watumishi wa Serikali jijini Arusha, wanatumia dawa za kulevya, hususan katika maeneo ya burudani, ikiwemo sehemu za VIP kwenye kumbi za starehe.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Julai 12, 2026, Ofisa wa DCEA Kanda ya Kaskazini, Abdulatif Saidy amesema mamlaka hiyo imeongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa watumishi wa umma, huku ikiendelea na operesheni za usiku katika maeneo yanayotajwa kuwa vinara wa matumizi ya bangi na mirungi.
Amesema DCEA imeanza kuendesha semina na mikutano ya uelimishaji katika taasisi na idara mbalimbali za serikali kwa lengo la kuwajengea watumishi uelewa kuhusu athari za dawa za kulevya kwa afya, familia na utendaji kazi.
"Tumeona kuna umuhimu wa kuhamishia nguvu zaidi katika taasisi za serikali kwa kutoa elimu kwa watumishi. Tunataka wajue madhara ya dawa za kulevya na wajiepushe nazo kabla hazijaharibu maisha yao na utendaji wao kazini," amesema Saidy.
Amesema kampeni hiyo siyo mpya, kwa sababu mwaka jana DCEA ilitoa elimu kwa zaidi ya watumishi 1,500 katika mkutano wa kitaaluma, na sasa imeongeza wigo wa kuwafikia watumishi wengi zaidi.
Saidy amesema mamlaka hiyo pia imekutana na wamiliki wa kumbi maarufu za starehe jijini Arusha na kuwapa elimu kuhusu mbinu zinazotumiwa kusambaza na kutumia dawa za kulevya pamoja na wajibu wao wa kisheria katika kuzuia vitendo hivyo.
Kwa mujibu wake, wamiliki hao wameelekezwa kuweka mabango yanayokataza matumizi ya dawa za kulevya, kushirikiana na vyombo vya dola, kutoa taarifa kuhusu watuhumiwa na kutoruhusu biashara au matumizi ya dawa hizo ndani ya maeneo yao.
Hata hivyo, amesema changamoto kubwa inaendelea kuwa baadhi ya watumiaji wanaokaidi maelekezo na wakati mwingine kuzua vurugu wanapozuiwa kutumia dawa hizo.
"Hatukutaka kuanza kwa kutumia nguvu. Kwanza tuliwapa elimu wamiliki wa kumbi za starehe, kisha tukaanza operesheni. Tulibaini baadhi ya watu wakitumia bangi na mirungi na hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi yao," amesema.
Kwa mujibu wa Saidy, kati ya Julai 2025 na Juni 2026, DCEA Kanda ya Kaskazini ilifanya operesheni 227 na kuwakamata watuhumiwa 550, wakiwemo wanaume 442 na wanawake 108.
Katika operesheni hizo, zilikamatwa kilo 5,417.26 za mirungi, kilo 3,010.30 za bangi na gramu 14 za heroini katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Kwa Mkoa wa Arusha pekee, amesema operesheni 121 zilifanyika na watuhumiwa 413 walikamatwa, wakiwemo wanaume 338 na wanawake 75. Pia zilikamatwa kilo 1,458.26 za mirungi na kilo 2,977.03 za bangi.
Amesema bangi na mirungi ndizo dawa zinazotumika zaidi mkoani humo, huku akibainisha kuwa DCEA itaendelea na operesheni pamoja na kuhamasisha waathirika wa uraibu kutafuta huduma katika vituo maalumu vya tiba.
Mbali na operesheni, Saidy amesema mamlaka hiyo imeanza kutumia wasanii, matamasha ya muziki na mabonanza kuifikia jamii, hususan vijana, ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya dawa za kulevya.
Amewataka vijana kujiepusha na makundi yanayochochea matumizi ya dawa hizo na kushiriki kutoa elimu kwa wenzao, huku akiwataka watumishi wa Serikali kuzingatia maadili ya utumishi na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu taaluma zao.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema wilaya hiyo inaendelea kushirikiana na DCEA kupitia ukaguzi wa kumbi za starehe, utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali na upelelezi wa taarifa zinazohusu matumizi ya dawa za kulevya.
"Tutatoa ushirikiano wote kwa DCEA. Hakuna huruma kwa mtu yeyote atakayebainika kuruhusu au kushiriki biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Lengo letu ni kulinda vijana na kuhakikisha jamii inakuwa salama," amesema Mkude.