Wabunge Komu, Kubenea walihojiwa kwa dakika 281

Muktasari:

Wabunge Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) jana Jumatano Oktoba 17, 2018 wamehojiwa kwa dakika 288 na kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilichofanyika katika hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam


Dar es Salaam. Wabunge Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) jana Jumatano Oktoba 17, 2018 walihojiwa kwa dakika 288 na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania kilichofanyika katika hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilikuwa na ajenda moja ya kuwahoji wabunge hao baada ya siku za hivi karibuni kuzua mjadala ndani na nje ya chama hicho kwa kile kinachodaiwa kuwa ni sauti yao iliyokuwa ikisikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekana kuhusika na sauti hizo kwa kile walichoeleza ni za kutengeneza huku Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo (Chadema) naye akieleza kupeleka suala hilo ndani ya chama.

Wawili hao waliwasili katika kikao hicho saa 8:01 mchana na kupokelewa na baadhi ya makada wa Chadema waliokuwa nje.

Dakika 10 baadaye Komu aliitwa katika kikao huku Kubenea akibaki nje akisubiri zamu yake.

Saa 9:40 alasiri wajumbe wa kikao hicho walitoka mapumziko kwa ajili ya chakula cha mchana.

Mmoja wa wazee wa Chadema alimfuata Kubenea sehemu aliyokuwa ameketi na kumkaribisha chakula.

Saa 10:58 jioni wajumbe walirejea ukumbini na kuendelea na kikao kuendelea kumhoji Komu.

Saa 11:32 jioni Komu alitoka kikaoni na alipofuatwa na waandishi kwa ajili ya kuelezea kilichojiri alisema hawezi kuzungumza chochote.

“Kwa mujibu wa katiba ya chama changu sina mamlaka ya kuzungumzia chochote suala hili lipo ndani ya kikao,” amesema.

Saa 11:40 jioni Kubenea aliitwa kikaoni katika mahojiano yaliyodumu hadi saa 2:35 usiku.

Saa 2:37 Kubenea alitoka katika kikao na kuungana na Komu aliyekuwa ameketi katika gari aina ya Toyota Noah wakisubiri kikao hicho kimalizike.

“Siwezi kuzungumza kwa sasa kwa kuheshimu kikao cha chama, nikizungumza itakuwa kinyume na taratibu za chama nasubiri maazimio,” amesema Kubenea jana.