Homa ya ini ni ugonjwa hatari kuliko Ukimwi

Mwanamke akipata chanjo ya homa ya ini, ugonjwa ambao unaua na kusumbua wengi duniani ikiwamo Tanzania. Picha ya Mtandao

Muktasari:

  • Wataalamu wanaeleza kuwa Hepatitis B au homa ya ini ni ugonjwa unaoambukizwa kwa urahisi, wenye madhara makubwa na wenye uwezo wa kuambukiza kwa wepesi kuliko Ukimwi.

Ugonjwa wa selimundu unasumbua wengi, umetengua ndoa za wengine, kwa sababu ya kutojua.

Hakuna shaka kwamba umewahi kusafiri nje ya nchi yako na kutakiwa kupata chanjo.

Kwa wengine, chanjo hiyo ikiwamo ya homa ya ini imeonekana kama usumbufu na  udhia mtupu. Hata hivyo, wapo wengine ambao hawaufahamu ugonjwa huu.

Kwa wanaoujua, wanahofia kuwa ugonjwa huu una madhara makubwa pengine kuliko  saratani na Ukimwi.

Homa hiyo au Hepatitis B inapewa uzito mdogo licha ya kuwa ni  ya hatari kubwa.

Wataalamu wanaeleza kuwa Hepatitis B au homa ya ini ni ugonjwa unaoambukizwa kwa urahisi, wenye madhara makubwa na wenye uwezo wa kuambukiza kwa wepesi kuliko Ukimwi.

Kitaalamu, ugonjwa huu, husababishwa na virusi vya Hepatitis B (HBV) ambavyo huathiri  mfumo wa utoaji wa sumu mwilini. Inaelezwa kuwa robo tatu ya watu ulimwenguni wameathiriwa kwa muda na homa ya ini na wengine milioni 350 wameathirika moja kwa moja.

Takwimu zinaonyesha kuwa homa ya ini huua watu 600,000 kila mwaka katika sehemu mbalimbali, idadi ya watu inayolingana na wale wanaokufa kutokana na malaria.

Maradhi haya ya ini yanaelezwa kuwa yanaweza kusababishwa na kunywa kileo kupita kiasi au sumu inapoingia mwilini.

Hata hivyo, mara nyingi ugonjwa huu husababishwa na virusi.

Wanasayansi kwa upande mwingine wamegundua virusi vitano vinavyosababisha ugonjwa huu na wanasema kwamba huenda kuna vingine vitatu.

Matokeo yake, sheria zimewekwa  katika nchi mbalimbali ambazo zinamtaka kila raia mgeni anayetaka kuingia katika nchi husika, kupata chanjo ya ugonjwa huu ili kuepusha maambukizi.

 Kila anayechanjwa  hupewa kadi maalum  itakayomwezesha kuingia katika nchi husika ili kuthibitisha kuwa amechanjwa.

 Hata hivyo, ujanja mwingi umekuwa ukifanyika katika baadhi ya nchi ikiwamo Tanzania ambapo watu hujipatia kadi za homa ya manjano kwa kutoa rushwa na kukwepa kuchoma chanjo hiyo pindi wanapotaka kusafiri nje ya nchi bila kujua madhara ya kutopata chanjo hiyo.

 Vilevile, chanjo hiyo iliwahi kukosekana nchini kwa zaidi ya mwezi mmoja kutokana na sababu ambazo haziwekwi wazi na mamlaka zinazohusika.

Hatari kubwa ya ugonjwa huu inatajwa ni namna ya uambukizaji wake ambapo, unaposhika damu au majimaji ya mwilini ikiwemo mbegu za uzazi huweza kuambukizwa.

 Wataalamu wanaeleza ubaya wake ni kuwa unaweza kuambukizwa kwa kufanya ngono na hata kwa kushika majimaji ya mwili wa mtu aliyeathirika ikiwemo damu, mate, machozi na mkojo.

Taarifa za Shirika la Afya Duniani(WHO) zinaeleza kuwa  kirusi cha homa ya ini kinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu kwa siku saba na kwa wakati huu, kirusi hiki kinaweza kusababisha maambukizi iwapo mtu hajapata chanjo ya kuuzuia.

Watanzania wengi bila kujua wamekuwa wakiugua maradhi mbalimbali yanayosababishwa na homa ya ini na bila kufahamu ini limekuwa likiathirika taratibu.

Dk Yuki Mark wa Hospitali ya Parktown North, Johanesburg, nchini Afrika Kusini anasema kuwa homa ya ini aina ya B inaweza kuua kimyakimya bila kuonyesha dalili zozote.

“Huenda dalili zikaonekana waziwazi miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa. Zinapoonekana, huenda tayari ini limenyauka au lina saratani na magonjwa hayo huua asilimia 25 ya watu walio na virusi vya HBV,” anasema Dk Mark.

 Aidha, mtaalamu huyo anasema, dalili kuu zinazojulisha kuwa mtu ana homa ya ini ni kutapika, kuchoka kupita kiasi, kuathirika kwa ini, homa na mkojo kuwa wenye rangi ya njano iliyokolea sana.

“Unaweza kuharisha na kutapika au kupata maumivu katika eneo fulani la tumbo lako, macho na ngozi kuwa vya njano,” anaeleza.

Homa ya ini aina ya B, inaweza kuingia mwilini mwa mtu kwa njia ya ngono, kama ilivyo Ukimwi na magonjwa mengine ya  zinaa. Hivyo basi, majimaji   katika mwili wa mwanadamu yanaweza kuwa chanzo cha maambukizi.

“Watu  wengi wanaendelea kuambukizwa kwa kutiwa damu yenye virusi hivyo, hasa katika nchi ambako hakuna vifaa bora vya kuchunguza virusi hivyo katika damu. Virusi vya HBV vina uwezo mkubwa zaidi wa kuambukiza kwa kulinganishwa na virusi vya Ukimwi,” anasema Dk Mark

Anaongeza: “Hata kiasi kidogo cha damu yenye virusi hivyo kama ile inayobaki kwenye wembe, inaweza kupitisha virusi hivyo na tone la damu iliyokauka kwa juma moja au hata zaidi inaweza kumwambukiza mtu virusi hivyo.”

Dk Mark anasema, madhara mengi huweza kumkumba mtu aliyepata maambukizi ya homa ya ini, kwani anaweza kupata shinikizo la damu, anaweza kuathirika ubongo au hata kupooza sehemu ya mwili wake.

Angalizo ambalo mtaalamu huyo anaeleza ni kuwa baada ya mtu kuambukizwa homa hiyo, hawezi kupona, kwani dawa kuu ya ugonjwa huu ni chanjo ya kuzuia homa ya manjano (yellow fever vaccination).