KONA YA MAKENGEZA : Tamba katika kutumbua

Sunday May 15 2016

 

By Richard Mabala

Wewe Makengeza, huna akili. Wizara yako ya Mama na Mwana na Babu na Bibi na nani zaidi sijui haina akili pia. Eti, jitambue, Jitumbue. Hapana. Hata kidogo.

No. La hasha. Unapaswa kusema tamba katika kutumbua. Kutumbua ni kazi muhimu, katika kutumbua tunaokoa jamii, kwa nini tusitambe?

Ndiyo maana, ingawa nampongeza mheshimiwa wetu mkuu kwa kazi yake ya utumbuaji, sina budi kusema kwamba yeye na Makamu wake wanakosea. Eti sisi tunaoiga kazi yao nzuri, tujihadhari. Eti tufuate sheria na kanuni. Nasema hapana, no, hata kidogo. Wao ndiyo wanapaswa kutamba katika kutumbua na wao. Ikiwezekana hata wawapige viboko kabisa. Unyenyekevu wa nini?

Upande wetu tunaotakiwa kufa katika kuiga, ndiyo zaidi. Bila kutamba mkuu atatuona saa ngapi? Watu watatusujudu saa ngapi? Lazima watu wajue sisi ni akina nani? Lazima wajue kwamba sisi tuko juu, juu, juu zaidi na wasithubutu kujilinganisha na sisi. Hata kama wao wana kazi nzuri namna gani, sisi ndiyo watawala.

Yaani, mimi nikiwa kazini, mtu mwingine ajidai kuvaa vizuri kuliko mimi. Kwanza hana adabu, ana nia mbaya ya kutaka kunidhalilisha mimi kwamba sijui kuvaa. Akinidhalilisha mimi, amedhalilisha aliyeniteua.

Kisha akiwa kazini, tai ya nini? Inaonyesha wazi kabisa kwamba hayuko makini katika kazi yake. Badala ya kutoa jasho kama mfanyakazi wa kawaida, anajidai na suti. Usiniambie kwamba kuna mgawanyo wa kazi. Hata kama kazi yake ni kuandika vitabu, lazima aonekane anafanya kazi.

Advertisement

Wale wengine wanaoiga sauti ya watawala ni majipu! Lazima watumbuliwe kwa sababu wanachafua hali ya hewa. Na vivyo hivyo, katika kumdhalilisha anayemwiga, anadhalilisha Taifa. Lazima ashtakiwe kwa kukosa uzalendo. Potelea mbali kama waliiga sauti hata ya Baba wa Taifa huko nyuma, sasa ni enzi ya kutamba. Ndiyo maana atakayeniigiza tu ataona cha mtema kuni.

Yeyote atakayenikosoa ataona cha mtema kuni. Mimi mtawala, wewe nani kuhoji? Nimesema, yeyote anayetia mchanga utambaji wangu atatambaa nakuambia.

Ndiyo! Bado tunakumbuka stori za enzi wa babu wa taifa wa nchi jirani. Ilikuwa marufuku kumdhalilisha kwa njia yoyote ile. Kwa mfano, akienda kwenye harambee na kuchangia hiki au kile ilikuwa marufuku kutoa mchango unaozidi wa kwake maana kufanya hivyo ni kumdhalilisha, ni kufanya aonekane maskini au bahili, hivyo ni uhaini.

Kwa hiyo, yeye akitangaza kuchanga laki mbili, ole wake atakayetoa zaidi ya laki moja na tisini na tisa elfu. Sasa alikuwapo mwehu fulani, nadhani alipata kichaa wakati wa vita vya Mau Mau dhidi ya wakoloni, ambaye alipenda kumpiku rais wake … hebu fikiria .. kumpiku rais wako … kweli? Kwa hiyo, mkuu akisema laki mbili basi yeye anaamka na kusema laki mbili na nusu, hadi mkuu analazimika kuongeza fedha zaidi papohapo ili asipikuliwe. Unajua mwisho wake huyu asiyekuwa na adabu?

Pamoja na utajiri wake wote, na umaarufu wake kisiasa, kakutwa ameuawa. Sasa sijui kwa nini aliuawa lakini watu walisema kwamba kazi yake ya kupinga na kumpiku mkuu ilichangia.

Kwa hiyo, usinielewe vibaya na upumbavu wako Makengeza. Simpingi mkuu wangu, mimi ni nani kumpinga? Nasema tu ajiamini zaidi, atambe katika kutumbua. Sisemi kwamba wanaojaribu kujifanya wakubwa kuliko sisi nao wakutwe waemuawa. Si utamaduni wetu.

Nasema kwa nguvu zote kwamba sisi tunaopenda kucheza ngoma anayoipiga mkuu wetu, lazima tutambe zaidi na zaidi watu watutambue. Watu wajue kwamba mafahali wawili hawakai zizi moja na mimi ndani ya himaya yangu ni fahali mwenyewe. Ohoo.

Mwenye kujidai fahali mwenye fahari kuliko mimi atatupwa nje ya zizi moja kwa moja. Usiniletee uanaharakati wako wa kupinga mfumo dume. Mfumo dume unadumu, haudumai na mimi ndiyo dume lenyewe, daima dumu.

Hivyo ieleweke kwamba katika himaya yangu, tunafuata masharti yafuatayo.

Kwanza, Hapa Vazi Tu. Watu wajue nimevaa nini kabla ya kutoka nyumbani. Nikiwa nimevaa suti, sawa wavae suti na wao pia. Lakini kama nimevaa nguo za mgambo basi wavae kimgambo na wao. Watapiga namba: 077777777 kila asubuhi kupata taarifa ya mavazi yangu ya siku. Unajua huko Ufaransa, enzi za ufalme, watu walikuwa wanaalikwa kuhudhuria sherehe ya kuamka na kuvaa kwa mfalme.

Mtu akialikwa alijua ni heshima kubwa. Naona bora turudie enzi hizo. Kwa njia hiyo watajua pia ninavaa nini. Lakini kwa sasa waanze kwa kupiga simu wakati nakarabati chumba changu cha kulala kwa ajili ya sherehe hiyo. Wawe na nguo zingine ofisini za aina mbalimbali maana naweza kuamua kuamka na kutumbua majipu wakati wowote.

Pili, Hapa Kazi tu. Tunapokwenda kufanya kazi, mtu asithubutu kuonekana anafanya kazi vizuri au kwa nguvu kuliko mimi. Nikipanda miti mitano, apande minne. Nikionekana kuhema kutokana na mbuzi choma na vikorombwezo vyake vya jana, wengine ndiyo waheme kabisa na hata kuzimia kuonyesha kwamba mimi ni mchapakazi kuliko wote.

Sasa wengine wanapenda kutamba kwamba hawajachoka wakati mimi niko hoi kabisa. Ukosefu wa adabu na nikisharudisha pumzi, nitamtumbua bila huruma.

Ndiyo. Enzi za yule zimekwisha. Baba yangu alinihadithia kwamba walipokuwa JKT walialikwa kwenda kulima kwa Baba wa Taifa. Alisema kwamba walijihimu kuamka mapema kuonyesha uzalendo wao, lakini bado wakamkuta amewahi na kuanza kazi kule shambani.

Sasa katika kulima, kila wakijitahidi wanakuta kwamba yeye yuko mbele. Siku nzima, aliwashinda licha ya jitihada zao za kiJKTJKT. Zile ni enzi zake, enzi za watu kupenda kujitesa katika kujitosa lakini dunia imebadilika.

Huwezi kutegemea mimi na ukuu wangu wote niliousaka kwa udi na ubani (zaidi ubani) niweze kuwashinda wote katika kujionyesha nachapa kazi. Ndiyo maana ni lazima wao wabaki nyuma. Wakiniumbua nitawatumbua.