Kuna siri kubwa katika biashara ya karafuu

Wednesday July 05 2017
KARAFUUUU

Ni kawaida kwa matokeo ya historia kujirudia, hasa mazingira yaliyopelekea hali kurejewa au marekebisho yaliyofanywa zamani kujiepusha na hali ile kupuuzwa.

Uzoefu kila sehemu duniani umeonyesha historia inapojirudia hilo marejeo huwa makubwa au hukuzwa na huwa na mazingira ama ya kupendeza au kuchukiza zaidi.

Hivi sasa Zanzibar inashuhudia kujirejea historia juu ya biashara ya magendo ya karafuu, hasa katika Kisiwa cha Pemba ambacho kinazalisha wastani wa asilimia 85 ya mavuno ya karafuu ya Zanzibar.

Kwa karibu miaka mitano sasa magendo ya karafuu yalipungua sana. Sababu iliyotolewa juu ya mabadiliko hayo ni kwamba wakulima wa zao hili walilipwa bei nzuri na Serikali na kwa hivyo hapakuwapo vivutio vya kuzisafirisha karafuu kwa magendo nje ya Zanzibar.

Wakati ule tuliambiwa mkulima alikuwa analipwa asilimia 80 ya bei ya soko la dunia, lakini taarifa za mitandao maarufu ya biashara ya kimataifa zilionyesha bei waliyolipwa wakulima wa Visiwani ni kati ya asilimia 60 na 65 ya soko la dunia.

Hata hivyo, tusisahau jingine lililojibanza na kuchangia hali hii. Nalo ni kwamba Kisiwa cha Pemba ni kambi isiyotetereka ya Chama cha CUF na viongozi wake walipokuwa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuliwafurahisha watu wa Pemba.

Advertisement

Hivi sasa watu wa kisiwa hiki ambao hukipa CUF asilimia zaidi ya 90 ya kura katika uchaguzi kwa kiasi fulani hawafurahishwi kuona viongozi wao hawamo katika Serikali na kupeleka wengine kutoipenda hata ikiwa inawapa haki zote kama wenzao wa Kisiwa cha Unguja.

Hali hii imezusha dhana kwa watu wengi wa Pemba, kuhisi hawatendewi haki na Serikali hata bila kuwa na sababu za msingi za kuwa na mawazo hayo.

Kwa maana nyingine biashara ya magendo ya karafuu ina mshiko wa kisiasa na kama hili tatizo la kisiasa lililopo Visiwani halitakwamuliwa biashara hii huenda ikaendelea kuathiri uchumi wa Zanzibar.

Huu ndiyo ukweli, kuukubali au kukataa ni suala jingine. Taarifa za hivi karibuni zimeeleza kuwa biashara hii, ikiwa pamoja na kusafirisha karafuu mbichi sasa imeshamiri, hasa kisiwani Pemba.

Kutokana na kuwapo hali hii, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Amina Salum Ali. Ameeleza hivi karibuni kwamba Serikali imeamua kuimarisha ulinzi kila pembe ya Pemba ili kuzuia magendo ya zao hilo.

Alisema biashara ya kuzisafirisha karafuu za Zanzibar nje kwa magendo na wakati huohuo kuzileta Visiwani karafuu ambazo kiwango chake ni cha chini kutoka nje na kuzichanga na zile za Zanzibar zenye kiwango cha juu zinaipotezea Zanzibar mapato.

Yaliyotokea awali

Tunapoitafakari hali hii inafaa tujikumbushe yale yaliyoahidiwa na Serikali na matukio mbalimbali ya siku za nyuma juu ya biashara ya karafuu.

Si mara moja wala mbili tangu zama za utawala wa Rais mstaafu wa awamu ya tano, “Komandoo” Salmin Amour Juma, kwa wakulima wa karafuu kuahidiwa kwamba Serikali ingeliingiza zao la karafuu katika biashara huria kama ilivyo kwa madini, mchele, maharage na vitunguu.

Lakini ahadi ile pamoja na kuendelea kutolewa hata wakati wa utawala uliofuata wa Rais mstaafu Amani Abeid Karume haikutekelezwa.

Sasa wakulima wa karafuu wanaambiwa Serikali haina nia ya kuliingiza zao hili katika soko huria na itakuwa mnunuzi pekee wa karafuu Visiwani na ndio pekee yenye dhamana ya kuziuza nje.

Tunaambiwa kuwa bei inayotolewa na Shirika la Taifa la Biashara la Zanzibar (ZSTC) ya kununua karafuu katika vituo vyake ni nzuri nainapangwa kulingana na bei ya soko la dunia.

Tuchukulie kauli ya Serikali ni ya kweli. Kama ni hivyo tujiulize hawa wanaozinunua kwa siri karafuu kwa bei ya juu kuliko ile bei inayotolewa na ZSTC, wakati mwingine zikiwa mbichi, wanapata wapi soko lenye bei ya juu zaidi kuliko ile inayoelezwa kuwa ndiyo bei yasoko la dunia?

Suala jingine muhimu la kuzingatia ni kwamba mbali ya wakulima kuuza karafuu zao majumbani kwao kwa bei ya juu na kupata fedha papohapo pia wanapata afueni nyingine. Nayo ni kuondokana na gharama na usumbufuwa kuzisafirisha kwenda kuziuza katika vituo vya ZSTC.

Vilevile, wakulima wakati wakizipeleka katika vituo vya ZSTC, mbali ya kutumia fedha kuzisafirisha pia hutumia muda mwingi njiani na kwenye vituo. Hapo upo msururu wa mchakato wa ununuzi, ukaguzi wa hali ya karafuu, kuzipima, kuandika karatasi za malipo na hatimaye ndio mkulima alipwe na aanze safari ya kurudi nyumbani.

Pamoja na haya yamekuwapo malalamiko mengi juu ya urasimu na hadaa katika vituo vya ununuzi vya ZSTC unaofanywa na baadhi ya wafanyakazi.

Haya nayo, ijapokuwa mengine siyo ya kweli, hayafai kupuuzwa.

Kauli za Serikali za kuimarisha ulinzi ardhini na baharini ili kudhibiti biashara ya magendo zimesikika mara kwa mara miaka nenda miaka rudi na bado biashara ya magendo haijasita.

Adhabu kali zimewekwa kwa watu wanaokamatwa wakishiriki kusafirisha karafauu kwa magendo, ikiwa pamoja na ile ya kifo (lakini hakuna mtu mmoja aliyekamatwa aliyenyongwa kwa kushiriki kusafirisha karafuu kwa magendo).

Lakini bado wanaojihusisha na biashara hii hawajatetereka na wanaendesha shughuli hizi kwa raha zao.

Ni vizuri suala hili likaangaliwa kwa uhalisia wake badala ya kutafuta njia za mkato na kauli kali ambazo uzoefu umeonyesha hazijasaidia kudhibiti biashara ya magendo ya zao hili.

Kama nilivyogusia hapo mwanzo suala hili limezungukwa na mengi, mbali ya bei nzuri anayopata mkulima anayeuza karafuu zake kwa wafanya biashara binafsi wanaozisafirisha karafuu nje ya nchi kwa magendo.

Hili la siasa na hisia za wakulima wa karafuu za kwa nini ni zao hili tu ndiyo linadhibitiwa na Serikali na siyo biashara nyingine halifai kupuuzwa.

Hapana ubishi kuwa karafuu ni tegemeo kubwa la fedha za kigeni kwa Serikali ya Zanzibar, lakini pia ndiyo tegemeo kubwa la kujikwamua na ugumu wa maisha la watu wa Kisiwa cha Pemba.

Ni vizuri kuliangalia kwa umakini pande zote mbili za sarafu.

Si siri kwamba wakulima wa karafuu wamekuwa wakilalamika kwamba hawatendewi haki.

Wanachotaka wao ni kuuza karafuu zao kwa bei wanayoona ina faida kwao, kwa wakati wanaotaka wao na kwa mnunuzi wanayemtaka kama ilivyo kwa mwenye kuuza mpunga, nyanya, maharage au dhahabu.

Ni vizuri kwa Serikali kulitafakari suala hili kwa umakini.

Vinginevyo biashara ya magendo, licha ya juhudi za kuidhibiti, itaendelea kushamiri kwa sababu kila Serikali ikija na mkakati mipya ya kuidhibiti hao wanaofanya biashara hii nao hutafuta mbinu mpya za usafirishaji.     

Advertisement