Marufuku ya uvamizi kwenye mito izingatiwe

Saturday February 15 2020

 

Sikio la kufa halisikii dawa, huo ndio msemo ambao unaweza kuleta maana kwa hali tunayoishuhudia katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko kufuatia mvua zinazoendelea.

Katika hilo, hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Masika kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikiwamo mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba,

Maeneo mengine ni Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

TMA imehadharisha kuwa mvua za masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, maeneo mengi ya mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mashariki mwa mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo mvua hizo zitakuwa na madhara yakiwamo mafuriko, lakini kabla ya mvua hizo tayari kulikuwa na hali kama hiyo, huku jiji la Dar es Salaam likiwa kinara.

Maeneo mbalimbali ya nchi yamekuwa yakipata athari kufuatia mvua hizo ikiwemo mafuriko hata katika mikoa ambayo hapo awali haikuwahi kuwa na historia ya matukio ya aina hiyo.

Advertisement

Hii inatokana na namna watu walivyovamia katika maeneo ambayo hasa yalipaswa kuwa njia ya maji na kuendesha shughuli za kibinadamu mfano kuanzisha makazi, ujenzi na hata kuchimba mchanga bila kufuata utaratibu.

Ikinyesha mvua ya saa moja lazima usikie kuna barabara zimefungwa hii inatokana na maji kuzuiliwa katika njia zake na kuongezwa kwa njia hizo. Pale Jangwani imeshakuwa eneo korofi kama ilivyo kwa bonde la Mkwajuni na Msimbazi.

Kila mwaka tumekuwa tukishuhudia watu wakilia kuharibiwa kwa nyumba au vitu vyao kusombwa na maji kwa sababu ya mafuriko, lakini baada ya muda wanarejea tena kuendelea na maisha yao kama kawaida.

Wakati bado suluhisho la maeneo hayo halijapatikana tunaona maeneo mengine ya pembezoni mwa mji nayo yameanza kufuata mkumbo huo. Watu wanajenga kwenye vyanzo vya maji na kuchimba mchanga bila kizuizi.

Mara kadhaa nimekuwa nikisikia upigaji marufuku wa shughuli hizo na hata kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu wanaokutwa kwenye maeneo hayo, na hivi karibuni wamesikika watendaji wa Bonde la Wami Ruvu wakipigia kelele suala hilo walipofanya ziara ya kushtukiza katika Bonde la Mto Tegeta.

Huenda maafa makubwa yakatokea jirani na bonde hilo kutokana na watu kuvamia na kuanzisha makazi. Tayari baadhi ya nyumba zimeshaanza kuathiriwa kwa kusombwa na maji zipo pia ambazo zimeanza kukatika kidogo kidogo.

Ofisa wa maji katika Bonde la Wami Ruvu Simon Ngonyani alisikika akiwaomba wananchi kuondoka kwenye maeneo ya mito na kuwasisitiza wasiweke makazi katika maeneo hayo kwa kuwa ni mazingira hatarishi na nyumba zao zinaweza kusombwa na maji.

Napata wasiwasi iwapo kwa mvua hizo zilizotangazwa na TMA kwamba hawa wavamizi walioweka makazi katika mabonde na kwenye vyanzo vingine vya maji watapona. Au wataiongezea serikali mzigo wa kuwapa huduma za dharura ilihali wanajua kuwa wanafanya shughuli zao na kuishi katika maeneo hatarishi.

Najiuliza, hivi tutaendelea kuombwa hadi lini katika mambo yanayotuhusu na yanayotishia usalama wetu. Inasikitisha kuona bado kuna watu hawataki kusikia hata wanapotahadharishwa wasiingie kwenye hatari.

Yaani usalama wako mwenyewe na familia yako lakini bado unaombwa na kubembelezwa kuepushwa na matatizo ambayo mwenyewe unapambania kuyavaa. Inashangaza mno.

Sheria inaelekeza wazi kwamba hakuna anayeruhusiwa kujenga ndani ya mita 60 za chanzo cha maji, ila ukipita katika maeneo mengi ya Jiji la Dar ni kama watu wameweka pamba masikioni.

Vilevile uchimbaji holela wa mchanga kwenye mito unasababisha kuongezeka kwa upana wa kingo za mto na hatimaye kusababisha maji kuvamia makazi ya watu.

Ajabu ni kwamba wakati mwingine watu wanaishi jirani na mito wanaangalia magari yakipita kuelekea mitoni kwa ajili ya kubeba mchanga. Wanakaa kimya kwa kile wanachodai hayawahusu. Matokeo ya kutojihusisha kwao ndiyo haya tunayoyasikia yanatokea.

Kila mtu hana budi kukumbuka kwamba maji yanafuata mkondo wake, hata ukifanikiwa ukiyazuia kwa miaka 10 ipo siku yatatafuta njia yake na hapo ndipo utasikia watu wanaomba serikali iingilie kati.

Sawa, serikali itatoa msaada kwa waathirika lakini tujiulize itafanya hivyo hadi lini, kwa nini tusijaribu kufuata sheria ili kupunguza uwezekano wa kutumia fedha kwa vitu ambavyo vinaweza kuzuilika?

endapo wote kwa pamoja tutaamua.

Hatutakatai dharura inaweza kutokea lakini basi iwe dharura kweli lakini sio kuifuata hatari mahali ilipo.

Basi tusikilize hata tahadhari iliyotolewa na TMA, jamani kuna mvua kubwa za juu ya wastani zinakuja na zinatarajiwa kunyesha kwa miezi miwili katika baadhi ya maeneo