Bale akubali yaishe kwa Zidane

Friday April 3 2020

 

Madrid, Hispania. Mshambuliaji wa Real Madrid, Gareth Bale yupo tayari kuondoa kinyongo dhidi ya kocha wake, Zinedine Zidane ili kurejesha uhusiano wao vizuri na amepanga kupigania namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Bale na Zidane walitofautiana msimu uliopita kocha huyo alipoanza kumuweka benchi mchezaji huyo hali iliyomlazimu kuanza kusaka timu ya kuhamia, jambo lililomfanya kuhusishwa na timu nyingi zikiwamo za China. Hata hivyo, mabosi wa Real walizima mpango huo baada ya majeruhi kuongezeka katika timu hiyo.

Tangu wakati huo, mchezaji huyo na kocha wake wamekuwa hawaivi hali iliyoelezwa kwamba imeathiri kwa kiasi kikubwa kiwango cha Bale ambacho kimeporomoka zaidi na hivyo kumuondoa kabisa katika kikosi cha kwanza cha wababe hao wa Santiago Bernabeu.

Kwa mujibu wa gazeti la The Mirror la Uingereza, mchezaji huyo amekuwa akifanya ‘mawasiliano ya kirafiki’ na Zidane katika juhudi zake za kutaka kumsogeza karibu kocha huyo ili aendeleze kipaji chake.

Hata hivyo, habari iliyochapishwa katika jarida la Diario la Hispania ilisema juzi kuwa, ifikapo Juni 30 mikataba ya wachezaji 37 klabuni hapo itahitaji kujadiliwa upya na huenda Bale aliyeifungia Real mabao 80 katika mechi 169 akaingia katika kundi hilo linalohusisha nyota wa kikosi cha kwanza, pili, tatu na vile vya vijana wa umri tofauti.

Vyombo vya habari vya Uingereza vimekuwa vikimhusisha mchezaji huyo kurejea Tottenham, lakini pia Manchester United, Chelsea na klabu za Italia na China zinamtolea macho mchezaji huyo wa kimataifa wa Wales.

Advertisement


Advertisement