Kagere atupiwa mzigo wa Alliance CCM Kirumba

Saddam Sadick, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara, Meddie Kagere, anatarajiwa kurudi uwanjani leo wakati mabingwa mara mbili mfululizo, Simba watakapowakabili Alliance, katika mechi ya pili ugenini katika ligi kwa kocha mpya, Sven Vandenbroeck.

Kagere aliyetupia mabao 10 hadi sasa katika ligi baada ya raundi 15, hakuwapo katika mechi iliyopita hapa Mwanza ambayo Wekundu wa Msimbazi walishinda 2-1 dhidi ya Mbao FC,

shukrani kwa bao la shuti la roketi kutokea mbali la kiungo Hassan Dilunga ‘HD’ na Jonas

Mkude aliyetumia asisti ya kona ya Ibrahim Ajib. Straika huyo raia wa Rwanda alikuwa akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Itakuwa ni mechi ya tatu ya ligi kwa kocha Mbelgiji, Sven, aliyerithi kiti cha Mbelgiji mwenzake Patrick Aussems aliyeonyeshwa mlango wa kutokea Msimbazi. Katika mechi ya kwanza Sven alitoka sare ya 2-2 dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa na ya pili ilikuwa ni dhidi ya Mbao

Alhamisi. Sven ameiongoza Simba katika jumla ya mechi tano, tatu nyingine zikiwa ni za Kombe la Mapinduzi, ambako alishinda mbili na kupoteza moja ya fainali walipolala 1-0 dhidi ya Mtibwa waliobeba taji hilo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Katika mechi ya leo, Simba inawania kuendeleza rekodi yake ya ushindi wa asilimia 100 dhidi ya Alliance, ambao wamekutana nao mara mbili na kushinda zote tangu timu hiyo ya Mwanza ipande daraja msimu uliopita. Mehi ya mwisho kukutana timu hizo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, huku mchezo wa awali uliopigwa kwenye dimba la Taifa Dar es Salaam, Alliance walichakazwa kwa mabao 5-1.

Mpambano wa leo unatazamwa kuwa mgumu kwani Alliance watakuwa wakipambana kuvunja uteja na kulipa kisasi, huku Wekundu wakihitaji kuendeleza rekodi yao nzuri.

Simba inaongoza Ligi kwa pointi 38 baada ya mechi 15, huku Alliance wakiwa na alama 20 katika nafasi ya 12 baada ya kushuka uwanjani mara 16.

Kocha wa Alliance, Fredy Felix ‘Minziro’ alisema ikiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu apewe majukumu kuiongoza timu hiyo, anahitaji ushindi ili kuanza vyema kibarua chake.

Alisema anaamini mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na kila timu kuhitaji ushindi, hivyo wanashuka uwanjani kwa lengo la kupambana kuvunja mwiko kwa vigogo hao wa Ligi Kuu.

“Ni kweli Alliance haijawahi kushinda mbele ya Simba, lakini kila kitu kina muda wake, kikubwa tuombe uzima, mengine tutazungumza baada ya dakika 90,” alisema Minziro.

Kwa upande wake Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema kurejea kwa kinara Kagere kunaongeza nguvu kikosini katika vita ya kusaka ushindi.

“Timu iko vizuri na matarajio yetu ni kushinda mechi hiyo, tayari Kagere amerejea baada ya kumaliza adhabu yake ya kadi tatu za njano, hata Hassan Dilunga yuko fiti,” alisema meneja huyo.