Nyota mpya afunguka vita ya namba Simba

Tuesday June 25 2019

 

By Thobias Sebastian, Mwananchi

Dar es Salaam. Shiza Kichuya ni miongoni mwa wachezaji wa Simba na timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ wa kizazi kipya walioitendea haki nafasi ya kiungo wa pembeni kwa kasi yake uwanjani.

Katika kuthibitisha hilo, tangu kiungo huyo anayeshambulia akitokea pembeni upande wa kulia, Simba haijatulia kwani imekuwa ikibadili mfumo wa uchezaji mara kwa mara kulingana na aina ya mechi.

Akiwa na umbo dogo kama ilivyokuwa kwa nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Abubakar Salum ‘Sure Boy’, Kichuya alikuwa mfungaji hodari wa mabao katika kikosi cha Simba.

Pengo la Kichuya aliyekuwa katika ubora wake msimu wake wa kwanza 2016-2017 baada ya kusajiliwa kimafia na aliyekuwa Kocha Joseph Omog.

Hata hivyo, ujio wa Patrick Aussems haukuwa mzuri kwa winga huyo kwani taratibu alianza kupoteza namba mbele ya mastaa wapya akina Hassani Dilunga, Clatous Chama pengine hata kwa kinda Rashid Juma na mkongwe Emmanuel Okwi.

Pamoja na kubadili kikosi mara kwa mara katika nafasi ya kiungo wa penbeni, Aussems alibaini kuna upungufu ndipo alipoamua kumbeba jumla Miraji Athumani akitokea Lipuli ya Iringa.

Advertisement

Miraji alicheza kwa mafanikio chini ya kocha na nahodha wa zamani wa Simba, Selemani Matola katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Kiwango chake kilimshawishi Aussems kuacha agizo kwa uongozi wa klabu hiyo akiwataka wamletee Miraji ambaye ni zao la Simba kwani alipita katika kikosi cha vijana kabla ya kutimkia Toto African na Lipuli

Miraji amerejea nyumbani na msimu ujao atavaa uzi wa rangi nyeupe na nyekundu baada ya kuipa mafanikio Lipuli katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho FA ambapo timu hiyo ilifungwa na Azam katika mechi ya fainali kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi.

Mchezaji sasa anakwenda Simba kupigania namba ambayo akiwa Lipuli aliimiliki vyema, hivyo ana kibarua kigumu cha kuwapiku akina Dilunga kupata nafasi.

Miraji anatakiwa kufanya kazi ya ziada kumhakikishia Mbelgiji Aussems hakufanya kosa kupendekeza jina lake katika ripoti aliyoacha kwa vigogo wa Simba.

Kauli ya Miraji

Wakati kukiwa na wasiwasi kama Miraji atapata namba Simba, winga huyo anasema hana hofu kwa kuwa anajiamini ni mchezaji hodari ndio maana amesajiliwa na klabu hiyo.

“Siwezi kukata tamaa imani yangu nakwenda kukutana na changamoto ambayo natakiwa kuikabili na kushinda ili niweze kutimiza malengo yangu ya kucheza

“Nafahamu wachezaji ambao wapo Simba ni wakubwa na wana uzoefu lakini nitakuwa namsikiliza kocha anataka nifanye nini katika na kufanya kazi,” anasema Miraji.

Miraji anasema anatambua Simba ni klabu kubwa tofauti na Lipuli lakini hana namna zaidi ya kupambana kupata katika kikosi cha kwanza ambacho kitamhakikishia nafasi ya kuitwa Taifa Stars.

“Narejea Simba kwa mara ya pili, mara ya kwanza nilionekana mdogo nilipandishwa kutoka timu ya vijana kwa maana hiyo ni mzoefu na nafahamu mambo mengi na hata ukubwa na presha ya timu naifahamu,”anasema Miraji.

Miraji alikuwa kikosi cha Taifa Stars kilichokwenda Misri kwa fainali za Afcon, lakini hakuwemo katika orodha ya nyota 23 waliobaki nchini humo.

Miraji anasema ndoto yake ya kurejea Simba imetimia kwa kuwa awali aliondoka kwenda kukuza kiwango chake Toto African kabla ya kutua Lipuli.

Advertisement