Rekodi hii kuibeba Simba kwa Mtibwa

Muktasari:

  • Mtibwa iliwahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1999 na 2000 imefunga mabao matatu tu katika mechi hizo 10, imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara 11 na haikuwahi kuifunga Simba kwa miaka sita tangu iliposhinda 2-0 Februari 24,2013.

Dar es Salaam. Wakati Simba leo inateremka uwanjani kuikabili Mtibwa Sugar, rekodi nzuri ya timu hiyo inaipa nafasi ya kushinda mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ingawa Mtibwa inaonekana ni timu ngumu kufungika inapocheza mechi kubwa, haina rekodi nzuri dhidi ya Simba. Katika michezo 10 ya Ligi Kuu Tanzania Bara miamba hiyo ilipokutana kwa misimu mitano iliyopita, imefungwa mechi sita na nne zilitoka sare.

Pia Mtibwa iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1999 na 2000 imefunga mabao matatu tu katika mechi hizo 10, imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara 11 na haikuwahi kuifunga Simba kwa miaka sita tangu iliposhinda 2-0 Februari 24,2013.

Rekodi hiyo inaipa Simba nafasi ya kushinda mchezo ambao ni muhimu kwa timu hiyo kupata pointi tatu ili kujisafishia njia ya kutwaa ubingwa mapema kabla ya mashindano hayo kumalizika Mei 28.

Pamoja na rekodi hiyo, umakini na utulivu wa mabeki na washambuliaji wa Simba dhidi ya Mtibwa na nyingine mbili zitakazofuata baina yao na Ndanda FC kabla ya kuivaa Singida United, ndio silaha ya kuwaweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Baada ya kupata matokeo wasiotarajia ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na suluhu ilipocheza na Azam, Simba imelazimika kuingia kwenye hesabu mpya ambazo ni kushinda mechi tatu kati ya tano zilizobaki ili iweze kutwaa ubingwa.

Mabeki wa Simba leo wanapaswa kuongeza umakini na nidhamu ya hali ya juu kimchezo ili timu yao ivune pointi tatu ambazo zitairejesha katika uongozi wa ligi kwani itafikisha pointi 85.

Vinginevyo udhaifu huo unaweza kutumiwa vyema na Mtibwa ambayo imekuwa na wachezaji wenye kasi hasa wale wa pembeni ambao ndio chachu ya kuzalisha mabao ya timu hiyo katika mechi wanazocheza.

Kasoro kubwa ya safu ya ulinzi ya Simba ni kukosa mawasiliano jambo ambalo limeifanya iwe inaruhusu mabao mepesi na kudhihirisha hilo, katika mechi dhidi ya Kagera Sugar beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alijifunga baada ya kutowasiliana vyema na kipa wake Aishi Manula.

Pia bao la Rahidhin Hafidh walilofungwa katika mechi waliyopa ushindi wa mabao 8-1 dhidi ya Coastal Union, lilitokana na kutegeana kwa mabeki wa Simba.

“Hatukucheza vizuri dhidi ya Kagera Sugar na tulistahili kupoteza mechi, lakini mchezo na Azam tulicheza kwa kiwango bora ingawa hatukuwa na bahati. Hatukuwa wabunifu kwasababu unapopata kona zaidi ya 13 katika mechi moja na ukashindwa kupata bao hilo linakuwa ni tatizo,” alisema Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu.

Hata hivyo, Simba ikitumia udhaifu wa safu ya ulinzi ya Mtibwa ambayo imekuwa ikifanya makosa ya mara kwa mara, inaweza kupata mabao ambayo huenda yakawafanya waibuke na ushindi katika mechi hiyo.

“Tunachukulia kwa uzito mchezo huu, ikumbukwe KMC wameshinda hivyo tumeshushwa kwa nafasi moja na tukishinda tunarudi pale,” alisema Kocha wa Mtibwa Zuberi Katwila.