Changalawe apigwa mabondia Tanzania wakosa tiketi ya Olimpiki Japan

Muktasari:

Nafasi pekee iliyosalia ya kufuzu Olimpiki kwa mabondia wa Tanzania ni mashindano ya dunia baadae Mei mjini Paris, Ufaransa endapo watamudu gharama za kuipeleka timu.

Dar es Salaam.Kipigo cha pointi alichopata bondia Yusuph Changalawe kimefifisha ndoto ya mabondia wa Tanzania kufuzu kushiriki Olimpiki 2020 Japan msimu huu.

Changalawe alianza vema pambano lake la awali kwa kumchapa, Martins Mauricio Paulo wa Guinea Bissau ameshindwa kuendeleza rekodi hiyo katika pambano la pili lililopigwa usiku wa kuamkia leo huko Dakar, Senegal.

Changalawe alikung'utwa na Samed Shakul wa Ghana anakuwa Mtanzania wa nne kupoteza nafasi ya kufuzu Olimpiki msimu huu baada ya Haruna Swanga, Alex Isendi na Mligwa Kaji kupigwa na kuondolewa mashindanoni.

Kwa matokeo hayo ya mashindano ya Afrika yanapelekea nafasi ya mabondia wa Tanzania kufuzu kushiriki Olimpiki ikiwa ngumu zaidi.

Nafasi pekee iliyosalia ya kufuzu Olimpiki kwa mabondia wa Tanzania ni mashindano ya dunia baadae Mei mjini Paris, Ufaransa endapo watamudu gharama za kuipeleka timu.

Kwenye mashindano ya Afrika yanayofungwa kesho Alhamisi, mabondia hao sanjari na kocha na mkuu wa msafara waligharamiwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).