Kilimanjaro Stars yaanza vibaya mashindano ya Chalenji

Muktasari:

Stars haijatwaa ubingwa wa mashindano ya Chalenji tangu mwaka 2010 ilipotwaa baada ya kuichapa Ivory Coast kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali.

Kampala, Uganda. Timu ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' imeanza vibaya mashindano ya Chalenji baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Kenya katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa KCCA jijini Kampala.

Bao lililoizamisha Stars katika mchezo wa leo lilifungwa mapema dakika ya tatu na Abdallah Hassan akimalizia pasi nzuri aliyopewa na Oscar Wamalwa.

Wamalwa aliwazidi ujanja walinzi wa Stars walioshindwa kumdhibiti ndani ya eneo la hatari na kupenyeza pasi hiyo kwa Hassan ambaye alibaki anatazamana na kipa Aishi Manula na kuujaza mpira wavuni.

Mara baada ya kuingia kwa bao hilo, Stars walionekana kuamka na kumiliki mpira wakijaribu kupenya kuingia langoni mwa wapinzani wao lakini hata hivyo kukosekana kwa ubunifu kwenye kutumia mipira ya mwisho wakiwa wamelisogelea lango la Kenya.

Kiungo mshambuliaji Lucas Kikoti aliyekuwa na jukumu la kuwachezesha washambuliaji, alishindwa kuhimili vishindo vya Kenya na kujikuta akitolewa huku nafasi yake ikichukuliwa na Eliuter Mpepo katika dakika ya 42.

Timu hizo zilikwenda mapumziko Kenya ikiwa mbele kwa bao hilo moja.

Mabadiliko yaliyofanywa katika dakika ya 63 yaliyofanywa na kocha Juma Mgunda aliyemtoa Paul Nonga na kumuingiza Ditram Nchimbi, yaliipa nguvu zaidi Stars ambayo ililipiga presha lango la Kenya mara kwa mara lakini walishindwa kuziona nyavu za wapinzani wao.

Hadi mwamuzi Ali Sabila kutoka Uganda anapuliza kipyenga cha kuashiria kumalizika kwa mchezo huo, matokeo yalibaki kama yalivyo na kuifanya Stars ikae mkiani mwa kundi B.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, kocha Juma Mgunda alisema wameadhibiwa kutokana na makosa yao.

"Tulifanya kosa la mapema ambalo wapinzani wamelitumia kupata bao la mapema. Tumejitahidi kutengeneza nafasi lakini mwisho wa siku hatukuwa na bahati lakini tunajipanga kwa ajili ya mchezo unaofuata dhidi ya Zanzibar," alisema Mgunda