Ronaldo audhika kuikosa Barcelona

Muktasari:

Ureno imesema ilimpima mara 18 na mara zote aligundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Turin, Italia (AFP). Mwanasoka nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo ameachwa katika kikosi cha Juventus kinachocheza mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya leo Jumatano dhidi ya Barcelona jijini Turin, ikiwa ni wiki mbili baada ya vipimo kuonyesha ana maambukizi ya virusi vya corona.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 35 na ambaye anaongoza kwa kufunga mabao katika historia ya michuano hiyo akiwa amefunga mabao 130, alihitaji kuonekana hana virusi hivyo saa 24 kabla ya mechi dhidi ya timu ya mpinzani wake mkubwa, Lionel Messi.

Akiwa mwenye hasira, Ronaldo aliweka picha yake katika akaunti yake ya Instagram, akiambatanisha na maneno yasemayo: "Najisikia vizuri na mwenye afya! Forza Juve! #finoallafine."

Aliongeza maneno kuhusu upimaji virusi akisema: "PCR ni ovyo".

Baadaye Ronaldo, ambaye ana zaidi ya wafuasi milioni 241 wa Instagram, aliondoa maneno hayo.

Kwa mara ya kwanza Ronaldo alipimwa na kugundulika ana Covid-19 wiki mbili zilizopita wakati akiichezea nchi yake ya Ureno, na amejitenga tangu arejee Italia.

Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha TV1, Ronaldo ambaye ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora mara tano, mara zote 18 alizopimwa, aligundulika kuwa na maambukizi.