Simba SC ilikosea hapa

Dar es Salaam. Benchi la ufundi la Simba lina kila sababu ya kuitazama na kuongeza ufanisi katika safu yake ya ushambuliaji, vinginevyo inaweza kuwagharimu kwenye mechi tano zilizobaki za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Matokeo ya suluhu dhidi ya Azam FC jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, yanatoa ishara isiyo nzuri kwa Simba hasa kipindi hiki muhimu ambacho vita ya kuwania ubingwa imepamba moto.

Ni sare ambayo sio tu imezidi kuichelewesha Simba kutwaa ubingwa pia ni muendelezo wa safu ya ushambuliaji kutofunga bao ikiwa ni mechi ya pili baada ya kushindwa kwa Kagera Sugar ilipolazwa bao 1-0 kwenye uwanja huo.

Baada ya kupata ushindi wa taabu dhidi ya Mbeya City, Prisons, JKT Tanzania wa bao 1-0 katika kila mchezo, Simba ilirudisha matumaini kwa kuibanjua Coastal Union 8-1, lakini kutofunga dhidi ya Kagera Sugar na Azam FC, kunaweza kuleta wasiwasi.

Ikiwa timu pinzani zitafanyia kazi kile kilichofanywa na safu ya ulinzi ya Kagera Sugar na Azam, hali inaweza kuwa ngumu kwa Simba katika mechi tano zinazofuata ambazo inahitajika kupata ushindi katika michezo kitatu tu ili itangaze ubingwa.

Ingawa Azam haipo katika mbio za ubingwa, mchezo wa jana ulikuwa wa kujiimarisha katika nafasi ya tatu, kulinda heshima na kumaliza unyonge walionao mbele ya Simba ambao hawajawafunga katika mechi nne mfululizo walizokutana kwa miaka miwili na miezi mitatu.

Timu hizo jana zilionyesha tamaa ya kusaka ushindi na hata namna mpangilio wa vikosi vyao ulionyesha kuwa mpango mkuu ni kushambulia na si kujilinda.

Timu zote mbili zilianza na mfumo wa 4-4-2 huku vikosi vikiwa na kundi kubwa la wachezaji ambao aina ya soka lao ni la kushambulia, Azam ikiwa na mawinga asili wawili, washambuliaji wawili na kiungo mmoja mshambuliaji.

Simba ilianza na viungo wanne lakini kati yao watatu ni wa ushambuliaji ikionekana ni mkakati wa kuhakikisha inamiliki zaidi mpira na kutengeneza nafasi.

Upangaji wa vikosi ulishabihiana na kile kilichotokea ndani ya uwanja kwani timu hizo zilicheza soka la kushambuliana kuanzia dakika ya mwanzo ingawa mara kwa mara hali ya uwanja uliokuwa na maji katika baadhi ya maeneo ilitibua mipango yao katika kusaka mabao.

Miongoni mwa nafasi nzuri ambazo Azam ilipata ni ile ambayo Donald Ngoma alipoteza dakika ya 29 akiwa anatazama lango, alipiga shuti juu.

Shambulizi la Ngoma lilikuwa kama ni kulipa lile lililofanywa na Simba dakika mbili kabla kupitia kwa Meddie Kagere ambaye alipiga shuti lililodakwa na kipa wa Azam, Razak Abalora baada ya kupokea pasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, Haruna Niyonzima, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi

Azam: Razak Abalora, Nico Wadada, Bruce Kangwa, Yakub Mohamed, Aggrey Morris, Stephan Kingue, Ramadhan Singano, Frank Domayo, Obrey Chirwa, Donald Ngoma, Joseph Mahundi.