Simba SC ilivyotibua dili la Kotei Yanga

Monday January 13 2020

 

By MWANDISHI WETU

UNAKUMBUKA dili la Luis Jose Miquissone lilivyobadilika ghafla kutoka Yanga na kutua Simba, sasa unaambiwa mambo yamehamia kwa kiungo fundi wa kukaba, Mghana James Kotei ambaye kwa mara ya pili dili lake la kutaka kutua Jangwani limetibuliwa na mabosi wa Msimbazi.

Yanga ilikuwa mbioni kumleta Kotei nchini tayari kwa kujiunga na timu yao ikiwa ni mara ya pili kwa klabu hiyo kuhitaji huduma ya kiungo huyo mkabaji kwa nyakati tofauti.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Kotei aliyeitumikia Simba kwa miaka minne alionyesha nia akiwa usoni na mabosi wa Yanga lakini walipompa kisogo akawatosa.

Sababu kubwa ambayo Kotei imemfanya kusita kujiunga na Yanga ni juu ya kuitumikia Simba ambapo aliogopa kupata wakati mgumu kuwatumikia wapinzani wao wa upande wa pili.

Awali mara baada ya mabosi wa Yanga na Kaizer Chiefs anayoichezea kufanya mazungumzo ya kutaka kumleta Jangwani, aliamua kufanya mawasiliano na bosi mmoja wa Simba na kuwashirikisha dili lake lote juu ya kuhitajiwa Jangwani na mabosi hao kuamua kumtia ‘sumu’ ili asitue Yanga.

Mbali na kuumwa sikio na watu wa Simba, pia Kotei mwenyewe ameonyesha kutofurahishwa na hatua ya klabu yake Kaizer Chiefs kumlazimisha kujiunga na Yanga bila ridhaa yake.

Advertisement

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kwamba Kaizer maarufu kwa jina kama Amakhosi hawakuwa wanakubali kiwango cha Kotei tangu asajiliwe mkataba wa miaka mitatu ambapo mbadala wake alikuwa ni Mkenya Antony Akumu wiki iliyopita alikuwa Afrika Kusini kukamilisha dili hilo.

Hata hivyo, Amakhosi ilitakiwa ili kupata nafasi ya kumsajili Akumu ni lazima imuondoe mchezaji mmoja wa kigeni na karata ikatua kwa Kotei ambaye hakufanikiwa kucheza hata mechi mbili za ligi na klabu hiyo.

TATIZO NI HILI

Katika mazungumzo yake na bosi wa Simba, Kotei mbali na kuogopa kuhamia kwa mahasimu wa klabu hao, lakini kiungo huyo ameonyesha kuihusudu sana klabu hiyo akikumbuka jinsi alivyosaidiwa na mmoja wa vigogo wa klabu hiyo wakati akitua kwa mara ya kwanza nchini.

Kiungo huyo alienda mbali zaidi akiwataka mabosi hao kuwahamasisha wachezaji kuhakikisha wanashinda mchezo wa fainali wa Kombe la Mapinduzi.

MENEJA ATIBUA ZAIDI

Wakati Yanga na Amakhosi wakijadiliana katika dili hilo kiungo huyo alitoa sharti la kumtaka meneja wake kushirikishwa katika mchakato huo. Klabu zote mbili zilikubali ushauri huo ambapo baada ya meneja huyo kutumiwa tiketi ya ndege ya daraja la uchumi (economy) aliigomea akisema anataka apewe tiketi ya daraja la biashara (business) kama ambavyo mkataba wao na Amakhosi unavyoeleza.

Inaelezwa baadaye meneja huyo alikuwa mgumu kupokea simu na kuzidi kuweka ugumu wa ukamilifu wa dili hilo.

AVUNJIWA MKATABA

Jana taarifa kutoka Afrika Kusini zilionyesha tayari Amakhosi imeamua kumvunjia mkataba kiungo huyo baada ya kuona anataka kuwachelewesha kukamilisha usajili wa Akumu.

Hata hivyo, uamuzi huo haukumfurahisha kiungo huyo baada ya kudai haki zake zimeminywa katika fidia za kumvunjia mkataba akiona kama klabu hiyo imefanya hivyo kumkomoa kwa hatua yake ya kugomea kujiunga na Yanga.

“Kotei ameona kama amekomolewa unajua yeye anasema Keizer haiwezi kumlizimisha kuhamia klabu wanayotaka wao hasa kama yeye hataki kwenda huko nafikiri hapo utaona Kotei ni vigumu kutua Yanga,” alisema mmoja wa marafiki wa kiungo huyo.

ATIMKIA

Jana kiungo huyo tayari alisharejea kwao Ghana ambapo mke wake alimtaka arejee kuonana na mtoto wao wa kwanza aliyezaliwa hivi karibuni.

Hatua hiyo imeifanya Yanga kutafakari gia ya kumshawishi kiungo huyo.

Advertisement