Sio Zengwe: Kuna jambo kati ya Yanga SC na wadhamini

Tuesday March 24 2020

 

By Angetile Osiah

WAKATI Manchester United inamsaini kiungo Mfaransa, Paul Pogba kulikuwa na mengi yaliyozungumzwa kuhusu uhamisho wake. Wapo waliosema kitendo cha kuchelewa kumtangaza kilisababishwa na siku aliyosajiliwa kuwa sikukuu na hivyo hakukuwa na shughuli katika soko la hisa.
Wapo waliosema kilisababishwa na mvutano baina ya Man United na wakala wake ambaye ilidaiwa alitaka Dola 20 milioni kwa kufanikisha mpango huo.
Na wako waliozungumzia usajili kwa ujumla wakisema Man United haikumuhitaji Pogba, lakini watengenezaji wao wa vifaa, yaani Kampuni ya Adidas ndiyo ilikuwa ikimtaka kama taswira yake mpya. Hisia ilitokana na rekodi za huko nyuma kuwa Kampuni ya Nike iliyokuwa mtengenezaji wa vifaa wa klabu hiyo ilichukizwa na kitendo cha Man United kukataa kumrejesha Cristian Ronaldo.
Ni kweli wadhamini hufurahi wakati klabu zinapomsajili mchezaji nyota, mwenye mvuto ambaye husaidia kuongeza mauzo ya jezi kama ilivyo kwa nyota hao wawili; Ronaldo na Pogba.
Lakini mambo hayo hufanywa kisiri sana wala isijulikane kama kampuni ndiyo inayosukuma mchezaji fulani kusajiliwa kwa kuwa klabu hizo zina wadhamini wengi na hivyo kumpa nafasi mmoja kufanya shughuli za klabu kunampa nafasi kubwa ya kuonekana kuliko wadhamini wengine, yaani mmoja hunufaika wengine wanapoingilia shughuli za utendaji za klabu.
Ilitokea hivyo kwa Simba wakati wa msimu wa usajili wakati mdhamini mmoja alipohusika katika kuongeza mikataba wachezaji, akiweka logo ya kampuni yake zaidi na kusahau wadhamini wengine ambao wameweka fedha nyingi zaidi, hadi baadhi ya watu walipoguna na kudokeza kuwa hali haiendi vizuri.
Lakini hivi ndivyo ilivyo Yanga. Mdhamini mmoja amewafunika wengine kwa sababu uongozi ni kama umemuachia afanye shughuli za kila siku, ambazo kimsingi zingefanywa na sekretarieti.
Wakati fulani ilionekana hata viongozi walikuwa hawajui ni mchezaji gani anakuja. Ilionekana kama walistuka tu kuona mfanyakazi wa mdhamini wao ameenda uwanja wa ndege kumpokea. Vyombo vya habari vilidokeza kuwa kuna mchezaji anakuja, lakini viongozi walipoulizwa hawakujua kitu.
Baadaye kidogo tukaanza kuona maofisa habari wakiambatana na mfanyakazi wa mdhamini huyo kwenda kupokea mtu mwingine aliyesemekana kuwa ni mtaalamu wa mifumo.
Inawezekana wadhamini wengine hawalalamiki, lakini wanaona wameweka fedha zao kwa klabu ambayo haithamini udhamini na hivyo haiweki taratibu za jinsi ya kuwatangaza wanaoweka fedha katika klabu.
Hii si sawa. Wanaweza kunyamaza hadi mwisho na baadaye wakajiondoa wakieleza hawakufaidika na udhamini bila ya kuweka bayana kuwa kilichowaondoa ni uongozi kutojali udhamini wao kutokana na kumpa mmoja wa wadhamini nafasi kubwa zaidi ya wengine.
GSM, Taifa Gas na SportsPesa ndio wadhamini wakubwa wa Yanga kwa sasa, huku Azam akiweka fedha za haki za televisheni. SportsPesa ndiye anayeweka fedha nyingi na ndiye anayewekwa kifuani mwa jezi za Yanga, sehemu ambayo mwenye fedha nyingi angepapenda.
Hawa wote wanaangalia wananufaikaje na kila habari muhimu inayotoka Yanga. Wananufaika na habari ambazo ni viporo au wananufaika na habari mpya ambazo wangependa ziwafikie watu ili washiriki mchezo wa kubeti. Wadhamini wengi wanasubiri kuona thamani ya fedha zao.
Na hii itawezekana tu iwapo uongozi na sekretarieti watajiwekea mkakati wa kutangaza habari za Yanga, mkakati ambao utanufaisha wote waliotumbukiza fedha zao kwenye klabu hiyo na kuvuta wengine watakaona thamani wanayopata wenzao.
Na hili ni jambo ambalo klabu zetu hazilioni kama ni muhimu. Unaweza kukuta habari ambayo ni muhimu inatolewa na ofisa uchochoroni, inapokuja kutangazwa rasmi inakuwa haina ile thamani ambayo mdhamini aliitegemea. Tunahitaji kurekebisha utendaji katika klabu zetu ili kampuni zione thamani iliyopo na kuingiza fedha nyingi ambazo zinahitajika sana kuendeleza mpira wetu.

Advertisement