Advertisement

Sven asuka mbinu mpya Msimbazi

Friday October 16 2020
sven pic

UKIACHANA na mkakati wa mechi za kirafiki, Simba imejipanga na mechi dhidi ya Prisons, Oktoba 22 na benchi la ufundi linafanyia kazi mbinu tatu kali za kutumia katika mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Nelson Mandela, Rukwa.

Mbinu hizo ni kushambulia kwa kasi kupitia katikati huku wakipiga pasi fupi za harakaharaka, ile ya kushambulia kupitia pembeni hasa kwa wachezaji wanaocheza nafasi ya winga na ile ya kuwalazimisha wapinzani wao kufanya makosa katika safu ya ulinzi.

Ndani ya Bunju Complex, benchi la ufundi la Simba juzi awali liliwagawa wachezaji wake katika vikundi vidogovidogo vyenye wachezaji watano watano ambao walikaa pande mbili, kila mmoja alitakiwa kukokota mpira kwa umbali mfupi kisha kupiga pasi upande wa pili ambako alipaswa kukimbia kwa kasi kubwa kuelekea upande ambao ameupeleka mpira huo.

Baadaye wachezaji hao waligawanywa kwa timu mbili ambapo, walitakiwa kuifanyia kazi mbinu hiyo na kocha Sven Vandenbroeck aliwataka wachezaji kutokaa na mpira kwa muda mrefu katika kujenga mashambulizi na aliwalazimisha kila mmoja kutogusa mpira zaidi ya mara tatu pindi akiupokea na kisha kupiga pasi kwa haraka kwenda kwa mwenzake kuelekea langoni mwa wapinzani kisha kufunga mabao.

Katika aina hiyo ya mazoezi, Larry Bwalya, Luis Miquissone, Chris Mugalu na Shomari Kapombe walionekana kufanya vizuri zaidi kuchezesha wenzao na kutengeneza nafasi za mabao.

Ukiondoa hilo, baadaye wachezaji walielekezwa kupiga pasi za pembeni kwenda kwa mawinga ambao walipaswa kupiga pasi kwa haraka kwenda kwa washambuliaji wao ama kuingia ndani ya eneo la hatari na kufunga wenyewe.

Advertisement

Kana kwamba haitoshi, pia Simba walifanyia kazi mbinu ya kuwalazimisha mabeki wa timu pinzani kufanya makosa ambapo, wachezaji wake wa safu ya ushambuliaji na kiungo walitakiwa kuwafuata kwa spidi na wingi mabeki wa upande wa pili pindi wanapokuwa na mpira katika eneo lao na hivyo kuwalazimisha wabutue au wapoteze mpira jambo ambalo linakuwa na faida kwa upande wa Simba.

Kundi kubwa la wachezaji lilihudhuria mazoezi hayo isipokuwa John Bocco, Joash Onyango, Francis Kahata, Meddie Kagere, Hassan Dilunga, Pascal Wawa na Clatous Chama kwa sababu mbalimbali kwa mujibu wa Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu.

“Kahata na Onyango ndio wameingia hivyo wataanza mazoezi, Dilunga, Wawa na Chama wana ruhusa kutokana na dharura ya mvua, Kagere alikuwa na timu ya Taifa wakati Bocco naye kama ulivyomuona ameanza mazoezi mepesi,” alisema Rweyemanu.

Mwanaspoti liliwashuhudia Kahata na Onyango wakiwa katika gari ndogo ya Simba wakati wenzao wakiendelea na mazoezi wakati huo Bocco alikuwa akifanya mazoezi ya kutembea chini ya usimamizi wa Daktari wa Simba, Yassin Gembe na mtaalam wa viungo, Adel Zrane. Awali, kabla ya mazoezi ya mbinu kuanza, wachezaji watano wa Simba waliokuwa katika kikosi cha Taifa Stars, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Mzamiru Yassin, Said Ndemla na Jonas Mkude walifanya mazoezi ya kupimwa ufiti chini ya Zrane sambamba na Erasto Nyoni na baadaye walichanganywa na wenzao.

Mechi dhidi ya Prisons itakuwa ya nne kwa Simba kucheza ugenini msimu huu, ambapo katika mechi tatu za mwanzo dhidi ya Ihefu, Mtibwa na JKT imekusanya pointi saba.

Iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu, ikatoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar na ikaja kuichapa JKT Tanzania kwa mabao 4-0.

Advertisement