VIDEO: Uwanja wa Simba kuitwa Simba Mo Arena, Naibu Spika Tulia atia neno

Sunday December 8 2019

 

Dar es Salaam. Wanachama klabu ya Simba wamepitisha rasmi uamuzi wa kuuita uwanja wao Simba Mo Arena badala ya Simba Complex uliopo Bunju.

Jina hilo limepitishwa muda mfupi baada ya Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara kufanya harambee isiyo rasmi ya ujenzi wa uwanja huo katika meza kuu na kupata ahadi Sh 55.5milioni.

Baada ya harambee hiyo, wanachama walipitisha jina hilo na kuachana na lile la awali la Simba Complex.

Katika Harambee hiyo, mwenyekiti wa zamani wa Simba, Swedy Mkwabi aliahidi kutoa Sh5 Milioni, Hanspope Zacharia Sh10 Milioni, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson Sh 5 Milioni, kaimu mwenyekiti, Mwina Kaduguda mifuko 20 ya cement, Salim Abdallah Try again  Sh15 Milioni.

Wengine ni Seleman Haroub (500,000), MO Dewji 20 milioni wakati Haji Manara alitoa tofali 1000.

Naibu Spika Tulia atia neno

Advertisement

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema, yeye ni shabiki kindaki ndaki wa Simba, ila amekuwa akitamani mafanikio ya klabu hiyo yaonekane pia katika klabu nyingine za soka nchini.

Dk Tulia ametamka hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo unaoendelea jijini Dar es Salaam.

"Klabu ya Simba ni mfano wa kuigwa na klabu za upande wa pili," alisema Naibu Spika huku baadhi ya mashabiki wakimshangilia na kuitaja klabu ya Yanga.

Alisema licha ya kauli mbiu ya klabu hiyo ya 'Iga ufe ...this is next level' bado anatamani Simba iendelee kupiga hatua, lakini klabu zingine zisione tatizo kuiga.

Naibu Spika huyo alisema kama wabunge wako tayari kuchangia ujenzi wa Bunju Complex ambao awali, mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji alisema hadi ukamilike utagharimu Sh 2.5 Bilioni huku akibainisha yeye Dewji atachangia Sh 500 Milioni katika ujenzi huo.

"Hata wabunge tuko tayari kuchangia, zoezi litakapoanza na kule 'mjengoni' mje sababu Simba ina wabunge wengi nchi hii," alisema Naibu Spika huku akimtaja spika, Job Ndugai na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa miongoni mwao.

"Bungeni wanachama na mashabiki wa Simba ndio wengi, hao niliowataja ni kwa uchache tu niwapeni picha, hivyo Simba ni timu nyingine," alisema.

Aidha Naibu Spika alisema mafanikio ya Simba yataendelea kuonekana kwa ushirikiano baina ya wanachama, mashabiki, viongozi na wachezaji.

Advertisement