Bibi Mwenda adai fedha msiba wa mdogo wa Kanumba

Monday December 9 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Msanii wa filamu nchini Tanzania, Fatma Makongoro maarufu Bibi Mwenda amezua kizaazaa baada ya kusimama mbele  ya gari la kubeba maiti lililokuwa na mwili wa Seth Bosco, mdogo wa aliyekuwa nyota wa filamu nchini marehemu Steven Kanumba,  mpaka apewe fedha.

Tukio hilo limetokea leo Jumatatu Desemba 9, 2019 muda mfupi kabla ya mwili wa Seth kupelekwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Kimara Temboni kwa ajili ya ibada.

Hata hivyo,  msanii Nova aliyekuwepo wakati wa tukio hilo amesema alichokifanya Bibi Mwenda ni utani.

"Huu ni utani wao wa makabila si unajua huyu mama in Mkurya hivyo mpeni tu hela aondoke hapo," amesema Nova.

Bibi Mwenda aliyekuwa amevaa gauni la maua na kujitanda mtandio wa bluu bahari licha ya kuombwa na watu kupisha gari hilo aligoma, kusisitiza kuwa atafanya hivyo ikiwa atapatiwa fedha.

Licha ya mmoja wa waombolezaji kumpatia Sh10,000, msanii huyo alisema haitoshi, alipatiwa kiasi kingine na watu watatu na kupokea huku akichukua Sh1,000 kwa mmoja wa watu hao, “hiyo hela na wewe umeiacha ya nini, ilete hapa.” Hata hivyo baadaye aliondoka eneo hilo na shughuli za msiba kuendelea.

Advertisement

Advertisement