Diamond ampa tano Harmonize

Sunday March 15 2020

 

By Muyonga Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Siku moja baada ya msanii Rajab Abdul maarufu Harmonize kuzindua albamu yake aliyoipa jina la Afro East jijini hapa Diamond Platinumz ametumia ukurasa wake wa Instagram kuitangaza albamu hiyo.
Harmonize au Konde Boy mwaka jana alitangaza kuondoka kwenye lebo ya WCB ambayo mkurugenzi wake ni Diamond Platinumz na tangu alipoondoka hakukuwa na ukaribu wa wawili hao.
Diamond ana mchango mkubwa katika muziki wa Harmonize kwa sababu alikuwa msanii wa kwanza kumsainisha na kumtengenezea jina, jana hakuwepo ukumbini ila leo Machi 15 amewaomba watu mbalimbali kupakua na kusikiliza albamu hiyo mitandaoni.
Mbali na Diamond Platinumz pia kaka yake na Dj wake Romy Jons, dada yake Esma ni miongoni mwa watu waliotumia akaunti zao za Instagram kuitangaza albamu hiyo.
Albamu ya Afro East ina jumla ya nyimbo 18 ikiwashirikisha wasanii kutoka ndani na nje ya nchi uzinduzi wake ulihudhuriwa na wasanii mbalimbali na mgeni rasmi akiwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete katika ukumbi wa Mlimani City.
Uzinduzi huo ulijawa na ubunifu mbalimbali ikiwemo jukwaa lilivyokuwa linabadilishwa kutokana na maudhui ya wimbo husika, kutumia watu mbalimbali mashughuri kama watangazaji wa vyombo tofauti nchini kupanda na kutambulisha wimbo.
Baadhi ya nyimbo ambazo tayari zilianza kusikika mitaani ni pamoja na hujanikomoa na uno.

Advertisement