Fainali BSS kufanyika mkesha wa Krismasi, washiriki wamchanganya Rita Paulsen

Wednesday December 18 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Fainali za kumsaka mshindi wa shindano la Bongo Star Search (BSS), nchini Tanzania linatarajiwa kufanyika usiku wa kuamkia sikukuu ya Krismasi  ambapo mshindi anatarajiwa kuondoka na kitita cha Sh50,000 milioni.

Akizungumza leo Jumatano Desemba 18, 2019, Mkurugenzi wa kampuni ya Benchmark 360, Rita Paulsen ambaye ni muasisi wa shindano hilo amesema siku hiyo washiriki watakaoingia tano bora katika kipindi cha shindano hilo Jumapili ya wiki hii, ndiyo watakaochuana fainali.

Akizungumzia hali ya mchuano ya washiriki hao, amesema kila mmoja ni mkali kiasi kwamba anapata wakati mgumu kubashiri kina nani watafanikiwa kuingia kwenye tano bora miongoni mwa 10 wanaowania nafasi hiyo.

"Kama jaji mkuu wa shindano hili, napata wakati mgumu  kwani washiriki wote 10 waliobaki sasa hivi ni wakali na hata hao watano watakaoingia fainali najua watakuwa wakali pia, inanipa wakati mgumu kwa kweli sema ndio hivyo katika mashindano lazima apatikane mshindi," amesema Mkurugenzi huyo.

Kuhusu  zawadi, Rita amesema tofauti na kipindi cha nyuma ambapo mshindi alipewa Sh50 milioni yote, kwa mwaka huu atapewa  Sh30 milioni taslimu na Sh20 milioni  itawekezwa katika muziki wake ikiwamo kumuingiza studio na kumtafutia menejimenti ambayo itamsimamia mwaka mzima.

Amesema wamefanya hivyo baada ya kugundua wanaopewa zawadi hiyo kutofanyia shughuli za kujiendeleza kimuziki  kutokana na baadhi yao kutowahi kushika kiasi hicho cha fedha na hivyo kujikuta wanaielekeza katika mambo mengine.

Advertisement

Pia, amesema katika kipindi chote cha kusaka washiriki wa mashindano hayo  kwa mikoa mitano ikiwemo Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Dar es Salaam, wamekutana na washiriki zaidi ya 5,000.

Kwa upande wa Meneja Masoko wa kampuni ya Startimes ambao ni wadhamini wakuu wa shindano hilo, David Malisa amesema shughuli ya upigaji kura kwa watu itaanza Desemba 22, 2019 na itasitishwa Desemba 24,2019 saa 5:00 usiku.

“Mshindi atapatikana kwa kupigiwa kura asilimia 20 na mashabiki wanaofuatilia kupitia luninga na asilimia 80 ataipata kwa majaji, ”amesema Malisa.

Fainali hizo zitafanyika  katika ukumbi wa next-door Arena jijini Dar es Salaam na kiingilio itakuwa ni Sh20,000 kawaida, VIP Sh50,000 na VVIP Sh100,000.

Advertisement