Hiki ndicho kilichotokea mgahawa wa Harmonize unaotembea

Muktasari:

  • Msanii Rajab Abdul maarufu Harmonize amesema makubaliano mapya na kampuni ya Sayona ndio sababu ya mgahawa wa  ‘Konde Boy’ uliopo katika gari kutoonekana mtaani.

Dar es Salaam. Msanii Rajab Abdul maarufu Harmonize amesema makubaliano mapya na kampuni ya Sayona ndio sababu ya mgahawa wa  ‘Konde Boy’ uliopo katika gari kutoonekana mtaani.

Kupitia mgahawa huo uliozinduliwa Oktoba 20, 2019, msanii huyo anayetamba na wimbo Uno na Kainama hugawa chakula mitaani kinachokuwa kimefungashwa katika mifuko midogo iliyoandikwa ‘Konde Boy mgahawa’.

Gari hilo lilipangwa kupita mitaani kila Jumapili kugawa chakula na siku ya uzinduzi ziliibuka vurugu kutokana na waliojitokeza kusukumana, kila mmoja akitaka kupata chakula.

Akizungumza leo Jumatano Januari 15, 2019  katika mkutano na waandishi wa habari, Harmonize amesema sababu ya gari hilo kutoonekana mtaani ni makubaliano aliyoingia na Sayona.

Msanii huyo ambaye leo ametangazwa kuwa balozi wa kinywaji cha Twist amesema ugawaji wa chakula hicho ulifanyika kwa takribani wiki tano, baadaye kusitishwa baada ya kampuni ya Sayona kuomba kuwaunga mkono.

“Kutokana na hatua hii sasa tutakuwa na magari matatu badala ya moja. Yatakuwa yakipita mitaa mbalimbali na huenda siku za kutoa chakula ikaongezeka.”

"Tuambizane ukweli sisi wenyewe hatuwezi kuwalisha watu wote wa Dar es Salaam ila kwa kuanza na gari moja tulionyesha nia ya kuwasaidia wachache tuliojaliwa. Ujio wa  Sayona kutuunga mkono ni faraja kubwa, nina imani tutawafikia watu wengi," amesema Harmonize.