Jeje wa Diamond wadaiwa kufanana na wimbo wa Wizkid, Burna Boy

Wednesday February 26 2020

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mashabiki wa muziki wametoa povu kulalamikia video na midundo ya wimbo ‘Jeje’ wa msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz kuwa umefanana na nyimbo za  wasanii wa Nigeria,  Burna Boy na Wizkid.

Tuhuma kuhusu wimbo huo zimekuja saa chache baada ya kuutoa, ikiwa ni siku kadhaa tangu ashutumiwe kuiga wazo la video ya wimbo ‘Gere’ kutoka katika wimbo ‘Brisa’, ulioimbwa na  msanii wa Brazil anayejulikana kwa jina la Iza.

Wimbo huo unaoitwa ‘Jeje’ ameuachia rasmi leo Jumatano Februari 26, 2020 katika mitandao ikiwamo Youtube ambapo baadhi ya watu walioutazama wamekuwa na maoni tofauti huku wengine wakisema ameiga midundo kutoka kwa nyimbo ya msanii Burna Boy (On the Low) na Wizkid  (Joro) wote kutoka Nigeria.

Hata hivyo meneja wa Diamond, Sallam SK, amesema kuwa hiyo imetokana na mtayarishaji wa nyimbo hizo kuwa mmoja.

“Nyimbo zote zimetayarishwa na mtayarishaji mmoja aitwaye Kelpvibe, ndiyo maana katika hizo nyimbo anatajwa mwanzoni kabisa,”amesema Sallam.

Lakini mashabiki wameendelea kumpopoa mitandaoni kwa kusema kuwa ameiga na amekosa ubunifu, pia wapo waliosema wimbo huo umefanana na ule wa Joro ulioimbwa na msanii Wizkid ambaye naye anatoka nchini Nigeria na ni kati ya wasanii wa Afrika wanaofanya vizuri kimataifa.

Advertisement

Baadhi ya waliotoa maoni katika mtandao wa Youtube ni pamoja na Anthony Agbor ambaye ameandika ‘Hii ni ‘Joro’ kabisa kutoka kwa Starboy ikiwemo wazo la muziki, video,Wizkid anatakiwa kufungua kesi ya kufanyiwa uharamia wa sanaa.

Kwevo Kevo ameandika, “Ubunifu wa Diamond unapotea, anaiga sana muziki wa Nigeria.”

Mussa Msangi ameandika, “Prodyuza aliyetengeneza hii ndo katengeneza Joro ya Wiz Kid.. touch zake ndo hiz!”

Humphrey Teitei ameandika, “Naenda kupata ukichaa kwa kuwa Simba ameiga wimbo wa Burna Boy na Wizkid.”

Wakati wengine wakitoa kasoro hizo, wapo waliosifia akiwemo Joseph Muchiri aliyeandika, “Wallah Diamond wewe ni nomaaaaaaaaaaaaaa!” huku  Erico Davido akiandika, “Sijutii kuwa shabiki wa Simba.”

Dee Simba amesema, “Simba huu wimbo ni noma sana yaani ni tamu sana kuliko Joro yake Wizkid.”

Ignation JR ameandika, “Mwanamuziki wa kipekee ambaye anafanya bidii sana usiku kucha kuupeleka muziki wa Afrika Mashariki na Afrika kiujumla hatua nyingine.”

Joseph Masalu amesema, “Moja ya sifa ya kuwa msanii ni kubadilika kila wakati, Diamond ndio yupo hivyo tumpongeze kwa hilo.”

Advertisement