Kumbe Harmonize ndiye alikuwa tatizo la Rayvanny WCB

Sunday December 15 2019

 

By Luqman Maloto

JUZIKATI kuna jamaa anajifanya yeye ndiye Konde Gang wa kufa. Anajiita Konde-Mania. Basi bwana, Konde-Mania akanianzishia zogo. Alisema WCB wanawekeza nguvu nyingi kwa Rayvanny ili kuziba pengo la Harmonize.

Halafu kwa msisitizo, Konde-Mania akasema: “Waambie ndugu zako wa WCB waache kupoteza nguvu zao, Konde Nation ni taasisi ya dunia. Harmonize sio wa kushindanishwa na Rayvanny, labda wamlete Diamond mwenyewe.”

Unajua mimi watu wenye ngenga kama Konde-Mania huwa siwarembei, nikampa makavu. Nikamwambia: “Kama mnajiamini mbona mnashindwa kufanya yenu mnakaa kufuatilia ya WCB? Rayvanny anawahusu nini?”

Kumbe Konde-Mania ana vimelea vya spika za kunadi biashara soko la Karume, anaongea bila kuchoka. Halafu anarudia maneno yale. Si nimekwambia ni sampuli ya spika za Karume?

“Hushangai siku zote Rayvanny yupo na utoaji wake wa nyimbo ulikuwa unajulikana? Tunashangaa sasa hivi baada ya Harmonize kujitenga na WCB, Rayvanny anatoa nyimbo bandika bandua. Hawamuwezi na hawatuwezi sisi Konde Nation,” Konde-Mania alinijia juu.

Ubishi nauweza, nikampandia juu pia. Nikamwambia: “Hivi unataka kwa sababu Harmonize ameondoka WCB ndio Rayvanny asitoe ngoma? Kama Konde Gang mnaumia Rayvanny kufyatua madude mfululizo si na ninyi mtoe?”

Advertisement

Tatizo Konde-Mania sio wa kushindwa. Akaendelea: “Harmonize hawezi kushindana na Rayvanny. Harmonize ‘size’ yake ni Diamond. Halafu Rayvanny bonge la mzinguaji, anatuimba sisi ‘hawara hana talaka’, kwanza ajifunze kutamka, haiitwi ‘taraka’ ni ‘talaka’.”

Ndipo nikajigundua nina kazi. Sasa najenga hoja ipi? Kuhusu ubishi wa talaka au taraka? Je, Diamond na Harmonize au Rayvanny na Harmonize? Nihamie kwenye mantiki ya ‘line’ hawara hana talaka? Nikaanza kupata kizunguzungu.

Sijui Konde-Mania alijua ameshanishinda au aliona pointi zake hazijawa kamili? Nilishtuka anaendelea: “Hata akituimba hawara hana talaka bado hawatuwezi. Yule Rayvanny ni cha mtoto sana. Kama vipi na sisi tunasema inategemea na aina ya hawara. Kuna hawara lazima talaka itoke.”

Hapo sasa nikamtolea macho, akasema: “Usinitolee macho, kuna hawara lazima talaka itoke. Tena hawara ni wao ndio maana Harmonize alipoomba kuondoka WCB, wakataka stahiki za kuachwa. Harmonize ikabidi awaachie Shilingi milioni 500 za matumizi. Ile milioni 500 sio talaka?”

Hivi kama ni wewe hapo ungemwacha? Aloo nilisema naye: “Unajua wewe una akili fupi sana. Sasa Rayvanny kuimba hawara hana talaka inahusika nini na Harmonize. Ule ni wimbo wake. Ninyi Konde Gang mbona mnajishtukia sana?”

Aliniacha kwani? Akanipandishia: “Kwani wewe unajua nini? Wewe si upoupo tu? Kwanza napoteza muda wangu bure kubishana na mtu ambaye hajui muziki kabisa. Nasema hivi, hawara talaka anayo, ndio maana Harmonize alilipa Shilingi milioni 500 WCB za talaka. Naongeza Rayvanny flag la Harmonize halikuti hata atambikie.”

Nilianza kuondoka bila kumuaga. Nilishaona sina uwezo wa kubishana naye, alivyo mgomvi akaanza kunicheka, halafu akasema: “Umekosa la kutetea eeh? Ndani ya mwezi mmoja Rayvanny katoa I Love You, Naogopa na Tetema Remix, halafu kawashirikisha Patoranking, Zlatana na Diamond, nguvu yote hiyo eti kumdhibiti Harmonize.”

Nina kawaida moja, nikishampuuza mtu huwa nafanya hivyo mazima. Sikutaka kumjibu, niliondoka zangu. Ni hapo niligundua yule Konde-Mania alitaka shari na mimi. Si alianza kinizomea? “Hilooo li WCB hilooo. Linatetea hata halijui kitu. Hilooo?”

Kuna wakati nilishawishika kugeuka nipigane. Ananishambuliaje bila kosa? Nilimtazama, nikagundua inawezekana ni kesi hiyo, nimpe “hook” moja afe, niende jela kwa sababu ya ukosefu wangu wa subira. Nikampuuza. Nikaondoka. Japo aliendelea kunishambulia kwa maneno na kunizomea juu. Sikugeuka.

Nikiwa peke yangu baada ya kuachana na Konde-Mania, yale mashambulizi yalianza kurejea kichwani. Hasa idadi ya nyimbo ambazo Rayvanny amekuwa akitoa mfululizo. Alifyafua I Love You, baada ya wiki mbili akaachia Naogopa, kabla ya wiki ikafuata Tetema Remix.

Naogopa ni bonge la dude na ndani yake ndio Rayvanny analalamika “hawara hana talaka”, halafu yule juha anayejiita Konde-Mania, anadai eti huo mstari ni shambulizi kwa Harmonize. Sijui yule taahira yupoje?

Nilishaamua kumpuuza, ngoja niendelee kumpuuza. Kuna hili la idadi ya nyimbo si la kupuuza kabisa. Hii kasi ya Rayvanny ya sasa katika kutoa nyimbo mbona imekuwa na viwango vya Six G? Hatukuwahi kuona haya huko nyuma. Kwa sentimimita kadhaa za urefu, kwenye eneo hili nilikubaliana kwa mbali na Konde-Mania.

Hata hivyo, sikutaka kumkukubalia waziwazi, angejidai sana. Na vile anapenda sifa sijui ningembebea wapi? Kimyakimya nikajiuliza; kama Rayvanny angekuwa na kasi hiyo mbona angekuwa mbali sana?

Sikuacha kujiuliza; Rayvanny alikuwa anasubiri Harmonize aondoke ndio achanue makucha yake? Kwa maana hiyo kama Harmonize angejitoa WCB miaka miwili iliyopita, pengine Rayvanny wa sasa angekuwa ‘intaneshno’.

Wakati Konde-Mania yeye alisema Rayvanny anapewa ‘busta’ WCB kwa kutoa ngoma mfululizo ili aendane na kasi ya Harmonize, mimi nikawaza tofauti, Harmonize ndiye kudumaa na kukua kikazi kwa Rayvanny. Si unaona sasa Rayvanny anaachia mawe kwa fujo? Unaweza kubet kuwa Harmonize angebaki WCB, kasi ya Rayvanny ya sasa isingeonekana.

Pamoja na ukweli mimi si muumini wa utoaji ngoma kwa fujo, bandika bandua, kwani huwafanya mashabiki wasikumiss, lakini kasi mpya ya Rayvanny ni ya kupongeza. Amekuja kwa kasi nzuri. Swali ni je, hiyo kasi inahusiana na Harmonize kung’atuka WCB?

Kingine ambacho si cha kuacha ni remix ya Tetema. Ndio nini badala ya kutengeneza video mpya, wakaenda kutujazia viraka? Wamezingua kinoma. Tetema Remix ni bonge la ngoma na lilipaswa kutengenezewa kichupa kipya.

Sijui waliona video ya zamani ni kali, hivyo kuwahamasisha kurudia vipande vingi? Au uvivu wa kurekodi upya? Pengine ufinyu wa bajeti, lakini ukweli ni kwamba wamechemka balaa.

Diamond alishindwa nini kurekodi video ya kipande chake? Kulikuwa na sababu ipi ya kurudia shots za mbele ya ndege na nyingine? Sishangai kuona Tetema Remix ni mzigo mkali lakini hautoboi inavyotakiwa. Ni kwa sababu ‘pipo’ zinaona zinaoneshwa viraka, wakati walitaka mzigo mpya.

Kwa vyovyote vile, Tetema Remix inaweza kuwa ndio ngoma iliyonikata stimu mwaka 2019. Wimbo mkali, video ya viraka.


Advertisement