Kwa nini Sauti za Busara ni zaidi ya tamasha la muziki

Hali ilivyo katika Mji Mkongwe, Zanzibar ni ile ya matarajio. Baada ya mwezi Januari kuwa hauna mwamko wa kibiashara, sasa biashara zimeanza kushamiri katika kipindi hiki ambacho kwa miaka kumi iliyopita kimekuwa ni msimu wa kuwa na watalii wengi.

Mbali na muziki na burudani zinazopamba kilele cha tamasha la Sautiza Busara, kuna mengi zaidi yanayotazamiwa kuwepo katika msimu huu.

Akizungumza wiki hii, Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Yusuf Mahmoud amesema kuwa kwa miaka mingi tamasha hilo limesaidia kuitangaza Zanzibar na Tanzania kimataifa kama maeneo bora ya utalii wa kiutamaduni.

“Kabla ya kuanzishwa kwa tamasha la Sauti za Busara miaka 17 iliyopita, mwezi Februari haukuwa msimu uliovutia watalii wengi lakini hali hiyo kwa sasa imebadilika kwa kiasi kikubwa, mwezi huu ndiyo unaopokea watalii wengi wanaokuja nchini kutoka katika kila pembe ya dunia,“ alisema.

Mahudhurio ya watu wapatao 27,000 ndani ya siku nne yana athari chanya katika biashara zilizopo Zanzibar na tamasha linachangia kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 10 katika uchumi.

“Umhimu wa tamasha hili ziko wazi, karibu kila hoteli zilizopo Stone Town na sehemu nyingine za Zanzibar zinakuwa zimejaa katika wiki ya tamasha,” aliongeza.

Wanufaika ambao ni wafanyabiashara walioizunguka Mji Mkongwe wanasema tamasha hilo limekuwa msimu ambao hakuna mfanya biashara anataka kuikosa.

Hawa Mohammed ana miliki duka la vinyago karibu na Ngome Kongwe na amejiandaa kwa kuagiza bidhaa kadha akitazamia kuongezeka kwa wageni watakaokuja kwenye tamasha.

"Wageni wengi wakija hapa wanataka kuondoka na ukumbusho kutoka Zanzibar na hii ndio sehemu pekee wanaweza kununua vitu kama hivyo kwa bei nafuu," anasema Hawa.

Tamasha limefanikiwa kufungua fursa za kiuchumi zilizopo katika visiwa vya Zanzibar katika namna ambayo haikuwa rahisi kuzigundua mpaka hapa tunapozungumza.

Kulingana na Mkurugenzi wa tamasha, mamia ya vijana wanaajiriwa na wanaendelea kukuza ujuzi wao kupitia tamasha hilo kwa idara kadhaa, kutoka idara ya utawala, wasimamizi wa jukwa, na idara ya uzalishaji.

“Tamasha la Sauti za Busara linatoa fursa kwa vijana kwa kufanya mafunzo na kukuza ujuzi wao katika nyanja za usimamizi wa hafla, masoko na mafunzo ya ufundi ambayo yanasaidia kuwakwamua kimaisha.”

Tamasha pia linatoa jukwaa kwa ajili ya uhuru wa kujieleza kupitia darasa la Movers & Shakers ambapo wazalishaji wa muziki, mapromota, mawakala, wasambazaji, na wadau wengine hukaa na kukubaliana kwa pamoja kujadili mada kama vile wanawake katika muziki: vitisho, changamoto na fursa.

Tamasha la Sauti za Busara la mwaka 2020 limekuja na kauli mbiu “Paza sauti, pinga unyanyasaji wa kijinsia.”

Tamasha pia kwa miaka kadhaa limekuwa sehemu ya kuwakutanisha watu wenye hsitoria tofauti tofauti, wanaoheshimu muziki wa kiafrika unaopigwa (live) mubashara katika aina zake mbalimbali.

Sambamba na lengo la waandaaji wa tamasha la kuhamasisha kuheshimu mkusanyiko wa tamaduni mbalimbali za muziki wa Afrika, wanasema kuwa mchanganyiko na uwiano baina ya wasanii wa Kitanzania, wale wanoatoka ndani ya Afrika na wale wa mataifa mbalimbali na hadhira iliyopo ndani ya tamasha hilo, ni siri kubwa ya mafanikio.