NO AGENDA: Maisha ya Darassa ni shule ya mafanikio kimuziki

Sunday February 16 2020

 

By Luqman Maloto

NISHIKE Mkono na Sikati Tamaa ni nyimbo bora zaidi sio tu kuimbwa na Darassa, bali pia katika soko la muziki Tanzania. Uzuri wa ujumbe na mashairi yake, ubora wa mistari yenye kufikirisha na floo nzuri ya Darassa, bado nyimbo hizo hazikumpa mafanikio.

Nishike Mkono na Sikati Tamaa zimebaki kuwa nyimbo nzuri za Darassa na ziliweza kumtambulisha kama mwanamuziki mzuri, lakini hazikumpa thamani ambayo alihitaji aipate. Hazikumpa ubora aliostahili.

Ukisikiliza mashairi ya Nishike Mkono na Sikati Tamaa unapata picha kuwa Darassa alitumia akili nyingi kuandika, vilevile kutumia muda mrefu kutengeneza mitindo ya kufloo kutoka baa moja kwenda nyingine.

Nyakati ambazo wasanii wanatoa nyimbo kisha wanategemea zaidi shoo ili waweze kupata fedha, nyimbo hizo na ukubwa wake hazikuweza kumpa Darassa shoo. Kwa hiyo Darassa hakuwa msanii aliyetengeneza fedha.

Kwa mtu ambaye alikuwa anapata nafasi ya kusikiliza nyimbo za Darassa kisha akaiona hali yake, angepata hali mbili kwa wakati mmoja. Kwanza angepata hasira kuwa muziki haupo ‘fea’, pili angemsikitikia Darassa kwamba havuni alichokuwa anastahili.

Wapo watu wanaingia studio kisha wanaimbaimba mistari laini, siku hiyohiyo anakutana na mdundo kisha anaandika mashairi hapohapo studio halafu anaingiza sauti na kumaliza kazi. Wimbo ukitoka unapata promo kisha unatamba. Watu wanasema ngoma kali wakati mwanamuziki hata hajaumiza akili.

Advertisement

Nyimbo zinazoweza kuishi kama Nishike Mkono na Sikati Tamaa, zinachezwa kisha watu wanazipotezea. Mtu anaumiza kichwa muziki haumpi pesa, wenye kufanya muziki poa-poa wanang’ara. Hayo si matokeo yenye kupendeza.

Sikuwaelewa kabisa Wabongo kwenye wimbo Sikati Tamaa, yaani hata kiitikio kizuri cha Ben Pol hawakukielewa. Katika Nishike Mkono, sauti nzuri ya Winnie hawakuielewa kabisa.

MUZIKI UNA MAAJABU

Wimbo Kama Utanipenda wa Darassa aliomshirikisha Rich Mavoko ulikuwa mzuri sana na ulimfungulia njia Darassa kuliko kazi zake za nyuma. Zile kazi za hisia na zenye kuufikirisha ubongo hazikufua dafu.

Ikabidi niusikilize Kama Utanipenda kwa ukaribu, nikagundua ni kazi bora sana. Ndani yake kuna mabadiliko makubwa kutoka Darassa wa awali mpaka alipotoa ngoma hiyo. Floo tofauti na uandishi wa kivingine. Ni ngoma yenye kuchangamsha kuliko kuteka hisia.

Darassa akazidi kunipa imani kuwa amefungua njia, kama alikuwa amefunikwa na paa basi limefunguka, ni pale alipotoa ngoma Too Much. Ni wimbo mkubwa lakini wa ujumbe wa moja kwa moja, siyo wa kuufikirisha ubongo.

Ndani ya Too Much unapata ladha nzuri, mtindo na ujumbe. Alichokiimba Darassa ndani ya Too Much ndicho ambacho tunaishi nacho kila leo. Bonge la wimbo.

Too Much unatosha kuusikiliza na kukupa ujumbe huku unakuburudisha ukiwa umekaa. DJ akiucheza klabu hapati shida kupayuka ili kuwahamasisha watu kuufurahia na kuucheza, wenyewe tu wakiusikiliza wanaamka vitini. Watu wanajikuta wanacheza bila kupangilia.

Kama Utanipenda na Too Much ni nyimbo ambazo zinathibitisha kuwa Darassa ana kichwa kizuri na ni hazina endelevu kwenye muziki wa Bongo na sanaa kwa jumla.

MUZIKI HAUPO ‘FEA’

Sikati Tamaa na Nishike Mkono ni kati ya nyimbo nyingi nzuri za Darassa ambazo zilidoda. Kama Utanipenda na Too Much ni nyimbo za Darassa ambazo zilimweka pazuri kibishara.

Ukitaka kujua biashara ya muziki haipo ‘fea’, wimbo Muziki ndiyo ambao ulivunja miamba na kupasua anga la kibiashara na kumweka Darassa kwenye kilele chake.

Ukiusikiliza Muziki huoni matumizi makubwa ya akili. Hakuna ujumbe mzito ndani yake, isipokuwa ni ladha kwa asilimia 100.

Biashara ya muziki haipo ‘fea’, ukiusikiliza wimbo Muziki unauona zaidi ufundi wa maprodyuza walioutengeneza kuliko waimbaji. Mashairi ya wimbo huo yanaakisi nguvu kidogo ya kichwa iliyotumika kuandika.

Muziki ni wimbo unaoburudisha zaidi lakini unaonekana wazi kuwa haukumgharimu Darassa nguvu nyingi kuuandaa. Hata hivyo, ndiyo wimbo ambao ulimpa mafanikio ambayo alikuwa akiyastahili miaka mingi iliyopita.

Ni hapo ndipo unaona namna ambavyo game la muziki lilivyo halina adabu. Mtu unajipinda kuandaa nondo za maneno (punch-lines) pamoja na ujumbe mkubwa ili wimbo ukisikika ukupe nyota nyingi sokoni, lakini watu wanadengua. Wimbo mkubwa lakini watu wanauchukulia poa.

Siku nyingine unaamua kufanya kitu rahisi cha kuwafanya watu wacheze na kusahau shida zao, hapohapo kila kitu kinabadilika. Taifa linageuka kichaa kwa mapenzi makubwa kwa wimbo wenyewe.

Hiyo ndiyo tafsiri ya Darassa, alishafanya muziki ambao ulionesha kabisa alitumia akili yake mpaka kufikia kiwango cha mwisho katika kufikisha ujumbe aliokusudia na kuburudisha lakini mapokeo ya watu yakawa tofauti mno.

Darassa kila alipopunguza matumizi makubwa ya akili ndipo alifanya muziki ambao uliwachukua watu. Kutoka ujumbe wa kimaisha na shida za dunia mpaka Kama Utanipenda, hapo Darassa alipunguza akili aliyokuwa anatumia kabla na alipata matokeo.

Kutoka Kama Utanipenda mpaka Too Much, unaona pia Darassa alipunguza kiwango cha matumizi ya akili yake na matokeo yakawa makubwa. Kutoka Too Much mpaka Muziki, Darassa kwa mara nyingine alipunguza akili kisha matokeo yalimuweka kwenye kilele cha biashara.

Kwa mantiki hiyo, Darassa alikuwa anatumia akili ya juu zaidi kwa kutoa nyimbo za kumfikirisha binadamu na shida zake, lakini akawa anaambulia ukame mfukoni wa kifedha kwa sababu wadau wa muziki hawakuheshimu ubora wa kazi yake.

Darassa alipopunguza matumizi ya akili katika kuandaa kazi zake, matokeo yakamuweka kileleni. Mungu ampe nini tena? Muziki kama burudani na fedha, Darassa alipatia sana kupitia wimbo, Muziki.

ELEWA “IPO NJIA”

Chukua kila ambacho nimekieleza kutoka mwanzo mpaka kufikia hapa kisha pokea ujumbe muhimu ufuatao; Siku zote maishani mwako, kwenye kuhangaika kwako, katika kuvuja jasho na kutaabika mpaka kukatisha tamaa, elewa kuwa “ipo njia”.

Darassa alionesha kuwa njia yake ya kutamba kwenye soko la muziki ilikuwepo, ila ilitaka subira, kuendelea kupambana na kubadili njia za ufanyaji kazi.

Kuwika kwa Darassa kupitia “Muziki” ni ujumbe muhimu kwamba unaweza kuwa mahiri kwenye kazi unayofanya lakini usipate mafanikio ya kifedha. Hata hivyo, ukiwa na nidhamu ya kubadilika na kujaribu aina tofauti za ufanyaji kazi, utajikuta umefanikiwa.

Shida ya Darassa ni kukariri. Baada “Muziki” amekuwa akitaka kukariri na kurudia alichokifanya kwenye Muziki. Anza Hasara Roho mpaka Relax, chukua nyingine kama Leo, Tumepoteza na zote baada ya Muziki, unamuona Darassa anajaribu kugandamizia Muziki.

Darassa ni bonge la darasa. Kama alivyobadilika na kutoboa, hata sasa anabilike. Asing’ang’anize staili.


Advertisement