ANTI BETTIE: Nikimwambia mchumba wangu tuishi pamoja ananitolea nje

Nina mchumba ambaye nimeshamtolea posa, ila nataka tuishi pamoja ndiyo nimtolee mahari na kufunga naye ndoa.

Anachonishangaza, hataki kuishi pamoja nami kabla ya ndoa, anaficha nini?

Hafichi kitu chochote, wewe hadi umemtolea posa kipi hukijui kutoka kwake?

Sidhani kama kuna kitu anaficha kama nilivyosema hapo awali, kwanza namsifia kwa sababu wasichana au wanawake wengi wanaona wakiposwa wana haki ya kuhamia kwa mwanaume, hii inawafanya wengi waishie kuposwa na ndoa kuota mbawa.

Hivi jiulize wewe mwenyewe utakuwa na haja gani ya kumuoa iwapo anakufulia, anakupikia, kila ukirudi unakuta vitu vipo sawa, kama watoto anakuzalia, mnalala na kuamka pamoja?

Unaweza kumuoa, lakini kwa miaka mingi baadaye na mtakuwa mnapasha kiporo. Kwangu, huyo yuko sahihi kwa kuwa unampenda na una hamu ya kuishi naye harakisha taratibu mfunge ndoa awe wako wa halali.

Kukaa pamoja kunaweza kuondoa mapenzi yenu kwa sababu mtazoeana na mtakuwa hamna kitu kinachowabana kisheria, lakini mkifunga ndoa kila mmoja atakumbuka kiapo mlichoingia na kuheshimiana.

Anapenda boga analichukia ua lake

Nina mpenzi tunayepanga kufunga ndoa, tatizo nilizaa kabla ya kuwa naye. Nikimweleza kuwa akinioa itabidi nimchukue mtoto wangu tukaishi sote, hataki. Tena ananionya kila mara kuhusu hilo.Nifanyeje?

Huna cha kufanya zaidi ya kwenda na mwanao, hakuna mama anayesonga mbele na kumuacha mtoto wake nyuma.

Kwanza chunga sana tabia za huyo mwanaume kabla hamjaingia kwenye ndoa, uhakikishe mmelimaliza hilo tena kwa uhakika kwamba utakwenda kwake na mwanao. Ikishindikana bora ubaki na mwanao utapata mume mwingine anayejali. Huyu inaonekana hana utu na anaweza kumdhuru mwanao siku zijazo. Matukio ya baba wa aina hiyo ni mengi yanapaswa kuwa funzo kabla hujaamua kumkabidhi maisha yako.

Mtu mwenye akili timamu hawezi kumkabili mama wa mtoto na kumwambia ‘nikikuoa simtaki mtoto wako’. Mwangalie sana huyo mwanaume.

Hata kama kuna mazingira rafiki kiasi gani kwa mwanao kubaki kwao, kwenu bado anapaswa afahamu wewe kama mama ndiyo mwenye jukumu la kwanza la mtoto wako.

Kama amekupenda kwa dhati na mwanao atampenda pia.

Inawezekana anamhofia baba wa mtoto, hilo kwangu siyo sababu ya kumkataa mtoto wako. Angetumia lugha nyingine kukuelewesha, ingawa anapaswa kujua ipo siku mtoto atakuja kwenu na ataishi nanyi japo siku chache.

Wewe ndiyo wa kulimaliza hili, chekecha akilini mwako kama ni sahihi kukutenganisha na mwanao au kuishi pamoja naye, ukipata jibu lifanyie kazi.

Ukilikubali hili kirahisi katika hatua hizi za awali, niamini huko mbele ya safari litakupa shida. Usikubali mapenzi yachukue nafasi ya mtoto wako ambaye ana kila sababu ya kupata mapenzi yako, hivi akikua akakuta hadithi mwanaume unayeishi naye au uliyefunga naye ndoa alimkataa atajisikiaje. Bila shaka atakuchukia zaidi wewe mama yake kuliko baba yake wa kufikia.

Amua kwa umakini hili kabla ya kuendelea na wazo la kufunga ndoa na kipenzi chako kisichotaka damu yako kwake.