Onyesho la Mariah Carey lapigwa kalenda, kisa corona

Mwanamuziki wa Marekani, Mariah Carey ameahirisha onyesho lake katika mji wa Hawaii kuhofia maambukizi ya viruso vya corona.

Katika mji huo watu watatu wamefariki dunia baada kuugua corona.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa  Instagram,  Carey amewaomba radhi mashabiki wake kwa onyesho hilo lililokuwa lifanyike  Machi 10, 2020.

“Kwa masikitiko makubwa nachukua fursa hii kuwatangazia mashabiki zangu kuwa nimeamua kusogeza mbele shoo yangu  hadi Novemba, 2020.”

“Nilikuwa na furaha kubwa  kuja Hawaii lakini kutokana na masharti yaliyowekwa kwenye usafiri wa kimataifa kutokana na virusi vya corona, sitoweza kufanya shoo yangu tena hadi Novemba,” amsema  Carey.

Wasanii wengine walioahirisha shoo zao kutokana na kuenea kwa virusi hivyo ni DJ Khalid, kundi la muziki la Korea  (BTS), bendi ya US Day Green na mwimbaji  Avril Lavigne.

Rapa  Stormzy kutoka  Uingereza aliyekuwa afanye shoo  Malaysia, Singapore, Japan, China na Korea Kusini ameahirisha shoo hizo hadi baadaye mwaka 2020.

“Ilikuwa nikutanishe dunia katika ziara yangu ya kimuziki, lakini tishio la kusambaa kwa virusi vya corona limenilazimisha kuahirisha” ameandika mwimbaji huyo.

Uwepo wa virusi hivyo pia unatishia kuahirishwa tamasha la Glastonbury  lililokuwa lifanyike ka siku tano mwishoni mwa Juni. Tamasha linatarajiwa kuhudhuriwa na watu  200,000 .