Roma alikutana na mzimu wa Che Guevara Zimbabwe!

Monday November 18 2019

 

By LUQMAN MALOTO

ALIVAA nguo nyeupe, akatuaga akilia. Akatwambia anakwenda Zimbabwe. Ilikuwa Agosti 10, 2017. Mmh! Zimbabwe tena kunani? Ikaonekana ni tukio la kurudisha mpira kwa kipa!

Ni Roma (Rhymes Of Magic Attraction), ongeza na Mkatoliki. Wazazi wake walimwita Ibrahim. Hati yake ya kusafiria iliyomwezesha kwenda Zimbabwe ina majina; Ibrahim Mussa Mshana!

Tukamwambia “Imba Roma Imba”, akasema yeye ni baba wa familia, akiuawa nani atamlea mwanaye? Akatupa stori nyingi kuhusu mahangaiko ya familia yake, mama yake alivyovamia mpaka vyumba vya kuhifadhia maiti kumsaka.

Nimekuacha mwana? Usijali, hapa hakiharibiki kitu. Aprili 2017, Roma alitekwa na washenzi fulani (washenzi tu). Walimchukua Roma na wenzake watatu. Walikaa nao siku tatu.

Masiku hayo yalipopita, wale washenzi (watekaji), waliwatelekeza ufukweni Bahari ya Hindi. Walipotembea bila ramani, ndipo walishtukia ni Mahaba Beach, Ununio, Dar.

Kabla ya hapo nchi ilisimama kumsaka Roma na wenzake. Vituo vya polisi, hospitali, ooh! Kumbe Mama Mshana (Mama Roma), alikwenda mpaka vyumba vya kubadilishia maiti! Mwanaye alitusimulia alipotuaga anakwenda Zimbawe.

Advertisement

Ni kwa kadhia hiyo aliyoipata ya kutekwa, Roma wakati anautangazia umma kuwa anakwenda Zimbabwe, aliamua kutushushua sisi tuliomtaka afunguke kwa kutuuliza: “Kipi bora nionekane nimekufa kiharakati?”

Kimsingi safari ya Roma Zimbabwe ilikuwa na majibu kuwa janki wa Tanga alirudisha mpira kwa kipa. Aliamua kujitenga kuepusha shari ili asimwache mtoto wake bila matunzo. Kwamba angeendelea na alichokuwa anakifanya mwanaye angemkosa baba. Alihofia kuuawa!

Maisha Zimbabwe vipi? Yalionekana poa kwake. Akawa anaimba “Mwajuma Kaolewa” na musical partner wake, Stamina, au “Kijiwe Nongwa”. Wakaimba mpaka “Kiba100” ukafungiwa na Basata, lakini haukuwatikisa watekaji.

Huko Zimbabwe alipokimbilia, wajeda walifanya yao, wakamwondoa Mzee Jongwe, Robert Mugabe (RIP). Kwamba alikimbia harakati Bongo, akakuta Wazimbabwe wanakinukisha kwa harakati za Chimurenga, Bob Mugabe aling’oka miezi mitatu baada ya Roma kutimkia Zimbabwe.

Iwe alikimbilia Zimbabwe kwa hasira, woga au kususa, maisha ukimbizini yatabaki kuwa ya ukimbizi. Hakuna uhuru, kwani unaishi mazingira usiyopenda ila unajilazimisha.

Roma aliacha maswali lukuki, kweli yule Roma aliyetamba kwenye “Viva Roma” kwamba “Leta difenda, leta wajeda, leta wagambo, Roma nimejitoa sadaka”, ndio wa kufikia kuimba “Wewe Shishi mimi Snura kwa sababu Snura ana chura. Wewe Wema mimi Zari, nipo Madale naishi vema”. Dah! Zimbabwe ilimharibu mwanaharakati. Ilimbadilisha kabisa!

Yule Roma jasiri, mnyoosha mistari bila hofu. Roma aliyesema hata Ikulu anaipiga chata akiwa amevaa mlegezo kwenye ngoma “Mathematics”, siyo yule aliyekwenda ukimbizini Zimbabwe, aligeuka mpiga umbea kwenye nyimbo.

Unaelewa nini nikisema maisha ya ukimbizini huwa sio halisi? Ukiwa mkimbizi huwezi kujitanua kama wenyeji. Zaidi utamiss mazingira na watu wako. Roma alipokwenda Zimbabwe, alipoteza mazingira aliyozoea na watu waliompenda.

Ni kweli, Zimbabwe alipata watu wapya na mazingira mapya. Waliomuunga mkono alipokuwa anatuimbia umbea wa “mimi timu Diamond wewe Ali Kiba” ni wengi. Walipenda!

Sisi wapenda muziki, tuliona matokeo ya kipaji kikubwa kwamba Roma alionesha uwezo wa kufanya zaidi ya nyimbo za harakati. Nilimsifu ‘alivyofloo’ vizuri katika wimbo wa Mwajuma Kaolewa. Ila kwa wanaharakati, alizidi kuwapoteza.

TUSIANDIKIE MATE!

Huu wino umejaa! Tangu alipoaga anakwenda Zimbabwe, zaidi ya miaka miwili imepita. Roma ameona kama Chimurenga walimuweza bosi wao Mugabe, ya nini aendelee kuishi ukimbizini?

Roma amerejea, tena amerudi na kifurushi chenye hasira za kutosha, anatutambia “hakuna wa kumnyamazisha, wala kumstopisha”. Roma amerudi nyumbani na ameupiga mwingi kwenye uwanja aliouzoea.

Ngoma “Anaitwa Roma” ndio imemrejesha Roma kwenye home ground. Uwanja umefurika watu, anapiga chenga za maudhi, anashambulia, anatoa pasi na kuomba tena, anapiga mashuti makali na kufunga magoli ya mbali, mengine anapasia nyavu kiulaini, kisha anarudi kukaba.

Watu wake wanashangilia, walimmiss, wanampa welcome back ya kishindo, maana hata alipowaaga kwa wimbo wake wa farewell “Zimbabwe”, hawakumwelewa. Walijua angerudi, na walitamani kuona anarejea. Ndio maana wamempokea bila kinyongo. Tena kwa kishindo!

Ona home ground palivyo na raha, “Anaitwa Roma” ni audio tu, no video, lakini aliteremsha utawala wa Baba Lao ya Diamond Platnumz ndani ya saa 20. Kwa zaidi ya wiki, tangu ilipotoka, Baba Lao iling’ang’ania namba moja kwa ku’trend.

Baba Lao ilipoifurusha Uno ya Harmonize, iling’ang’ania. Ali Kiba alipowasha Mshumaa, alitambia wengine na kuishia namba mbili. Mshumaa wa Ali haukuweza kuinguza Baba Lao.

Roma akasema yeye ndiye mwenye vina vyenye mvuto wa kimiujiza, akawang’oa wote. Zingatia, Mshumaa, Baba Lao na Uno ni video, Roma ni audio, lakini amenyoosha YouTube na ku’trend namba moja.

Hayo ndio matunda ya kucheza home ground. Unakuta mashabiki wapo tayari. Roma hahitaji kutumia nguvu nyingi kutangaza nyimbo zake zenye sura ya harakati, kwani tayari ana mashabiki lukuki na wana njaa kali ya huduma yake.

MZIMU WA CHE

Zamani kidogo, Roma alitwambia kwenye ngoma “Mathematics” kuwa ndoto zake zilikuwa awe padri, lakini ziliyeyuka baada ya kupuliziwa moshi wa weed. Bangi. Sijui anavuta yule dogo?

Anyways, bora moshi wa bangi kuliko ukutane na mzimu wa mwanaharakati Ernesto Che Guevara. Ukikimbia harakati halafu ukakutana na mzimu wa Che, utarudi utake usitake.

Che alipenda harakati kuliko maisha yake. Mwaka 1959, baada ya kuongoza mapinduzi ya kumng’oa aliyekuwa diktekta wa Cuba, Fulgencio Batista, akishirikiana na mtu na kaka yake, Fidel na Raul Castro, alipewa bonge la cheo.

Fidel Castro baada ya kujitangaza kiongozi wa Cuba, alimteua Che kuwa Waziri wa Uchumi na Diplomasia. Hivyo Che alikuwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Mambo ya Nje kwa wakati mmoja. Ungedhani aliona maisha aliyapatia. Che alijiuzulu akaenda zake kwenye harakati.

Che alimwandikia barua Fidel, akamwambia: “Nimeshamilisha jukumu langu la mapinduzi.” Akaacha uwaziri, akaenda Kongo msituni kufanya harakati, kisha Bolivia ambako aliuawa.

Itakuwa Roma alipitiwa na mzimu wa Che ambao umemrudisha kwenye harakati, ingawa anawashtukia Wabongo akisema “wanauliza siku hizi Roma huimbi za kiharakati, huku wakisema Ununio ndio kumbukumbu iliyobaki. Mbona hamkumsapoti Mange na ninyi mtakuwa wanafiki.”

Roma ana akili, anajua watu wanapenda nyimbo zake za harakati, lakini akipata matatizo hawatakuwa naye. Watakujaza upepo utajaa, mwisho unabaki peke yako. Alipokwenda Zimbabwe alisema, hata panadol hawakumpelekea kipindi akiuguza majeraha ya kutekwa.

Advertisement