Saa 72 ngumu za Miss Tanzania katika fainali Miss World

Tuesday December 10 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia saa 72 kabla ya fainali ya urembo ya dunia (Miss World), mrembo wa Tanzania, Sylvia Bebwa amesema hana presha na fainali hiyo akisisitiza kuwa amejiandaa kufanya vizuri.

Akizungumza kutoka kwenye kambi ya Miss World jijini London, Uingereza, Sylvia alisema maandalizi yake katika kambi hiyo ni ya kiwango bora na anaamini atakuwa miongoni mwa warembo bora wa dunia Jumamosi.

Sylvia ni miongoni mwa washiriki kutoka nchi zaidi ya 100 duniani ambao wanashiriki kwenye fainali hizo za urembo.

Miss Tanzania katika fainali za dunia anafanya mradi wa namna ya kuwahudumia watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi alisema licha ya ushindani uliopo katika kambi yao, lakini anaamini atafanya vizuri.

"Nilipata uzoefu wa watu mbalimbali waliofanya vizuri kabla ya kuja kambini, nilijifunza mengi kupitia wao na nimetumia uzoefu wao kuhakikisha nafasnya vizuri," alisema.

Sylvia aliwaomba Watanzania kuendelea kumpigia kura ambazo alisema zitamuongezea nafasi ya kufanya vizuri zaidi katika fainali hizo.

Advertisement

Ili kumpigia kura mrembo huyo wa Tanzania unatembelea mtandao wa miss world kisha unachagua mobstar unajisajili kwa kufuata maelekezo na baada ya hapo una 'like' picha za mrembo huyo tayari unakuwa umempigia kura.

"Zoezi la kupiga kura litafungwa Ijumaa saa chache kabla ya fainali, upigaji kura ni hatua muhimu ambayo itaniongezea nafasi ya kushinda, niwaombe Watanzania wenzangu kunisapoti kwenye hilo kama mwakilishi wao," alisema.

Akizungumzia hali ya kambi, Sylvia alisema ni ya kiwango bora na kila mrembo ana shauku ya kufanya vizuri, ingawa amesisitiza kuwa pamoja na ushindani, lakini anaamini atafanya vizuri na kuweka historia nyingine kwa Tanzania baada ya ile ya 2005, Nancy Sumari alipotwaa taji la Miss World Afrika.

Advertisement