Singeli kung’aa kwenye tamasha la Sauti za Busara kwa mara ya kwanza

Muktasari:

  • Tamasha la Sauti za Busara kuanza kutimua vumbi Februari 7 hadi 10, 2019 na miongoni mwa wasanii watakaowasha moto wa burudani ni pamoja na wa miondoko ya singeli kutoka kundi la SKide.

Dar es Salaam. Wasanii wa miondoko ya singeli kwa mara ya kwanza watapanda kwenye jukwaa la Sauti za Busara linalotarajia kuanza kutimua vumbi Visiwani Zanzibar kuanzia Februari 7 hadi 10, 2019.

Miongoni mwa wasanii zaidi ya 400 watakaoshiriki kwenye tamasha hilo na waimbaji wa Singeli kutoka Tanzania wajulikanao kwa jina la SKide wataupeleka muziki huo kimataifa kupitia tamasha hilo.

Miongoni mwa sifa za washiriki wa tamasha hilo ni pamoja na kuimba na kucheza nyimbo mubashara, hivyo wanamuziki hao wa singeli watayakamata majukwaa matatu tofauti yatakayotumika kwenye tamasha hilo kuupaisha muziki huo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi tamasha hilo, Yusuf Mahmoud, amesema “Kwa miaka kadhaa  watazamaji wamekuwa wakitarajia vitu vya kipekee na vipya kila wakati.

“Tunaamini orodha ya wasanii ya  mwaka huu, pia ni bora kuwahi kutokea, kwani tunaendelea kuonyesha muziki halisia wa Kiafrika wenye utambulisho,” anasema Mahmoud.

Mahmoud anataja baadhi ya vikundi na wasanii watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo kuwa ni pamoja na Mokoomba (Zimbabwe), Fid Q ( Tanzania), BCUC (Afrika Kusini), Afrigo Band (Uganda),Fadhilee Itulya (Kenya), Mkubwa na Wanawe Crew (Tanzania), SKide singeli (Tanzania), Damian Soul (Tanzania),Jackie Akello (Uganda), Faith Mussa (Malawi) na  Asia Madani (Sudan/Misri).

Wengine ni  M’ToroChamou (Mayotte), HobaHoba Spirit (Morocco), Shamsi Music (Kenya), Sofaz (Reunion), Dago Roots (Reunion), Lydol (Cameroun), Stone Town Rockerz (Zanzibar), Ithrene (Algeria), Ifrikya Spirit (Algeria), Trio Kazanchis + 2 (Ethiopia/Switzerland), Rajab Suleiman  na  Kithara (Zanzibar).

Naye  Meneja wa tamasha hilo  Journey Ramadhan anasema  wageni watapata ladha tofauti kutoka kwenye midundo ya Kiafrika halisia ikiwamo ya muziki wa singeli wenye asili kutoka nchini Tanzania.

Anasema kauli mbiu ya tamasha hilo mwaka huu ni kupinga vitendo vya rushwa wakishinikiza viongozi kutoka katika kila sekta kutimiza majukumu yao ya kila siku pasi na mianya ya kuidai au kuiomba.