#WC2018: England wametinga robo fainali wakiweka rekodi hizi

Wednesday July 4 2018

 

By Fadhili Athumani

Moscow, Russia. Eric Dier alikwamisha wavuni mkwaju wa mwisho wa penalti na kuwahakikishia watoto wa Malkia nafasi katika hatua ya robo fainali, katika mchezo wa mwisho wa hatua ya mtoano uliopigwa jana usiku dhidi ya Colombia, kwenye dimba la Spartak.

England iliyoshinda kwa mikwaju 4-3 (1-1), sasa imeungana na Uruguay, Ufaransa, Ubelgiji, Brazil, Sweden, Croatia na wenyeji Russia katika raundi ya nane bora ambapo watakutana na Sweden waliofuzu kwa kuiondoa Swtzerland kwa ushindi wa goli 1-0 kwenye mchezo uliochezwa mapema jana.

Bao la sita la Harry Kane, kwenye michuano hii ambayo ni mbili zaidi ya mpinzani wake wa karibu Romelu Lukaku, lilionekana kutosha kuivusha Three Lions, ukiwa ni ushindi wa kwanza ndani ya miaka 12, katika hatua ya mtoano kwenye michuano mikubwa.

Hata hivyo, kunako dakika ya 93, kama kawaida yake, Mkombozi wa Colombia, mfia timu, kijana Yerry Mina, aliwanyanyua mashabiki wa Colombia, alipopiga kichwa safi akiwa ndani ya boksi, lililotinga nyavuni na kulazimisha mchezo uingie kipindi cha dakika za nyongeza.

Dakika 30, zilimalizika kwa sare hiyo hiyo ya 1-1, ikafuata hatua ya matuta ambapo England waliibuka washindi baada ya wapigaji wa Colombia Metues Urobe na Carlos Bacca kukosa mikwaju yao. Kwa upande wa England ni Jordan Henderson tu ndiye aliyekosa. Mwisho wa siku England wakavuka mwanangu.

Ikumbukwe kuwa, ushindi wa jana, ulimaanisha kuwa, hii ni mara ya pili, katika historia ya soka ya taifa la England, kushinda mchezo kwa mikwaju ya penalti. Mara ya kwanza ilkuwa ni mwaka 1996. Walipoifunga Spain kwenye michuano ya kombe la Euro.

Kingine ni kwamba, Harry Kane, amefanikiwa kufikisha mabao sita, katika michuano yake mitatu ya Kombe la Dunia. Hii ni dalili nzuri kwa nahodha huyo, kwani mpaka sasa ni wachezaji watatu tu ndio walikuwa wamefikisha idadi hiyo au zaidi. Sandor Kocsis wa Hungary (9), Mjerumani Gerd Muller (7) na Muargentina Guillermo Stabile (7).

 

 

Kama hiyo haitoshi, Harry Kane aanakaribia kuifikia rekodi ya Alan Shearer katika michuano ya Kombe la Dunia. Hadi sasa Shearer anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa England amewahi kuchezewa faulu nyingi zaidi. Alichezewa faulu 11, katika mchezo dhidi ya Tunisia, kwenye Kombe la Dunia 1998. Harry Kane jana alipigwa Viatu mara tisa!