#WC2018: Modric asema Russia habari nyingine

Monday July 9 2018

 

Moscow, Russia. Wakati Croatia ikitarajiwa kuvaana na England katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia, Luka Modric amesema mechi ya juzi usiku dhidi ya Russia ilikuwa ya aina yake.

Alisema England ni timu bora na mchezo wa nusu fainali utakuwa mgumu, lakini wanajindaa kwa mechi zote kwenye fainali hizo.

Modric alisema mchezo ulikuwa mgumu na ‘iliandikwa’ nyota hao kupata ushindi wa mikwaju ya penalti, baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 120.

Nahodha huyo aliyekuwa mchezaji bora wa mchezo huo, aliiongoza Croatia kufuzu nusu fainali kwa ushindi wa penalti 4-3.

Croatia itapepetana na England katika mchezo wa nusu fainali keshokutwa kwenye Uwanja wa Luzhniki. Awali, wapinzani wao walisonga mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sweden.

Modric alisema hawakutarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa Russia ambayo tangu mwanzo wa fainali hizo haikupewa nafasi ya kupenya kwenye hatua ya makundi.

“Mfumo wetu wa kucheza ulibana, hatukupenda kucheza kamari kupoteza pasi, kwa maana hiyo mpira ulikuwa katikati kipindi cha pili,”alisema nyota huyo wa Real Madrid.

Modric alidai kuwa Croatia ilitawala dakika 30 za nyongeza na walikuwa na uwezo wa ‘kumaliza’ mchezo, lakini iliandikwa lazima wafike hatua ya mikwaju ya penalti.

Hata hivyo, alidokeza kucheza dakika 120 ilikuwa kazi ngumu kwa kuwa tayari walicheza muda kama huo katika moja ya mechi zilizopita ndani ya siku sita.