#WC2018: Penalti zavunja rekodi Russia

Muktasari:

  • Makosa binafsi ya wachezaji, kuongezeka kwa umakini wa waamuzi na matumizi ya teknolojia ya video kusaidia waamuzi (VAR), vimetajwa kama sababu ya fainali za mwaka huu kuwa na idadi kubwa ya mikwaju ya penalti iliyoweka rekodi mpya.

Dar es Salaam. Wadau wa soka nchini wametaja mambo matatu yaliyochangia Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Russia, kuweka rekodi ya kuzalisha idadi kubwa ya penalti ndani ya muda wa kawaida wa mechi kuliko fainali nyingine zote zilizopita.

Makosa binafsi ya wachezaji, kuongezeka kwa umakini wa waamuzi na matumizi ya teknolojia ya video kusaidia waamuzi (VAR), vimetajwa kama sababu ya fainali za mwaka huu kuwa na idadi kubwa ya mikwaju ya penalti iliyoweka rekodi mpya.

Wakati hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia ikianza kesho, hadi sasa penalti 27 zimetolewa ndani ya dakika 90 za mchezo.

Idadi hiyo imechangia fainali za mwaka huu kuvunja rekodi iliyowekwa kwenye fainali za mwaka 2002 zilizofanyika Korea na Japan ambako jumla ya penalti 18 zilitolewa.

Katika jumla ya penalti 27 zilizopatika kwenye Kombe la Dunia, penalti 20 zimetikisa nyavu za timu pinzani na saba ziliota mbawa.

Tangu fainali za mwaka 2002 zilipoweka rekodi ya kuzalisha idadi kubwa ya penalti za muda wa kawaida wa mchezo, awamu zote zilizofuata zilikabiliwa na uhaba wa penalti.

Hata hivyo, mambo yamegeuka kwenye fainali za mwaka huu ambapo kumepatikana penalti tisa zaidi ya zilizotolewa wakati wa fainali za Korea na Japan.

Penalti hizo zilizotolewa mwaka 2002, zilizaa mabao 13 baada ya wapigaji kutumbukiza mpira wavuni huku penalti tano zikiota mbawa.

Baada ya fainali za mwaka 2002, penalti 17 zilitolewa kwenye fainali zilizofanyika Ujerumani 2006 ambapo kati ya hizo, 13 zilifungwa huku nne zikikoswa na katika fainali zilizofuata 2010 nchini Afrika Kusini, penalti 15 zilipatikana, zilifungwa tisa na kukoswa sita.

Uhaba wa penalti uliendelea kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Brazil mwaka 2014, ambapo zilipatikana 13, 12 zilifungwa na moja ilikoswa.

Mkufunzi wa kimataifa wa waamuzi wa soka anayetambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Leslie Liunda alisema penalti hizo hazijatolewa kwa bahati mbaya.

“Kwanza tunapaswa kujiuliza kwa nini penalti zinatolewa? Penalti hazitolewi kwa sababu refa amejisikia kutoa penalti, bali zinatokana na makosa ambayo wachezaji wamekuwa wakifanya eneo la hatari. Hivyo inawezekana kabisa kwamba umakini wa wachezaji umepungua na wanafanya makosa yanayosababisha waadhibiwe,” alisema Liunda.

Pia alisema Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kupitia kamati ya waamuzi, limekuwa likifanya tathmini ya mara kwa mara kuhusu uchezeshaji wa waamuzi na tayari kuna maboresho yamefanywa ili kuona vyema tukio kwa ufasaha.

“Teknolojia ya video ina mchango mkubwa kwa sababu inamsaidia mwamuzi kuona kwa usahihi tukio ambalo hana uhakika nalo. Siku zote sisi tunaotazama kwenye luninga tunakuwa na nafasi kubwa ya kujiridhisha juu ya uhalali wa tukio.

Hii ni tofauti na mwamuzi ambaye anatakiwa afanye uamuzi wa haraka kuendana na kasi ya mchezo. Uwepo wa teknolojia unampa msaada wa kujiridhisha iwapo kunatokea tukio analohisi hajalitazama vizuri mfano hizo penalti,” alisema Liunda.

Kocha wa Azam Hans van der Pluijm, licha ya kukubali kuwa teknolojia ya video imechangia kuongezeka kwa penalti, alikubaliana na hoja ya kuongezeka kwa umakini wa waamuzi.

“Ukitazama penalti zote zilizotolewa hadi sasa kwenye Kombe la Dunia, utakubaliana na mimi hakuna hata moja ambayo ni upendeleo.

Wachezaji wamekuwa wakifanya makosa na waamuzi wamekuwa wakitoa penalti kama adhabu sahihi hivyo kimsingi, niwapongeze marefa wamefanya kazi kubwa na nzuri kwenye fainali hizi,” alisema Pluijm.