HOJA BINAFSI : Saikolojia ya kujiamini ilivyoipa Leicester City ubingwa ligi ya Uingereza

Sunday May 8 2016Freddy Macha

Freddy Macha 

Kila mpenzi wa soko Ulaya ameshangazwa namna timu ndogo ya Leicester City ilivyonyakua kombe la Ligi Kuu ya Uingereza mwaka huu. Matarajio yalikuwa Chelsea, Arsenal, Manchester United, Manchester City au Liverpool.

Yanatuhusu nini tusioishi Ulaya?

Kuna sababu inayotufanya Waafrika wengi tufuatilie mashindano ya soka Ulaya.

Mosi, wachezaji wa Kiafrika ni washiriki. Watoto na vijana wanaouatilia mechi hujenga ndoto siku moja watakuwa maarufu na matajiri kama Yaya Toure, Didier Drogba, Samuel Eto’o au Riyad Mahrez – nyota chipukizi wa Leicester City.

Riyad Mahrez (mshambuliaji wa timu ya taifa ya Algeria) karibuni alitwaa tuzo la mchezaji bora kijana mwaka 2016, Uingereza. Hiyo ni mbali na kuchangia mafanikio na jahazi la Leicester City Football Club (LCFC).

Unapofika Uingereza, huusikii sana mji wa Leicester. Ni kama kutajiwa Singida ama Sumbawanga badala ya Tanga, Arusha na Mwanza.

Advertisement

Ukiwa Uingereza utaimbiwa Manchester, Birmingham, Liverpool; siyo Leicester. Tangu niishi hapa, nimewahi kufika Leicester mara moja kufanya maonyesho na kikundi cha tamthiliya. Ni mji uliojazana Wahindi, Wapakistani na wageni. Kwa maana hiyo hutegemei wawepo wachezaji wazuri wa soka.

Wahindi na Wapakistani ni wapenzi zaidi wa mchezo wa “cricket”- hivyo kwa kuanzia ni maajabu kusikia mji huu mdogo umeiteka ligi ya Uingereza ya 2015-2016.

Ukiacha mji -sasa tuje kwenye timu.

Kihistoria, LCFC, haijawahi kufikia hata klabu kumi bora za ligi ya England.

Ilianzishwa mwaka 1884 na mara ya mwisho kushinda -au kufikia kiwango cha juu- ilikuwa 1929.

Kila timu ya mpira huwa na jina la utani. Arsenal huitwa “wanabunduki” (Gunners), mathalan. Jina la Leicester ni mbweha au mbwa mwitu.

Rangi zao ni samawati na nyeupe (kama Chelsea). Kuitwa “mbweha” sina hakika ni balaa au masihara.

La tatu ni kocha

Licha ya ukocha mzuri Claudio Ranieri alifukuzwa kila alipokwenda. Aliwahi kushinda vikombe vya maana kwao Italia na “Copa El Rey” - Hispania.

Baadaye akaajiriwa na Chelsea hadi alipotimuliwa na Roman Abramovich, 2004. Hakuthaminiwa. (Wapo mahodari wengi duniani ambao hudharauliwa....)

Imeelezwa kuwa licha ya kufukuzwa na Abramovich, wachezaji wengi aliowanunua au kuwajenga walikuja kuwa kiini cha ngome ya wana- Chelsea tunayoijua leo. Claude Makelele, Didier Drogba na John Terry, nk.

Jose Mourinho alipoingia mwaka 2004 na kuanza kutangaza usultani, alikuta Ranieri alichoanza kukijenga akakiendeleza na kukikamilisha.

Baada ya kuzunguka zunguka, Ranieri aliishia kuwa kocha wa timu ya taifa Ugiriki. Huko nako alitimuliwa hadi alipoajiriwa na Leicester City mwaka jana. Leicester isiyojulikana wala kumbabaisha mpenzi yeyote.

Mbweha, fisi au Mbwa mwitu?

Kati ya wachezaji maarufu waliowahi kuichezea LCFC ni golikipa maarufu wa zamani wa Taifa la Uingereza iliyoshinda Kombe la Dunia la 1966, Gordon Banks. Banks alichukua nafasi ya kipa wa pili kwa ustadi ulimwenguni kwa karne ya 20.

Wa kwanza ni Lev Yashin wa Urusi ; wa tatu Dino Zoff wa Italia.

Ongezea kuwa mkurugenzi mkuu wa LCFC ni mwanamke, Susan Whelan....

Upo hapo?

Watangazaji wa TV la Sky na wanahabari mbalimbali nchini wote walimsanifu sana Claudio Ranieri alipoingia mwaka jana kutoka Ugiriki.

Kidogo kidogo timu ikaanza kumchapa kila mtu vigingi. Hadi kufikia Krismasi mwaka jana (kidesturi, Waingereza huanza kunusa mnofu wa nani atachukua taji mwezi Mei)- LCFC ilishazichapa timu kubwa kubwa kama Manchester City (na utajiri wake)...kupitia nguvu za wachezaji wake wadogo wasiojulikana; wengi wenyeji.

Akina Danny Drinkwater na Jamie Vantry...sasa hivi wamesajiliwa ndani ya timu ya taifa.

Kihistoria mara chache hutokea maajabu kama haya.

Kipindi cha ligi ya 2003 na 2004- Arsenal ilishinda taji bila kufungwa na timu yoyote na hatimaye kukatiwa jina la “Invicibles” yaani kitu kisichoonekana au kushindikana.

Tathimini iliyojikusanya kuhusu LCFC ya 2016- siyo tu fundisho kwa wapenzi wa soka bali wengine tusiotegemea kufanya la maana au kufanikiwa joto la jaha maishani.

Mosi ni imani

Kocha Claudio Ranieri alipofika Leicester aliwahimiza wachezaji kujiamini.

Saikolojia ya kuweka imani kichwani inakwenda na shairi la gwiji Shaaban Robert- “Kila Mtu”:

“Mambo makubwa kuweza, kuyatenda kila mtu. Moyoni mwangu nawaza, kuwa si rahisi katu, lakini mambo madogo, mtu yeyote huweza kwa njia bora si ndogo, kujaribu kufanyiza.”

Ukidhamiria jambo, ukafanya kwa nidhamu na moyo utaliweza, ndiyo nguzo kuu.

Hapo ndipo ulipo mbuyu, bahari, msufi na ghorofa ishirini.

Kama kocha, Ranieri amesifiwa kwa kuwapa wachezaji motisha na kuwatoa hisia za woga.

Hili kwangu linanikumbusha enzi zile kocha Marcio Maximo alipoiinua Taifa Stars kuanzia 2006 hadi 2010. Alitupa motisha nzuri wa kujiamini....Wengi tukaanza kuvaa jezi za Tanzania. Tukaamini kuwa na sisi kumbeeee!

Jambo la tatu lililoifanikisha Leicester City ni kutumia ulicho nacho kutimiza malengo. Timu kubwa za Chelsea, Arsenal na Manchester huwa na wachezaji wanaonunuliwa kwa mabilioni na mishahara ya mamilioni ....Nahodha wa Uingereza na mshambulizi maarufu wa Manchester United, Wayne Rooney kwa mfano hulipwa Pauni 300,000 kwa juma. Hizi ni kama Sh953 milioni. Linganisha hizo na mshahara wa mchezaji Jamie Vardy- wa Leicester City- yaani Pauni 45,000 kwa juma (Sh143 milioni). Ni nyingi kwetu sisi wengine ndiyo, ila ukilinganisha mishahara ya hawa wanasoka wa kulipwa, kuna tofauti ya chura na nyoka, msumeno na kibiriti.

Wastani huo umezagaa katika wachezaji wa klabu kubwa na ndogo duniani.

Ikawaje Rooney asiiwezeshe Manchester United kushinda ilhali Vardy na wenzake wamecheza kiume?

Kifupi ni mseto huo wa imani ya ndani ya mtu, uongozi mzuri, kutumia vipaji na kile ulichonacho mkononi bila kusubiri fedha nyingi au malaika wa mbingu kukuondoa matopeni.

Kukuondoa katika kinamasi na kukupandisha juu ya mti wa mafanikio.

Matokeo sasa utalii umejengwa, mishahara imepanda, biashara imepamba moto Leicester na Ranieri anaitwa shujaa.

Tovuti : www.freddymacha.com