MAONI: TFF isibweteke mafanikio ya Kili Queens

Monday November 25 2019

 

Timu ya Taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens leo inacheza mchezo wa fainali ya Kombe la Cecafa dhidi ya Kenya kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Kilimanjaro Queens ilifuzu fainali baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali kwa kuifunga Uganda bao 1-0 na Kenya iliichapa Burundi mabao 5-0.

Queens inawania ubingwa huo kwa mara ya tatu katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Timu hiyo imeonyesha kiwango bora katika mashindano ya mwaka huu ambayo yameshirikisha timu nane, ambazo ni Zanzibar, Sudan Kusini, Burundi, Uganda, Kenya, Djibout na Ethiopia na wenyeji Kilimanjaro Queens.

Kilimanjaro Queens imecheza ikiwa na uzoefu baada ya kutwaa kombe hilo mara mbili mfululizo mwaka 2016 nchini Uganda na 2018 yalipofanyika Burundi.

Mashindano ya mwaka huu yamekuwa na mafanikio kutokana nchi nyingi kushiriki na hivyo kuweka msisimko.

Advertisement

Mashindano ya mwaka huu yameboreshwa na viwango vya wachezaji wa timu zilizoshiriki licha ya baadhi kama Zanzibar na Djibout kukutana na vipigo vikubwa katika mechi zao.

Lakini mafanikio hayo ya Kilimanjaro hadi kufika fainali hayawezi kuendelea kama hatuna mikakati ya dhati ya kujenga soka la wanawake vinginevyo mwakani mambo yanaweza kuwa mabaya kwa timu hiyo.

Ni wazi kuwa wachezaji waliopo sasa Kilimanjaro Queens ni matunda ya muda mrefu ya programu za vijana ambazo zilitiwa nguvu na kampuni kama Coca Cola na Airtel na hivyo kuzalisha wachezaji ambao wanang’ara sasa.

Wapo wengine waliotokana na programu za vyama vya wilaya kama Kinondoni, ambayo imekuwa na timu imara za wanawake zilizokuwa zinatoa wachezaji wengi katika timu ya taifa na pia tunaweza kusema ndiyo wilaya chimbuko la soka ya wanawake.

Ni vizuri basi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuangalia namna gani itaweza kujenga misingi imara ya maendeleo ya soka ya wanawake kwa kuwa na programu bora zitakazosaidiwa na mashindano bora.

Hivi sasa kuna Ligi Kuu ya Wanawake, lakini si imara kutokana na ukweli kuwa uendeshaji wake unaathiriwa na uwezo wa kifedha wa timu zinazoshiriki.

Mara kadhaa mechi za ligi hii husimama na wakati mwingine kusogezwa mbele kutokana na timu ama kukwama njiani au matatizo mengine ya kifedha.

Haya yote hayawezi kuzalisha timu imara ya Taifa kama ligi haitakuwa imara

Hii ndiyo ligi ambayo tunatarajia kuwa itatoa wachezaji watakaokuwa wanaitwa timu za taifa, kuanzia za vijana, za pande mbili za Muungano na ile ya taifa. Hivyo isipokuwa bora, kiwango cha sasa cha timu za Taifa kitaporomoka na hivyo kupoteza uwezo wa kuteua timu imara.

Ni vizuri basi kwa TFF kuandaa mkakati wa kuwa na ligi imara ya wanawake, lakini pia kuendeleza programu za vijana ili kuandaa kizazi kijacho cha wachezaji watakaounda timu imara za Taifa.

TFF haitakiwi ibweteke na mafanikio ya Kilimanjaro Queens au hata Twiga Stars, badala yake inatakiwa ijikite katika kuandaa mikakati ya kuzifanya timu hizo ziendelee kung’ara na pia kizazi kipya kiendelee kuzalishwa ili kusiwe na pengo kati ya timu iliyopo sasa na ile itakayokuja baadaye.

Ni imani yetu kuwa TFF itaandaa programu ya kuhakikisha soka ya wanawake inakua na Tanzania inaendelea kung’ara katika soka hilo.