MAONI: Vikao kati ya Serikali na wafanyabiashara vizae matunda kwa manufaa ya pande zote

Sunday June 9 2019

 

Kwa mara nyingine, jana Rais John Magufuli alikutana na wafanyabiashara Ikulu jijini Dar es Salaam na kila upande ulieleza mawazo na malalamiko yake ili kuboresha mazingira ya biashara na kuwezesha kila mmoja kunufaika.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli alieleza juhudi ambazo Serikali inafanya kuboresha sekta ya biashara na mambo ambayo baadhi ya wafanyabiashara hufanya katika kukwamisha juhudi hizo, ukiwamo udanganyifu na ukwepaji kodi.

Rais Magufuli asema baadhi ya wafanyabiashara hutoa rushwa na wengine kufanya udalali na kujihusisha na uhalifu, mambo ambayo tunaamini yataendelea kufanyiwa kazi kwa kuwa yamekwishafahamika.

Vilevile, kikao hicho kilitoa fursa kwa baadhi ya wafanyabiashara kuzungumza kwa niaba ya wenzao kuhusu kero wanazokabiliana nazo katika shughuli zao.

Kwanza, ifahamike kwamba pande zote, wafanyabiashara na Serikali, zinahitajiana katika kutekeleza majumu yake.

Wakati Serikali inawategemea wafanyabiashara ili walipe kodi, ushuru na tozo mbalimbali ili ipate fedha za kutekeleza majumu yake na kutoa huduma za jamii, wafanyabiashara wanaitegemea Serikali katika kuweka mazingira mazuri, sera na sheria rafiki za kuwezesha biashara kufanyika na faida kupatikana.

Advertisement

Mkutano wa jana haukuwa wa kwanza kwa wafanyabiashara kukutana na Rais na kutoa dukuduku zao. Tofauti pekee ni aina ya wafanyabiashara walioalikwa na hasa kwa kuwa wametoka wilayani.

Mbali na hayo, tulitarajia kusikia malalamiko mapya, tofauti na yale ya awali kutoka kwa wafanyabiashara, lakini mengi yamekuwa yaleyale ambayo yalikwishaelezwa na Serikali kuahidi kuyafanyia kazi.

Mathalan, yamekuwapo malalamiko muda mrefu ya wafanyabiashara kubambikiwa kodi kubwa, ukaguzi na tozo za mamlaka zaidi ya moja na kero katika ufuatiliaji wa vibali na leseni katika taasisi tofauti.

Haya yote yamekwishaelezwa na wafanyabiashara zaidi ya mara moja na hata kukemewa na viongozi mara kadhaa.

Hata Rais amesema kuna utitiri wa tozo na taasisi za uthibiti kwa wafanyabiashara, akizitaja TBS (Shirika la Viwango Tanzania), Osha (Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi), TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania), Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Wakala wa Vipimo, Nemc, Tume ya Ushindani, Ewura, Sumatra na nyingine nyingi na zimekuwa zikihusika katika kutoza tozo na ada mbalimbali.

Pamoja na kwamba tusingetarajia kusikia tena kero hizo tukiamini zingekuwa zimefanyiwa kazi, tumefarijika kusikia hata Rais anazikumbuka na hivyo tunashawishika kuwa bado zinafanyiwa kazi na huenda katika mikutano ijayo zitakuwa historia.

Aidha, tunapenda kupongeza utaratibu huu wa kukutanisha pande hizo mbili kwa kuwa ni muhimu na unastahili kuenziwa. Lakini la muhimu zaidi ni kuyafanyia kazi yake yote yanayopendekezwa ili yasijirudie.

Ni vyema sasa malalamiko ya mara kwa mara yanayotolewa na wadau wa sekta hii yakasikilizwa na kutengenezewa miongozo ya utekelezaji ili kupata matokeo chanya na endelevu. Ukitekelezwa kwa ufanisi, mpango huu utachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na kimataifa.