TRA, polisi ‘wanusa jipu’ StarTimes, TBC
Muktasari:
Polisi na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanachunguza mzigo ulioingizwa nchini na kampuni ya StarTimes na kuhifadhiwa kwenye ofisi zake zilizo ndani ya uzio wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Mikocheni, Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Polisi na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanachunguza mzigo ulioingizwa nchini na kampuni ya StarTimes na kuhifadhiwa kwenye ofisi zake zilizo ndani ya uzio wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Mikocheni, Dar es Salaam.
Polisi pia inachunguza kama bidhaa zinazoingizwa na kampuni hiyo ni zile zinazotumika kwenye biashara ya ving’amuzi au kwa ajili ya shughuli nyingine, kwa mujibu wa ofisa mawasiliano wa TRA.
StarTimes ni kampuni ya China inayofanya biashara ya kuuza ving’amuzi kwa ajili ya vituo mbalimbali vya televisheni, hasa vya TBC.
Habari ambazo gazeti hili imezipata kutoka vyanzo mbalimbali, zinaeleza kuwa mzigo huo unaosadikiwa pia kuwa na simu za mkononi na vifaa vya pikipiki, uliingizwa juzi na kuhifadhiwa kwenye ofisi za StarTimes.
Habari hizo zinasema kuwa baada ya TRA kuutilia shaka mzigo huo, ilituma maofisa wake ambao walikesha usiku wa kuamkia jana kuufanyia upekuzi ili kujua kama unalingana na bidhaa zilizoko kwenye nyaraka walizotumia kuuingiza nchini.
Gazeti hili lilifika ofisi za kampuni hiyo jana saa 3.30 asubuhi kupata ufafanuzi juu ya taarifa hizo, lakini hakuna aliyekuwa tayari kuzungumza lolote, kwa madai kuwa mmoja wa waandishi hao wa habari alipiga picha jengo la kampuni hiyo bila ya ruhusa.
Mmoja wa walinzi wa kampuni hiyo, alikanusha taarifa za kukamatwa kwa mizigo ya kampuni hiyo, akisema “hakuna kontena wala mzigo ulioingizwa hapa, na kama kontena zingekuwepo si mngeziona”.
Juhudi za kuzungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya StarTimes, Clement Mshana ziligonga mwamba baada ya askari aliyejitambulisha kwa jina la Isack Mwakyembe kusema ameagizwa na viongozi wa juu kutoruhusu mwandishi wa habari kutoka chombo chochote zaidi ya TBC kuingia.
“Nimepewa maagizo asubuhi ya leo kwamba humu ndani asiingie mwandishi na mimi nafuata utaratibu huo,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema kulikuwa na utata katika upangaji wa mizigo wa simu za mkononi zilizoletwa na Startimes.
“Watu wetu wako hapo StarTimes kuhakiki na kujiridhisha juu ya taarifa hizo. Tutawajulisha baadaye.” Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema apigiwe simu baada ya saa mbili kwa kuwa alikuwa kwenye kikao. Hata hivyo, alipotafutwa baadaye, hakupatikana.