VIDEO-Bunge laomboleza kifo cha Bilago, wabunge waangua vilio

Wabunge wakiengua vilio baada ya Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kutangaza bungeni taarifa ya kifo cha Mbunge wa Buyungu, Mwalimu Kasuku Bilago jijini Dodoma leo. Mawaziri na wabunge wameanza kutia saini kitabu cha maombolezo ya mbunge huyo aliyefariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Dk Ackson ametumia kanuni ya 33 (2) kuliahirisha Bunge hadi kesho.

 Vilio na simanzi vilitawala katika ukumbi wa Bunge kutokana na kifo cha Mbunge wa Buyungu (Chadema) Kasuku Bilago aliyefariki dunia Jumamosi Mei 26.

Wakati huo huo, leo Mei 28, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ametumia kanuni ya 33 (2) kuliahirisha Bunge hadi kesho huku akieleza namna msiba huo ulivyowagusa wabunge.

“Waheshimiwa wabunge, Spika wa Bunge mheshimiwa Job Ndugai  anasikitika kuwatangazia kifo cha mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago kilichotokea juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwa mujibu wa kanuni zetu, leo shughuli za Bunge hazita endelea na badala yake tutakuwa na maombolezo,” amesema Naibu Spika.

Hali ya majonzi ilidhihirika mapema bungeni kwa wabunge walio wengi kuvalia mavazi ya rangi nyeusi.

Kabla ya kuingia bungeni wabunge walikaa vikundi vikundi wakijadiliana kuhusu msiba huo.

Wakati Naibu Spika Ackson akitoa taarifa za msiba na kuahirisha Bunge, wabunge Julius Kalanga (Monduli), Suzan Kiwanga (Mlimba), Halima Mdee (Kawe) na Dk Semesi Sware (Viti Maalum ) wote wa Chadema walikuwa wakilia.

Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya (Chadema) alishindwa kabisa kujizuia na wabunge walilazimika kumpa usaidizi.

Dk Tulia amesema Bilago alihamishiwa Muhimbili Mei 22 mwaka huu, akitokea hospitali ya DCMC Jijini Dodoma alikokuwa akipata matibabu.

Amesema marehemu ataagwa bungeni kesho (Mei 29) saa sita mchana na baada ya hapo atasafirishwa kwenda Kakonko ambako Spika Ndugai na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai,  watashiriki mazishi hayo.

Pamoja na wawakilishi hao, wabunge  wote wa Mkoa wa Kigoma  wamepewa nafasi ya kushiriki katika mazishi yatakayofanyika Kijiji cha Kasuka Wilaya ya Kakonko keshokutwa.