Miasha jela kwa kumlawiti mtoto wa miaka 10

Muktasari:
- Deus Joseph anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 154(1) na (2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Geita. Mahakama ya Wilaya ya Geita, imemuhukumu kifungo cha maisha Deus Joseph baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka 10.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Devotha Kassebele baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na pande zote mbili akiwemo shahidi XYZ ambaye ni muathirika wa tukio hilo.
Deus Joseph anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 154(1) na (2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Njiriku Mabula ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Aprili 22, 2024 huko katika kijiji cha Saragurwa Wilaya na Mkoa wa Geita.
Shahidi wa kwanza ambaye ndiye mwathirika wa tukio hilo aliyepewa jina la XYZ, ameieleza Mahakama kuwa siku ya tukio akiwa shambani akilinda ndege wasiingie kwenye shamba la mpunga mshtakiwa Joseph akiwa shamba la jirani alimuita.
Amedai kwenye shamba alilokuwa mshtakiwa, kulikuwa na miwa na mshtakiwa huyo alimuita ili akampe miwa na alipofika alimuuliza kama ameoga kisha akamkamata na kumuinamisha na kumlawiti.
“Aliniinamisha akanifunga mdomo sikuweza kupiga kelele na baada ya kumaliza aliniachia nikaenda nyumbani kumwambia mama,” amesema shahidi XYZ.
Akijitetea mahakamani hapo Mshtakiwa huyo amedai Aprili 23, 2024 akilinda mpunga shambani walifika viongozi wa kijiji cha Sanza na kumkamata lakini hawakumueleza sababu.
Amedai baada ya kufika kwenye ofisi ya kijiji alielezwa anashtakiwa kwa kosa la ulawiti.
Baada ya Mahakama kumtia hatiani Wakili Mabula aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Mshtakiwa aliiomba Mahakama kumuachia huru kwa kuwa hajatenda kosa hilo. Kufuatia maombi hayo, hakimu Kassebele alimuhukumu kifungo cha maisha.