Diamond, naibu waziri ni vuta nikuvute

Dar es Salaam. Unaweza kusema hali si shwari kati ya msanii Nassib Abdul ‘Diamond’ na Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza kutokana na wawili hao kujibizana kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Mvutano huo ulianza juzi baada ya Diamond kuhojiwa na kituo cha Redio Times ya jijini Dar es Salaam akimtuhumu naibu waziri huyo kufungia nyimbo za wasanii zikiwamo zake mbili za ‘Hallelujah’ na ‘Wakawaka’ bila kuzingatia hasara na usumbufu wanaoupata wakati wa kuziandaa.

Alisema wasanii nchini hutumia fedha na muda mwingi kuandaa nyimbo hizo ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wasanii wa nje ya nchi.

Baada ya Diamond kueleza hayo, jana Shonza alimjibu katika mahojiano aliyofanya na Mwananchi, “Nimemsikia lakini siwezi kumjibu kwa sababu zipo taratibu za kufuata kama anaona hajatendewa haki.”

Alisema kama yupo anayeona hakutendewa haki milango ipo wazi kwake kuandika barua ya malalamiko.

Hata hivyo, alisema wasanii wanapaswa kuelewa kuwa hakuna aliye juu ya sheria hata kama ni msanii mkubwa namna gani.

“Aliyewafungia wasanii sio Shonza, bali ni mamlaka na kama mlivyoona safari hii hadi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeingilia kati suala hilo, sasa mtu anaporusha tuhuma kumlaumu Shonza atakuwa hanitendei haki,” alisema.

“Isitoshe ofisi zetu zipo wazi anayeona ameonewa afuate taratibu katika kudai haki yake na sio kulalamikia pembeni.”

Baada ya majibu hayo ya Shonza kuzua mjadala katika mitandao ya kijamii. Jana mchana, Diamond alimjibu akisema hata naibu waziri huyo alipaswa kuwaandikia barua wasanii kuhusu kuwafungia nyimbo zao.

“Suala la barua unalijua leo baada ya kukosa point (hoja) sahihi? Ungekuwa unajua kama taratibu sahihi ni kuandika barua, mbona hukuwatumia pia wasanii barua za kuwa unafungia kazi zao,” alihoji.

“Kwa kuwa uliyapeleka kwenye social media (mitandao ya kijamii) na redio, nami nikakupelekea huko ili uienjoy (ufurahie) zaidi.”

Kilio cha Diamond

Malalamiko ya mwanamuziki huyo yalianza wiki iliyopita akiwa nchini Kenya wakati wa uzinduzi wa albamu yake ya A Boy From Tandale akisema mamlaka ziangalie kusudi la mwanamuziki anapoandaa wimbo wake.

Akihojiwa na Kituo cha Redio cha Classic FM nchini humo alisema: “Nyimbo kama Wakawaka na Hallelujah nilifikiria kufanya kitu ili soko lingine watusikilize, Serikali lazima ielewe. Kinachouma zaidi zinaweza zikafungiwa nyimbo zetu zikachezwa za kina Nick Minaj.”

Alisema chombo kilichopewa dhamana ya kuwasimamia wasanii hakiangalii kitawasaidia vipi, bali kitawakanya vipi.

Alidai kuwa viongozi hawafanyi utafiti kabla ya kutoa uamuzi isipokuwa wanaangalia kuonekana wanafanya kazi ili wasitumbuliwe.

Alimmwagia sifa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuwa amekuwa msaada kwa wasanii kwa kufanya utafiti kabla ya kutoa uamuzi.

“Naibu waziri amenizidi elimu, umri, mamlaka na vitu vingi lakini kwenye elimu ya sanaa nimemzidi hivyo alipaswa kunisikiliza kabla ya kufungia nyimbo,” alisema.

Alisema ni muhimu kwa viongozi kuwa na ushirikiano na wasanii kwa sababu mafanikio yao yanalinufaisha Taifa kwa ujumla.

Pia, alionyesha kushangazwa na kufungiwa kwa nyimbo zilizotoka miaka ya nyuma, akisema haina tija kwani haziuzwi wala kusikilizwa tena.

Kabla ya mahojiano nchini Kenya, uongozi wa lebo ya WCB ambavyo Diamond anaiongoza, ulitoa tamko ukisema hauoni ubaya wa nyimbo hizo kwani kabla ya kutolewa huwa zinapitiwa na mlezi wao ambaye ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Februari 28, TCRA iliandika barua kwa vituo vya redio na televisheni ikiviagiza visitishe kucheza nyimbo 15 za wasanii kadhaa kutokana na kuwa na maudhui ambayo yanaenda kinyume na maadili na kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) 2005.

Nyimbo zilizofungiwa ni Hallelujah na Wakawaka (Diamond), Kibamia(Roma Mkatoliki), Pale Kati Patamu, Maku (Makuzi) na Mikono Juu (Ney wa Mitego), Hainaga Ushemeji (Manifongo) na I am Sorry JK (Nikki Mbishi).

Nyingine ni Chura na Nimevurugwa (zote za Snura), Tema Mate Tumchape (Madee), Uzuri Wako (Jux), Nampa Papa (Gigy Money), Nampaga (Baranaba) na Bongo Bahati Mbaya wa Young D.