Magufuli: Muda wangu ukifika nitaondoka tarehe hiyohiyo

Rais  John  Magufuli akiwasalimia wanachi wa Naliendele mkoani Mtwara wakati akielekea kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Barabara ya Mtwara-Newala-Masasi yenye urefu wa  Km 210 na sehemu ya Mtwara-Mnivata km 50. Picha na Ikulu

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema muda wake wa uongozi ukiisha ataondoka madarakani tarehe hiyohiyo kwa kuwa yeye sio rais wa maisha.
“Mimi sio rais wa maisha ni rais wa muda, nataka niwahakikishie muda ukimalizika nitaondoka tarehe hiyohiyo ila kabla sijaondoka, maendeleo myapate kweli ili mwingine atakayekuja aje ayaharibu mwenyewe na itakuwa dhambi yake kwa Mwenyezi Mungu,” alisema jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Newala akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Mtwara.

“Kwa hiyo nitasimamia (nchi) kwa uadilifu mkubwa. Mafisadi wote nitalala nao mbele kwa sababu kutumbua ndio nimeanza, ukila hela ya serikali hata kama una cheo gani utaondoka tu.” Alisema katika kipindi chake cha uongozi maendeleo yameanza kupatikana ikiwamo ununuzi wa ndege, elimu bila malipo, umeme maji na mambo mengine.

“Kwa hiyo mmenichagua nisimamie, usimamizi ni kazi kubwa ndugu zangu, naomba tushikamane. Ninataka Tanzania iwe ya viwanda,” alisisitiza.

Aliwataka viongozi wa Mkoa wa Mtwara kusimamia viwanda vinavyoanzishwa bila kuchelewesha na kuonya asije kutokea mfanyakazi yeyote wa kuzembe katika hilo.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kuzungumzia suala hilo, Januari mwaka jana, alimuelekeza katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuwajulisha wanachama wa chama hicho na umma wa Watanzania kuwa anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala unaoendelea juu ya kuongezwa kwa kipindi cha urais kutoka miaka mitano iliyowekwa kwa mujibu wa Katiba, hadi miaka saba.

Aidha, Machi 23 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alimuonya Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia akimtaka kuachana na kampeni ya kutaka muda wa urais kuongezwa akisema ndani ya chama hicho hakuna usultani. Nkamia amekuwa akijitokeza mara kwa mara kutaka muda wa urais uongezwe ili Dk Magufuli akae madarakani muda mrefu zaidi ya ule unaotambulika kikatiba wa miaka mitano katika kipindi kimoja au miaka 10 vipindi viwili.

Maneno matamu sasa ni makavu

Awali, akizindua ujenzi wa barabara ya Mtwara- Tandahimba-Newala mpaka Masasi kwa kiwango cha lami kilomita 50 kati ya 210, Rais Magufuli alisema maneno matamu kwake yaliisha na yamebaki makavu.

“Inawezekana baada ya kutoka kwenye wizara ya ujenzi mmepata mawaziri wanaowaeleza maneno matamu matamu, mimi matamu yalishaisha yamebaki maneno makavu makavu, nawaambia hivyo leo,” alisema Rais Magufuli akizungumzia makandarasi wazembe wasiomaliza kazi kwa muda uliopangwa.

Aliitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutumia sheria na kuwafukuza makandarasi wasiotimiza wajibu wao.

“Wasije Tanzania kufanya majaribio. Hapa ni mahali pa kazi, na niwaombe makandarasi mliosajiliwa katika nchi hii mbadilike. Wale makandarasi wasio perform wafukuzwe, asiye perform vizuri achaneni naye. Tanzania isiwe sehemu ya majaribio.”

Rais Magufuli alisema barabara hiyo itarahisisha usafirishaji wa mizigo kutokana na upanuzi wa Bandari ya Mtwara unaofanywa kwa Sh137 bilioni kuruhusu meli za mafuta kutua na bidhaa nyingine ambazo zitasafirishwa kwenda maeneo mengine ya nchi na nje kama Malawi.

Akizungumza na wakazi wa Naliendele kuhusu utekelezaji wa mradi wa barabara ya kilomita 210 ya Mtwara-Newala-Masasi alisema kuchelewa kukamilika kwake, Rais Magufuli alishangazwa na hatua ya Serikali kutoa zabuni kwa Kampuni ya Dott Services Limited, inayojenga barabara hiyo akisema ina uwezo mdogo.

“Nawafahamu makandarasi wote, huyu haku-perform vizuri kwenye ujenzi wa barabara ya Same- Mkumbara, lakini kwa sababu alishinda tenda, sasa ahakikishe anaimaliza,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alimwagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi nchini (ERB) Profesa Ninatubu Lema kuwadhibiti washauri, “Consultant (mshauri) asiye-perform vizuri achaneni naye, Tanzania isiwe sehemu ya majaribio.

Utafiti

Pia, Rais Magufuli amekitaka Kituo cha Utafiti cha Naliendele kilichopo Mtwara kufanya tafiti zaidi ya zao la korosho ili kujua kama zao hilo linaweza kutengeneza bidhaa nyingi zaidi.“Nimeambiwa mnafanya utafiti pia wa kupata juisi ya korosho, endeleeni kufanya utafiti ili matokeo ya utafiti huu yaendelee kusambazwa kwa wananchi. Kama divai, itengeneze divai ya korosho, kama ni gongo ambayo ni special, itengenezeni itengenezeni iliyopimwa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hata pombe kali zinazokuja ni gongo tu lakini zimepimwa.

“Mnajua tunavidharau sana vitu vyetu lakini ambayo percentage (asilimia) yake inajulikana na kupitishwa katika vipimo vyote vya maabara. Yule anayetaka kulewa kwa dakika mbili analewa tu kwa dakika mbili.”

Aliitaka Wizara ya Kilimo kukiimarisha kituo hicho kwa kukiongezea bajeti ili kiweze kufanya kazi vizuri.

Aliwataka wananchi wa Mtwara kujua kuwa Serikali anayoongoza ipo pamoja nao katika kukuza maendeleo.