Kauli ya Kabudi kuhusu Azory nayo itapita kimya kama ya Lugola?

Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi, juzijuzi alimzungumzia mwandishi wa habari, Azory Gwanda kwa namna iliyoleta tashwishi. Waziri Kabudi, ingawa baadaye alikanusha kuwa hakueleweka vizuri, alimtaja Azory kuwa sehemu ya watu waliopotea na kufariki dunia.

Yalikuwa mahojiano kwa lugha ya Kiingereza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC). Zipo sentensi tatu ambazo waziri huyo alizizungumza ambazo ndizo zilikuwa na sura ya kuleta mwanga, kwamba Azory ambaye alitoweka tangu Novemba 2017, yaani mwaka mmoja na miezi nane iliyopita, alishafariki dunia.

Waziri Kabudi aliulizwa kuhusu kutoweka kwa Azory na mahali alipo sasa. Alijibu, “Let me tell you, when you refer to that matter, that is one of the most painful experiences, that Tanzania went through. In the Rufiji area is not only Azory Gwanda who has disappeared and died.”

Tafsiri yangu ya Kiswahili kwa maneno hayo ni hii: “Ngoja nikwambie, unaporejea jambo hilo, ni moja ya maumivu makali mno ambayo Tanzania ilipitia. Katika eneo la Rufiji si Azory Gwanda peke yake aliyepotea na kufariki. Watanzania wanajua Azory alipotea lakini hawajui alipo. Waziri Kabudi anasema si yeye pekee aliyepotea na kufariki dunia. Je, ilikuwaje waziri akajichanganya kwa kutoa jibu la jumla, au naye amekuwa na wasiwasi kama yu hai au la, ndio sababu alisema hivyo ili kuwaandaa Watanzania kisaikolojia?

Katika mahojiano hayo, Waziri Kabudi pia alisema maneno haya: “Azory Gwanda is part of many other Tanzanians which have been killed in that area.” Tafsiri ya Kiswahili: Azory Gwanda ni sehemu ya Watanzania wengi ambao wameuawa kwenye eneo hilo.

Hapo Kabudi alizungumza kauli iliyonyooka mno, kwamba Azory ni sehemu ya Watanzania wengi waliouawa. Yaani Azory ni sehemu ya Watanzania waliouawa. Kabudi alisema haya maneno kwa bahati mbaya au huo ndio ukweli?

Hakuishia hapo, ipo kauli nyingine: “The state is not only dealing with Azory Gwanda, the state is dealing with all those who have unfortunately died and disappeared in Rufiji, be Azory, of whom leery it is very painful for someone who was doing his job to pass on. And I was a journalist, so I feel so.”

Tafsiri yangu: Dola haishughuliki na Azory Gwanda peke yake, dola inashughulika na watu wote ambao kwa bahati mbaya wamekufa na kupotea Rufiji. Awe Azory, ambaye nadhani inauma sana kwa mtu ambaye alikuwa anafanya kazi yake kufariki dunia. Nami nilikuwa mwandishi wa habari, nahisi hivyo.” Tuiweke vizuri, ni kweli alichosema Waziri Kabudi kuwa dola haiwezi kushughulika na Azory peke yake. Hata hivyo, Kabudi aliweka wazi hisia zake kwa Azory aliyekuwa anafanya kazi yake kufariki dunia, kuwa inauma. Anaongeza uzani kuwa hisia hizo anazo hata yeye kwa sababu pia alikuwa mwandishi wa habari.

Hivi hisia za Waziri Kabudi kama mwandishi wa habari ndizo zilizomfanya aongee hayo? Inabidi waziri ajiulize, kwamba baada ya kusema hayo maneno, nani atamwelewa kuwa hajui na hana taarifa za mahali alipo Azory au alipopelekwa?

Baadaye Waziri Kabudi alikanusha kuwa hakusema Azory ameshafariki dunia. Labda Je, waziri alizungumza hisia zake badala ya ukweli, hivyo kulazimika kukanusha? Nani aliyetazama au kusikiliza yale mahojiano atamwamini?

Bunge la lizinduke

Kama alivyosema Waziri Kabudi, Azory ni sehemu ya Watanzania wengi waliopotea. Alikuwa akifanya shughuli zake ukiwamo uchunguzi wa matukio ya mauaji Kibiti.

Suala lake limeshazungumzwa bungeni mara kadhaa, sawa na Ben Saanane, ambaye alikuwa msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyepotea Dar es Salaam Novemba 2016, mpaka sasa hajapatikana.

Pia, yupo aliyekuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Kigoma, Simon Kanguye, alipotea Julai 2017, hadi leo hajapatikana.

Wapo pia waliotekwa na kupatikana baadaye kama mwanamuziki Roma Mkatoliki na wenzake, walitekwa Dar na kuachiwa Dar, mfanyabiashara Mo Dewji aliyetekwa Dar na kuachiwa Dar; Kada wa Chadema, Mdude Nyagali, aliyetekwa Songwe na kuachiwa Mbeya. Raphael Ongagi, ambaye alikuwa msaidizi wa Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alitekwa Dar na kuachiwa Mombasa, Kenya.

Wa karibuni kabisa ni Allan Kiluvya, msaidizi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, alitekwa Dar na kuachiwa Dar. Ongeza maiti nyingi zilizookotwa katika fukwe za Bahari ya Hindi na Mto Ruvu, ambazo haziwahi kutolewa maelezo.

Haya ni uthibitisho kwamba tatizo la utekaji na watu kupotea ni kubwa na limeenea sehemu mbalimbali za nchi. Si Rufiji peke yake inayotajwa na Waziri Kabudi. Sasa basi, yeyote anayetoa majibu yenye kutoa mwanga wa matukio hayo, anapaswa kuulizwa zaidi asaidie kupata ukweli badala ya kuishia kuwa ametafsiriwa vibaya.

Bunge lina nafasi nyeti ya kumbana Waziri Kabudi ili aseme kama alizungumza bahati mbaya, maneno yalimponyoka kwa kuzongwa na hisia au alitamka ukweli ambao hakutakiwa kuutamka.

Itakuwa ajabu kama Bunge litaacha kauli hii ipite kimyakimya, kama lilivyonyamaza bila kumhoji Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliposema Julai mwaka jana kuwa Azory alikwenda kutafuta maisha.

Dhahiri, Lugola aliuambia umma kuwa Azory alijipoteza kwa kushindwa maisha, alithibitisha kuwa hakutekwa. Bunge lilikaa kimya, halikumhoji Lugola, wakati alionekana anazo taarifa za mahali alipo. Je, na hii kauli ya Kabudi Bunge litaacha ipite?