Kortini kwa kumpa ujauzito dada yake ambaye ni mwanafunzi

Muktasari:

  • Mshitakiwa Gabriel Nyantori (25) leo Jumatatu amefikishwa mahakamani akituhumiwa kwa makosa mawili ikiwamo kuzini na kumpa mimba dada yake.

Serengeti. Gabriel Nyantori (25) amefikishwa mbele ya mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Serengeti mkoani Mara akituhumiwa kwa makosa ya kuzini na dada yake na kumpa mimba.

Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Ismael Ngaile, mwendesha mashitaka, Faru Mayengela leo Jumatatu Januari 14, 2019 amesema mshitakiwa anakabiliwa na makosa mawili.

Amesema kosa la kwanza ni kuzini na dada yake mwenye umri wa miaka (16) mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Kibeyo na kosa la pili ni kumpa mimba dada yake, makosa ambayo aliyatenda Aprili 30, 2018 nyumbani kwao, Kibeyo.

Kesi hiyo ilifika kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali, hata hivyo mshitakiwa amekana mashitaka na kesi imeahirishwa hadi Januari 29, 2019 huku mtuhumiwa akipelewa mahabusu.