Aliyeibua hoja ya taulo za kike amgeukia Waziri Mkuu

Muktasari:

  • Mbunge wa Viti maalum (Chadema), Upendo Peneza ameeleza nia yake ya kurejesha tena hoja yake kuhusu gharama za taulo za kike (Sodo) ili bidhaa hiyo iweze kuuzwa kwa bei nafuu na kugawiwa bure shuleni.

Dodoma. Baada ya Serikali ya Tanzania kupendekeza kufuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika taulo za kike, mbunge wa Viti maalum (Chadema), Upendo Peneza amesema atarudisha upya hoja yake kuhusu gharama za bidhaa hizo ili ziuzwe kwa bei ya chini na kugawiwa bure shuleni.

Peneza ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 19, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

Peneza alipiga kelele kwa muda mrefu kuhusu gharama za taulo za kike hadi Serikali kufikia hatua ya kuziondolea VAT mwaka 2018/19, lakini katika bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020, iliwasilisha pendekezo la kuondoa kodi hiyo kwa kuwa haijaweza kufanya bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei nafuu kwa walengwa na badala yake inawanufaisha wafanyabiashara.

 “Wakati tunaomba taulo bure na elimu bure na kushindikana niliongea na Waziri Mkuu na kunitaka niongee na  wadau mbalimbali kuhakikisha tunapata punguzo katika VAT. Tutarudi kwake tena kuomba suala hili tena lizingatiwe na Serikali.”

“Kigezo ni kimoja tu wizara ya Tamisemi imeshatoa waraka unaoelekeza asilimia 10 ya fedha zinazokwenda kwenye mashule zitumike kununua taulo za kike. Kila mwezi Serikali inapeleka Sh20 bilioni, kwa miezi kumi inapeleka Sh200 bilioni,”amesema Peneza.

Ameongeza, “Ukichukua asilimia 10 ya Sh200 bilioni ni Sh10 bilioni, kama Serikali ikinunua taulo za kike kwa Sh2,500 tunahitaji Sh46 bilioni na kama itanunua kwa Sh1,500 itahitaji Sh28 bilioni kupeleka taulo za kike kwa wanafunzi milioni 1.8 nchi nzima.”

Amesema inawezekana taulo hizo za kike kutolewa bure mashuleni, Serikali kuongeza fedha kidogo.

“Katika Bajeti ya 2018/19 Serikali iliondoa kodi ili wanawake wapate taulo za kike kwa bei nafuu, leo mnatueleza mnarejesha kodi hiyo kwa sababu imeshindwa kuleta matokeo ambayo Serikali iliyategemea.”

“Aprili 23, mwezi huu niliuliza swali bungeni  ni kiasi gani cha kodi ambayo Serikali ilikusanya katika taulo za kike na kujibiwa mwaka 2016/17 ilikusanya  Sh3 bilioni mwaka 2017/18 ilikusanya Sh2.4 bilioni,” amesema.

Amebainisha kuwa Mei 28, 2019 katika siku ya hedhi duniani alikutana na wauzaji wa bidhaa hiyo na waliwaeleza kuwa wauzaji wa jumla na wasambazaji wamepunguza bei za taulo hizo kwa vielelezo.

“Shida ipo kwa wauzaji wa rejareja ndiko ambako bei haijapungua. Kabla ya kuondoa kodi, Serikali ilisikiliza maoni ya wadau mbalimbali, hebu turudi tuzungumze tena kuona namna gani punguzo hili litaonekanaje miongoni mwa wananchi na si kufanya haraka,” amesema.

Mbunge huyo amesema mwaka 2016 na 2018 alichangia bungeni kuhusu taulo za kike na kueleza kuwa kuondoa kodi  haitoshi, kuitaka Serikali kuanzisha mfumo wa namna ya kusimamia maslahi ya walaji wa mwisho.

“Waziri (wa Fedha na Mipango) ameleta upande mwingine kwamba wanapunguza asilimia tano ya kodi ya mapato ya kampuni, hiki kiasi hakitagusa badiliko la bei ya moja kwa moja kwenye taulo za kike. Badiliko hili linagusa faida ya mwisho ambayo muuzaji au mwenye kiwanda anapata. Kama tukiweka kule hatusababishi badiliko la bei la moja kwa moja,” amesema.

Amepongeza pendekezo la Serikali la kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 10 hadi sifuri kwenye malighafi za kutengeneza taulo za watoto, kutaka jambo hilo kufanyika hata katika taulo za kike kwa maelezo kuwa malighafi zinazotumika kutengeneza taulo za watoto ndio zinazotumika kutengeneza taulo za kike.

“Kampuni ambazo Serikali itazipunguzia kodi hizi isimamie bidhaa kwa bei elekezi ili unafuu uonekane moja kwa moja kwa wananchi,” amesema Peneza.